Miaka 25 ya Kujitolea Bila Darasa: Safari ya Asha Issa Muhammed ya Kuvunja Vikwazo kwa Watu Wenye Uziwi Zanzibar

NA-FATMA SULEIMAN-PEMBA 
Kwa zaidi ya robo karne, Asha Issa Muhammed ameandika historia ya kipekee katika mapambano ya kuhakikisha watu wenye uziwi hawabaki nyuma katika kupata elimu, taarifa na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii. 
Bila kuwa na ofisi rasmi wala darasa la kudumu, amekuwa akiendelea kufundisha Lugha ya Alama na elimu mjumuisho kwa moyo wa kujitolea.

Asha mwenye umri wa miaka 55 ni mkazi wa Vitongoji, Chake Chake, Pemba na mama wa watoto watatu. Alianza kufanya kazi katika Umoja wa Watu Wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ) mwaka 1991 akiwa mfanyakazi wa kawaida.
 Kutokana na mapenzi yake kwa watu wenye ulemavu, baadaye alijikita katika kuwahudumia watu wenye uziwi na kujifunza Lugha ya Alama.

Safari yake ilianza pale alipoteuliwa kushiriki mafunzo ya siku kumi kupitia mpango wa majaribio wa shule maalumu (Pilot School) uliowashirikisha walimu kutoka Tanzania Bara.
 Baada ya kurejea Pemba hakuridhika na elimu hiyo pekee, akaenda kuendelea kujifunza katika Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) jijini Dar es Salaam, hatua iliyomjengea uwezo wa kuwa mkalimani na mwalimu wa Lugha ya Alama.
Leo hii Asha si mwalimu tu bali ni mlezi, mshauri na kiongozi anayehakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki ya kuelewa na kueleweka.

Anasema lengo lake ni kuwafundisha walimu wa Lugha ya Alama pamoja na watu wenye ulemavu ili wasiachwe nyuma katika kupata elimu, huduma za afya, haki, ajira na taarifa muhimu zinazogusa maisha yao.
Kwa sasa anaendesha darasa lenye wanafunzi 28.
 Darasa hilo hutoa mafunzo ya Lugha ya Alama, elimu mjumuisho, ujasiriamali pamoja na mfumo wa kuweka na kukopa unaowasaidia wanafunzi kujijengea uwezo wa kiuchumi.
Miongoni mwa wanafunzi wake ni Asha Juma Said, ambaye anasema ndoto yake ni kuwa miongoni mwa watu watakaosaidia kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa kikamilifu katika jamii.

"Ninajifunza Lugha ya Alama kwa sababu naamini kila mtu ana haki ya kuelewa na kueleweka. Natamani kuwa sehemu ya mabadiliko hayo," anasema.

Mnufaika mwingine ni Haitham Yunus Yahya, mwanamke mwenye ulemavu wa uziwi ambaye anaendelea na masomo katika darasa hilo. Haitham anasema jambo analojutia ni kuchelewa kujiunga na mafunzo hayo.

"Laiti ningeanza mapema, ningekuwa mbali zaidi. Lakini bado nina matumaini kwa sababu nimepata mwalimu anayejitoa kwa dhati," anasema.

Pamoja na mafanikio hayo, Asha anakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa sehemu rasmi ya kufundishia.

"Nimetembelea ofisi nyingi kuomba hata chumba kimoja kwa ajili ya kuendesha shughuli zetu lakini sijafanikiwa. Hivi sasa tunafundisha mara moja kwa wiki katika eneo la Mkanjuni Istiqama, jambo linalotufanya tushindwe kuongeza siku za masomo," anasema.

Anaongeza kuwa hata kikundi chao cha kuweka na kukopa bado hakijafikia uwezo wa kutoa mikopo kwa wanachama kutokana na mtaji mdogo.

Licha ya changamoto hizo, mafanikio yake yanaonekana wazi. Wanafunzi wengi aliowafundisha tayari wanatumia Lugha ya Alama katika kuwahudumia watu wenye ulemavu, huku wengine wakihamasisha jamii kujifunza lugha hiyo.

Kwa Asha, mafanikio makubwa ni kuona mtu mwenye uziwi akipata nafasi ya kushiriki katika elimu, hospitali, mikutano ya kijamii na huduma nyingine bila kutengwa kwa sababu ya ukosefu wa mawasiliano.

Kwa upande wa hali halisi Zanzibar, bado kuna uhaba wa wakalimani wa Lugha ya Alama katika taasisi nyingi za umma. Tafiti zimeonyesha kuwa pamoja na uwepo wa baadhi ya walimu na wakalimani katika shule maalumu, bado kuna changamoto ya uhaba wa wataalamu, vifaa vya kujifunzia na mafunzo endelevu.

Aidha, tafiti na wadau wa sekta ya ulemavu wamekuwa wakieleza kuwa huduma za ukalimani bado hazijafikia kiwango kinachohitajika katika hospitali, mahakama, vyombo vya habari na ofisi za umma, jambo linalowafanya watu wenye uziwi kushindwa kupata huduma kwa usawa.

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeanza kuchukua hatua za kuimarisha elimu mjumuisho. Mwaka 2026, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ilisaini makubaliano ya miaka mitano yenye thamani ya shilingi bilioni tatu kwa kushirikiana na Norwegian Association of Disabled (NAD), yakilenga kuboresha elimu mjumuisho, kuongeza matumizi ya Lugha ya Alama shuleni na kuwajengea uwezo walimu.

Kwa upande wa Tanzania kwa ujumla, Serikali imeeleza kuwa wakalimani 300 wa Lugha ya Alama wameshasajiliwa katika kanzidata rasmi, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za ukalimani katika taasisi mbalimbali.

Hata hivyo, kwa Zanzibar bado hakuna takwimu rasmi za umma zinazoonyesha idadi kamili ya walimu na wakalimani wa Lugha ya Alama, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuwa na mfumo rasmi wa usajili na takwimu.
Asha anaamini mafanikio ya kweli yatapatikana pale jamii itakapobadili mtazamo kuhusu ulemavu.

"Watu wenye ulemavu hawahitaji huruma, wanahitaji fursa. Wajifunze Lugha ya Alama, wawakaribishe katika shughuli za maendeleo na wahakikishe hakuna anayeachwa nyuma," anasisitiza.

Baada ya zaidi ya miaka 25 ya kujitolea, Asha Issa Muhammed ameendelea kuwa mfano wa uongozi wa kujitolea. Bila ofisi, bila darasa la kudumu na bila rasilimali za kutosha, ameendelea kujenga daraja la mawasiliano kati ya jamii na watu wenye uziwi.

 Historia yake inaonyesha kuwa mabadiliko makubwa huanza na mtu mmoja mwenye maono, moyo wa kujitolea na imani kwamba kila binadamu anastahili kusikilizwa na kueleweka.
MWISHO.

Post a Comment

0 Comments