Imeandikwa na Moza Shaaban (ZU)
Kila siku mwanadamu amekuwa akihangaikia afya yake na ustawi wake.
Kwa karne zilizopita, mwanadamu alitumia mimea, mboga mboga na wanyama, ili kuponya magonjwa na maradhi mbali mbali yaliokua yakimsibu.
Kwa vile wakati haugandi, sayansi inayochunguza faida na athari za vitu vya kemikali, kwa matibabu au kuzuia magonjwa, kupunguza maumivu na nyenginezo ilizuka.
Na hapa dawa mbali mbali ambazo ni muhimu kwa matumizi ya binaadamu, zilianza kutengenezwa hususan zile za kemikali, ili kurekebisha au kuboresha hali ya afya ya mtu.
DAWA NI NINI ?
Dawa za binaadamu ni kitu chochote, ambacho binaadamu anatumia kwa lengo la kutibu au kukinga maradhi yasishambulie kinga za mwili.
Zinaweza kuwa katika aina tofauti, kama vile vidonge, sindano, matone, creams au loshan pamoja na za unga unga.
Kwa mfano, dawa za antibiotics hutumiwa kutibu maambukizi ya bakteria, za antiviras hutumiwa kutibu maambukizi ya virusi, na dawa za analgesic hutumiwa kupunguza maumivu.
Kitaalamu dawa haziliwi tu kama njugu, bali kuna matumizi sahihi ambayo mugonja, anatakiwa kuyajua, na sio rahisi kujua bila kupata maelekezo kutoka mtaalamu wa afya.
Kwa lugha nyepesi, Ili dawa ifanye kazi mwilini, ina kiwango maalumu (dozi) na muda wa matumizi yake, iliyoandikiwa mgonjwa kutumia baada ya daktari kuthibitisha ugonjwa uliopo.
Lakini kwa sababu moja au nyingine wapo watu hutumia dawa bila maelekezo ya daktari, na hili limekua kama jambo la kawaida tu,kwani watu wengi humeza dawa bila kuzingatia vipimo.
JE JAMII INAMTAZAMO GANI ?
Hamdu Hassan Bakari (65) wa Mjimbini, anasema udhibiti mdogo wa dawa, ni miongoni mwa sababu zinazo pelekea watu kutumia dawa bila maelekezo ya daktari.
Anasema hakuna udhibiti wa kutosha juu ya upatikanaji wa dawa, na kwa sasa mtu anapojisikia kuumwa, hubisha hodi kwenye maduka ya kuuzia dawa na kununua atakayo.
‘’Baadhi ya maduka ya vyakula yanajihusisha na uuzaji wa dawa kama za antibayotiki (panadoli), ambapo wao hawana usajili rasmi wa kufanya biashara hiyo,’’anaeleza.
Abdull-hamid Shaabani Haji mkaazi wa Vitongoji Chake chake Pemba anasema, kutokumudu gharama za matibabu, ni moja kati sababu zinazo pelekea, watu wengi kutumia dawa bila kupata maelekezo ya daktari.
Rehema Mohamed Makame (45), mkaazi wa Mtambile Mkoani, anaeleza kuwa, usumbufu wanaopata wagonjwa katika baadhi ya hospitali na vituo vya afya, unapelekea watu kutofika hospitalini, ili kueleza magonjwa yanayowasibu, na kasha kujikadiria dawa.
‘’Utamaduni mbovu wa kila mgonjwa kujikadiria dawa, umekuwa ukiathiri kinga za mwili, na kusababisha baadhi ya wakati, dawa nyingine kutofanyakazi mwilini,’’anaeleza.
Hata Sada Mohamed Amour, wa Mjimbini anafafanua kuwa, waliowengi wamekuwa wakitumia dawa kiholela kwa kule kutokujua madhara ndani ya miili yao.
‘’Watu wengi hawana uwelewa wa kutosha kuhusu madhara yanayoweza kujitokeza, iwapo watatumia dawa kiholela bila yakupata maelekezo kutoka kwa wahudumu wa afya,’’anaeleza.
WATAALAMU WA AFYA YA BINADAMU WANASEMAJE?
Rashid Suleiman Ali ambae ni Afisa tabibu kutoka kituo cha afya Kangani Mkoani nasema, athari moja wapo anayoweza kuipata mtu, anaetumia dawa kiholela ni kusababisha usugu wa dawa mwilini mwake ‘Resistance of Drugs’ hapo baadae.
Yussuf Omar Masoud daktari kutoka kituo cha afya Kangani anafafanua kuwa, utumiaji dawa kiholela uaweza kusababisha madhara ya muda mrefu, ikiwemo viungo kupoteza nguvu
‘’Kwa mfano, matumizi ya dawa za usingizi ‘sleeping pills’ ukivitumia bila kufuata maelekezo ya mtaalamu, mwisho wa siku, unaweza kupata ulemavu usiotarajiwa,’’anafafanua.
Nae Maryam Said Abdallah Mfamasia kutoka kituo cha afya cha Buguruni Dar-es-salaam anasema, kutumia dawa bila kufuata maelekezo ya daktari kunaweza kusababisha kuongeza sumu mwilini.
Kwani anabainisha kuwa, dawa hutengenezwa kwa kutumia chembe chembe za kemikali, ambazo kimsingi ni sumu zinazoua vimelea vya ugonjwa, ingawa kwa utaratibu maalum kutoka kwa mtaalamu.
‘’Dawa ni sumu, iliyotengenezwa maalum kwa ajili ya kuua vimelea vya maradhi, ingawa ukiitumia kiholela, inaua hata mtu mwenyewe kwa kule kukosa mpangilio wa kitaalamu,’’anafafanua.
BARAZA LA FAMASIA LINASEMAJE?
Elizabeth Shekalage ambae ni Msajili wa Baraza la Famasia nchini , anaeleza kuwa, madhara ya kutumia dawa kiholela ni pamoja na kuleta ulemavu wa kudumu na hata kusababisha kifo.
Kwani ili dawa ifanyekazi mwilini, inakiwango maalumu (dozi) na muda wa matumizi wa dawa, aliyoandikiwa mgonjwa, kutumia baada ya daktari kuthibitisha ugonjwa uliopo.
Aidha mtaalamu huyo, anasema kuwa, kwa dozi ikiwa kubwa, kunasababisha kuongeza kiwango cha dawa, ambacho hakitakiwi kwenye mwili na huleta madhara ya figo, ulemavu na hata kifo.
MITANDAO YA KIJAMII
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kua, ipo hatari ya idadi kubwa zaidi ya watu kupoteza maisha, kutokana na usugu wa vimelea vya magonjwa aliyetumia dawa holela.
WHO kwenye utafiti wake wa mwaka 2019, limekugundua kuwa, magonjwa sugu dhidi ya dawa, husababisha vifo laki 7 duniani kote kila mwaka.
Ambapo kwa idadi ya vifo hivyo, ni sawa na wastani wa vifo 58,333 kwa mwezi, sawa na vifo 1,944 kwa siku, huku WHO, likiendelea kutahadharisha juu ya ulaji wa dawa kiholela.
Aidha WHO, limeonya kuwa, ikiwa mikakati haitochukuliwa ya kudhibiti watu kujilia dawa ovyo, huwenda ifikapo mwaka 2050, watu milioni 10, ikawa wanapoteza uhai kila mwaka duniani kote.
NINI KIFANYIKE?
Hemed Nassor Mbarouk mkaazi wa Mjimbini Mkoani, anasema ni vyema kwa wizara ya Afya Zanzibar, kutoa elimu kwa wananchi, juu ya athari za matumizi ya dawa kiholela.
Ali Mohamed Makame mkaazi wa Mtambile, anashauri ni vyema kwa wataalamu wa afya, kuimarisha huduma za afya vituoni na hospitalini ili kupunguza tatizo hilo.
Salama Omar Ali mkaazi wa Mchanga mdogo, anashauri kuwa, wizara ya afya Zanzibar, idhibiti uuzwaji dawa kiholela madukani, ili kuhakikisha matumizi ya dawa yanakuwa sahihi kwa mgonjwa.
Rashid Suleiman Ali Afisa tabibu wa kituo cha afya Kangani alisema, ni vyema kwa wagonjwa kufika katika vituo vya afya, ili kupata vipimo na maelekezo sahihi ya madaktari namna ya utumiaji wa dawa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto Tanzania bara Dk. Seif Shekalage alisema, ili kudhibiti athari zinazoweza kujitokeza, ni vyema kwa wamiliki wa maduka ya dawa, wafuate utaratibu sahihi wa utowaji wa dawa kwa wagonjwa.
Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba, Khamis Bilali Ali, anasema ni kosa la kitabibu mgonjwa kujikadiria dawa mwenyewe.
‘’Chakufanya ili kudhibiti hali hiyo, hata wauzaji dawa katika maduka yanayotambulika, wasitowe dawa pasi na buku la mtaalamu wa afya alivyoelekeza,’’anaushauri.
chanzo: https://pembatoday.blogspot.com/2023/09/wanaokula-dawa-kwa-kujikadiria-wenyewe.html
0 Comments