Wakulima wa Mwani Pemba wafunguka kinagaubaga kuhusu zao hilo. Serikali yaja na neema kwao.

Imeandikwa na Abuu Bakar (ZU)

Mwani yaani ‘sea weeds’ ni aina ya zao, lenye mnasaba na kiumbe hai, kinachopatikana baharini pekee.

Kwa uasili wake viumbe hawa, huota na kukua kwenye fukwe zenye asili ya mawe au mchanga mzito, nyasi za baharini na kwenye matumbawe.

 Kwa karne mbili na nusu zilizopita, zao la mwani, halikubeba thamani yake, na lilionekana kama vile ni bustani ya habarini yenye lengo la kuwapendezesha viumbe kama samaki.

Kwa kule kucheza cheza kwao, kufanya mazalio, nyumba, sehemu za mapunziko na chakula kwa baadhi ya viumbe.

Ilionekana, kama vile mwani ni viumbe vinayoota na kufa kila baada ya muda, na hakuna aliyefikiria kuwa, iko siku zao hilo linaweza kuwa sehemu ya kukuza pato la mtu au taifa.

Baada ya kuonekana kuwa na thamani, sasa wataalamu wanatueleza kuwa, ziko aina mbali mbali za mwani, ambazo hutofautiana kutoka ukanda mmoja wa bahari na mwingine.

Kwa mfano Tanzania, kuna aina mbili kuu za mwani, ule unaoitwa “Eucheuma denticulatum” au kwa jina jingine hujulikana kama “Eucheuma spinosum” na aina ya pili inaitwa “Kappaphycus alvarezii”.

 Kwa kwaida mwani huwa na rangi ya kijani, kahawia na nyekundu, ambapo rangi hizo zinasababishwa na kuongezeka au kupungua kwa kina cha maji ya bahari.

Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, imeanisha kuwa, uzalishaji wa zao la mwani umeongezeka kutoka, tani 10,531 kwa mwaka 2021 hadi tani 12,594 kwa mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 20.

Taarifa ikafafanua kuwa, usafirishaji wa mwani nje ya nchi umeongezeka kutoka tani 12,124 kwa mwaka 2021 hadi tani 13,972 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 15.

CHANGAMOTO ZIPI WANAZOZIPATIA WA KULIMA WA MWANI?

Mkulima wa zao hilo kutoka shehia ya Sizini Salma Khamis Juma, anasema hulazimika kufanya jitihada binafsi, ili kuupata mwani, ikiwemo kutembea kwa miguu kwa kuvuuka sehemu zenye hatari.

Changamoto nyingine anasema, sehemu wanazopita kutafuta mwani zina kuwa na tope na visiki vinavyochoma mithili ya misumiri, ambapo huwakumba wao, wasio na viatu vya kinga.

‘’Mwani hata ukifika nao juu kwa ajili ya kuuwanika, umeshapitia kadhia kadhaa, na wakati mwengine unaweza kushindwa kurudia siku nyingine kwa miguu kupata majeraha,’’anaeleza.

Haisau siku aliyongia kwenye dimbwi lenye tope, na kuzama mpaka magoti, wakati anarudi kuvuna mwani shambani kwake, na kuokolewa na mwenzake.

Mkulima Raya Ali Bakar wa Shehia hiyo ya Sizini wilaya ya Micheweni, anaeleza kuwa, kama sio shujaa wa kweli, ni vigumu kwa mwanamke kujiingiza kwenye kilimo cha mwani.

Anaona kuwa machungu, shida, kadhia ya kuuza roho inayowakabili wakulima wa mwani, ni vyema ikaenda samba mba na bei husika.

‘’Sisi wanawake ambao tumejiingiza kwenye kilimo cha mwani, ni sawa na kuuza maisha yetu kila siku, na huku ukiangalia bei nayo inaumiza kama matayarisho ya kilimo chenyewe,’’anaeleza.

Ali Salim Bakar, anaeleza kuwa kilimo cha mwani hawezi kukifafanisha na kilimo chochote chenye tija na taifa, kutokana na ugumu uliopo wakati wa matarisho yake.

Kule kulimwa ndani maji, kushughulikiwa ndani ya maji na hata kuvunjwa ndani ya maji ni ishara kuwa, kilimo hicho kinaishi pamoja na changamoto zake.

‘’Kila mmoja anasema kama akipata kazi nyingine anaweza kukihama kilimo cha mwani, maana machungu ni makubwa ingawa bei haiendani na kazi zake,’’anaeleza.

Zainab Ali Bakar, anasema ukosefu wa vifaa kinga, vidau vya kusafirishia mwani, bei na wizi unawakosesha furaha katika kazi yao ya kilimo cha mwani.

 UONGOZI WA SHEHIA YA SIZINI

Sheha wa shehia ya Sizini Suleiman Shaame Hamad, anasema wakulima wengi wanaoendesha kilimo hicho ni wanawake, hivyo ni vyema wakaangaliwa kwa jicho la huruma.

‘’Naelewa kuwa, kwa sasa serikali inayomikakati kabambe ya kuhakikisha, wakulima wa mwani wanasahau machungu wanayopata kwenye kilimo hicho,’’anaeleza.

Sheha anawakumbusha wakulima wa zao hilo, kuwa nao watakuwa juu kama walivyowakulima wa zao la karafuu, hasa baada ya uwepo wa kiwanda cha kusarifia mwani Chamanangwe.

Afisa Uvuvi Wilaya ya Micheweni Abdalla Issa Nassor, anasema kuwa wakulima wanakabiliwa na changamoto nyingine inayowakabili wakulima hao ni ya maradhi kwa mwani wao.

Jambo hilo hufanya mwani kuharibika, na kuwafanya wakulima wa zao hilo, kutokufikia malengo yao waliyojiwekea.

Kutokana na changamoto hizo miradi mbali mbali  imeanzishwa kuwasaidia vikundi tofauti, ikiwemo mradi wa IUCN ambao makao makuu yake yapo Dar es Salam, ambapo mradi huo husaidia sehemu mbili kwa Pemba, Mkoani na Micheweni.

Kwa upande wa Micheweni Umesaidia kikundi cha Mikoko, kinachoitwa Shirikani Coparetive Society, kikundi cha Ufugaji wa samaki kinachoitwa Mapambano Coparetive Society na kikundi cha mwani Tuelewane kilichopo kinowe.

SERIKALI KUU INASEMAJE

Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Suleiman Massoud Makame anasema kwa mwaka huu wa fedha, mkazo zaidi umewekwa kwenye maendeleo ya viwanda vya kusarifu samaki, mwani na mazao mengine ya bahari.

 Aidha anasema machungu wanayoyapata wakulima wa mwani wa Unguja na Pemba, yataondoka karibuni kuwatafutia mikakati ya vitendo iliyowekwa na serikali ya awamu ya nane, ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha kusarifia mwani.

Akisoma taarifa ya kitaalamu wakati mwenge wa uhuru ulipotembelea Juni mwaka 2023, Mkurugenzi mkuu Kampuni ya mwani Zanzibar Massoud Mohamed Rashid, anasema ujenzi wa kiwanda hicho umefikia hatua nzuri.

Alieleza kuwa, ujenzi huo ambao unajengwa na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar ‘KMKM’ uko katika awamu ya kwanza, kati ya zile tatu hadi kukamilika kwake.

Alieleza kuwa, awamu ya kwanza inajumuisha ujenzi wa jengo kuu la kiwanda, ujenzi wa ghala pamoja na uzio maalum kwa ajili ya kulihifadhi eneo hilo.

‘’Awamu ya pili utajumuisha ujenzi wa maeneo ya bustani, ufungaji wa mitambo husika na awamu ya tatu ni kuanza uzalishaji bidhaa zitokanazo na mwani,’’aliwaeleza wakimbiza mwenge kitaifa.

Kwa wakati huo, tayari ujenzi huo wa awamu ya kwanza umeshafikia asilimia 86, na ukitarajiwa kutumika shilingi bilioni 8.2 ingawa wameshatumia shilingi bilioni 4.024 na utakapomalizika wote, utagharimu shilingi bilioni 13.

‘’Mradi huu wa kiwanda, utakapomalizika utakuwa na uwezo wa kusarifu mwani tani 30,000 kwa mwaka, ambapo umiliki wake kwa asilimia 55 utakuwa serikalini na asilimi 45 utakuwa wa kampuni ya Nutri-san.  

Taarifa kutoka wizara ya Uchumu wa Buluu na Uvuvi Zanzibar, zinaeleza kuwa, usafirishaji wa mazao ya baharini ikiwemo matango bahari, mwani, dagaa, kaa na pweza umeongezeka kutoka tani 19,063 mwaka 2021 hadi tani 23,158 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 21.

Uzalishaji wa zao la mwani nao umeongezeka kutoka tani 10,531 mwaka 2021 hadi tani 12,594 kwa mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 20.

Huku pia ikianishwa kuwa, usafirishaji wa mwani nje ya nchi umeongezeka kutoka tani 12,124 mwaka 2021 hadi tani 13,972 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 15.


chanzo: https://pembatoday.blogspot.com/2023/09/wanawake-walima-mwani-pemba-wadadaua.html

Post a Comment

0 Comments