CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI WATOTO WA KIKE KATIKA KUPATA ELIMU KASKAZINI A UNGUJA
Na Tatu Juma Zanzibar
Elimu ni haki ya msingi kwa kila mtoto bila kujali jinsia. Hata hivyo, katika jamii nyingi, watoto wa kike bado wanakumbana na changamoto mbalimbali zinazowazuia kupata elimu sawa na ile wanayoipata wavulana. Miongoni mwa changamoto hizo ni mzigo mkubwa wa kazi za nyumbani na ushiriki katika shughuli za kilimo, hali inayochangia baadhi yao kushindwa kuhudhuria masomo ipasavyo au kuyaacha kabisa.
Katika familia nyingi, watoto wa kike hutegemewa kufanya kazi mbalimbali za nyumbani kama kupika, kufua, kuchota maji, kulea wadogo zao, kusafisha nyumba na kuwahudumia wagonjwa. Kutokana na hali hiyo, hulazimika kuamka mapema kutekeleza majukumu kabla ya kwenda skuli, jambo linalowafanya baadhi yao kuchelewa au kukosa vipindi vya masomo.
Mbali na hilo, wanaporudi nyumbani baada ya masomo huendelea na kazi hizo hadi usiku, hali inayowapunguzia muda wa kujisomea na kufanya kazi za skuli. Matokeo yake ni kushuka kwa kiwango cha ufaulu na wakati mwingine kuacha masomo kabisa.
Changamoto nyingine ni ushiriki wao katika shughuli za kilimo, hasa katika maeneo ya vijijini. Watoto wengi hushirikishwa katika kulima, kupanda, kupalilia na kuvuna mazao. Wakati wa msimu wa kilimo au mavuno, baadhi ya wazazi huona ni muhimu zaidi watoto kusaidia shambani kuliko kwenda skuli. Watoto wakike huathirika zaidi kwa kuwa mara nyingi hubeba majukumu ya nyumbani na kilimo kwa wakati mmoja.
Mkurugenzi wa Elimu Mbadala na Elimu ya Watu Wazima, Bi. Mashavu Ahmada Fakih, amesema miongoni mwa mikakati ya Serikali za Tanzania na Zanzibar ni kuiwezesha jamii kielimu kwa kuwapatia fursa watoto na vijana waliokatiza masomo ili waweze kupata elimu na ujuzi wa kujikomboa kiuchumi.
Bi. Mashavu aliyasema hayo alipokuwa akikabidhi baiskeli kwa wanafunzi waliokatiza masomo kutokana na sababu mbalimbali na ambao kwa sasa wamejiunga na darasa maalumu la elimu mbadala katika eneo la Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A, Unguja.
Alisema lengo la mpango huo ni kuwawezesha vijana kujua kusoma, kuandika, kufanya hesabu pamoja na kupata ujuzi wa ujasiriamali.
"Tuna mikakati mingi ya kuwasaidia vijana waliopo nje ya mfumo rasmi wa elimu. Tunaamini kuwa ujuzi hauzeeki. Hapa Mkwajuni tunatoa mafunzo mbalimbali ikiwemo ya kuendesha bodaboda kwa wanaume na wanawake," alisema Bi. Mashavu.
Aliongeza kuwa baadhi ya vijana wa kike wamejifunza kuendesha bodaboda, kutengeneza sabuni, uchoraji, ufundi umeme, utunzaji wa nyumba na udobi, na miongoni mwa fani nyingine zinazowawezesha kujitegemea.
Naye Afisa Elimu Wilaya ya Kaskazini A, Bw. Juma Mwadini Abdallah, amesema licha ya jitihada zinazofanywa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, bado baadhi ya wazazi hawajatoa ushirikiano wa kutosha katika kuwahamasisha vijana kurejea masomoni.
Alisema wazazi wengi huvutiwa na shughuli za utalii kwa kuwa zinatoa kipato cha haraka, jambo linalowafanya baadhi yao kutotilia maanani umuhimu wa elimu kwa vijana wao.
"Tumezunguka katika shehia zote za Wilaya ya Kaskazini A kutoa mwamko kwa wazazi na vijana kuhusu umuhimu wa elimu mbadala. Kupitia juhudi hizo tumefanikiwa kuwaibua vijana wengi walioacha masomo na kuwapatia nafasi ya kuendelea na elimu pamoja na mafunzo ya stadi za maisha," alisema.
Alibainisha kuwa maeneo ya Kijini, Kidombo, Mkwajuni na Kidagoni yana idadi kubwa ya vijana waliojiunga na programu hiyo.
Mwalimu wa Skuli ya Mkwajuni Msingi B, Bw. Bakari Khamis Mussa, alisema kuwa bado kuna baadhi ya watoto wanaokosa msukumo wa elimu kutokana na wazazi wao kutothamini umuhimu wake.
Kwa upande wake, Kaimu Sheha wa Donge Kipange, Bw. Rajab Said, amewashauri wanafunzi walioacha masomo kujiunga na programu za elimu mbadala ili kupata elimu na stadi mbalimbali zitakazowasaidia kukabiliana na changamoto za maisha.
Amesema viongozi wa shehia wanaendelea kufanya juhudi za kuwatafuta na kuwahamasisha vijana waliokatiza masomo na kujishuhulisha na kazi tofauti ili warejee katika mfumo wa elimu.
Mwanafunzi Jamila Omar Muhammed, mwenye umri wa miaka 18 mkazi wa Chaani Juwakuu, alisema, aliacha masomo baada ya kufika darasa la form 4 kutokana na wazazi kukosa ada ya malipo yakumuendeleza na masomo na kuamua kubaki nyumbani akijishughulisha na kazi za nyumbani pamoja na kilimo.
Jamila amesema kujiunga kwake na darasa la elimu mbadala kumemsaidia kwa kiasi kikubwa kwani sasa ana uwezo mzuri wa kusoma na kuandika, pamoja na kupata maarifa ya ujasiriamali.
"Nina matumaini ya kujiajiri baada ya kumaliza mafunzo haya na kupata kipato halali kitakachonisaidia kujitegemea," alisema.
Naye Bi. Mbaki Haji wa Haji, mkazi wa Muange, alisema binti yake aliacha masomo akiwa darasa la saba amejiunga na elimu mbadala na kwa sasa anaonesha mafanikio makubwa katika masomo hayo.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010, inaeleza kuwa Serikali inapaswa kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa sawa katika elimu bila ubaguzi wa kijinsia.
Ripoti ya UNICEF, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar na NBS kuhusu kazi za watoto imeonyesha kwamba:
Asilimia 7.6 ya watoto wenye umri wa miaka 5–17 Zanzibar walikuwa wanajihusisha na kazi mwaka 2021.Kazi nyingi za watoto zilikuwa katika kilimo kisicholipwa cha familia na asilimia 75.9 ya watoto Zanzibar walikuwa wakifanya kazi za nyumbani (kupika, kufua, kutunza watoto, kusafisha n.k.).
Mashirika ya kiraia yamekuwa mstari wa mbele kutetea haki ya mtoto wa kike kupata elimu. Miongoni mwa mashirika hayo ni Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA Zanzibar), ambacho kimechangia kwa kiasi kikubwa katika kampeni za kutetea haki za wasichana kupata elimu.
Mkurugenzi Mstaafu wa TAMWA Zanzibar, Dk. Mzuri Issa, aliongoza juhudi za kupinga sheria zilizokuwa zinawaadhibu wanafunzi wa kike waliopata ujauzito.
"Karibu nchi nzima ilikuwa inaunga mkono sheria hiyo kali kwa kuamini kuwa ingewazuia wasichana kujihusisha na ngono, lakini watu walikuwa wanasahau kuwa mtoto wa kike anakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ubakaji, umaskini, ukosefu wa ulinzi na shinikizo kutoka katika mazingira yanayomzunguka." Alisema Dr Mzuri.
Kwa sasa, TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na UN Women na Ubalozi wa Norway inatekeleza mradi wa miezi minane unaojulikana kama "Tunaweza Pamoja", unaolenga kuwawezesha wanawake na watoto wakike kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Ili kupunguza tatizo la watoto wa kike kukosa elimu kutokana na kazi za nyumbani na shughuli za kilimo, jamii inapaswa kubadili mtazamo kuhusu mgawanyo wa majukumu ya kifamilia. Wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto wote, wavulana na watoto wakike wanapata nafasi sawa ya kusoma.
Serikali, walimu, viongozi wa dini na jamii pamoja na mashirika mbalimbali wanapaswa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike.
Kwa kumalizia, kazi za nyumbani na shughuli za kilimo zimeendelea kuwa miongoni mwa sababu zinazowazuia watoto wakike wengi katika Wilaya ya Kaskazini A Unguja kutimiza ndoto zao za kielimu. Ushirikiano wa familia, jamii na serikali unahitajika ili kuhakikisha kila mtoto wa kike anapata haki yake ya elimu na nafasi ya kujenga maisha bora ya baadaye.
0 Comments