Na-Fatma Suleiman-Pemba
Juhudi za kufanya biashara, utayari katika kusimamia bidhaa zake, Uchangamkiaji fursa za Maendeleo, Changamoto kutokumrudisha nyuma, fursa ushiriki katika nafasi za uongozi , uaminufu ndio siri iliyojificha kwa aisha.
WADI ya Tibirinzi yenye wakaazi 5138 Wilaya ya Chake Chake mkoa kusini Pemba ndipo ambapo nilimuibua Aisha Ali Abdalla Mfano wa kuigwa na wanajamii wadi hiyo ambayo ina wanawake wapatao 2649 kwa uthubutu wake katika kutimiza ndoto na malengo yake aliyojiwekea ya kuwa mfanya biashara.
JEE AISHA NI NANI?
Aisha mwenye Umri wa miaka 33 ambae ni mjasiriamali wa bidhaa za urembo aina ya Mafuta ya haliudi huianza siku yake kwa kusimamia biashara ya mikoba, viatu na mafuta ya haliudi anayoyatengeneza na kuyasambaza kwa wateja mbalimbali ndani ya kisiwa cha Pemba.
Ingawa ni mwenye ulemavu wa macho, yaani haoni kabisa ,anaongoza biashara yake kwa mafanikio kupitia nidhamu, uzoefu na ushirikiano wa wasaidizi wake sambamba na matumaini ya kufikia maendeleo aliyojiwekea
Lakini nyuma ya mafanikio hayo kuna simulizi kubwa zaidi ya juhudi za wanawake wenye kuutafuta uongozi.
Na watu wenye ulemavu wanavyolazimika kufanya kazi kwa bidii mara mbili zaidi ya wasio na ulemavu ili kuthibitisha uwezo wao katika uchumi na uongozi.
Uchunguzi huu umebaini kuwa licha ya kuwepo kwa sheria zinazolinda haki za watu wenye ulemavu, wanawake wengi wenye ulemavu bado wanakabiliwa na vikwazo vya kijamii, kiuchumi na kisiasa vinavyowazuia kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu maisha yao.
Aisha anasema changamoto kubwa si ulemavu wake bali mtazamo wa jamii.
CHANGAMOTO
Anaeleza kuwa mara nyingi watu humuona kama mtu anayehitaji kusaidiwa badala ya mtu mwenye uwezo wa kuajiri wengine, kuendesha biashara na hata kuongoza.
Alipoamua kugombea nafasi ya Mwakilishi wa Viti Maalumu Mkoa wa Kusini Pemba mwaka 2020, alikumbana na maswali yaliyolenga zaidi ulemavu wake kuliko uwezo wake wa kiuongozi.
Baadhi walihoji angewezaje kuhudhuria vikao, kusoma nyaraka au kuongoza wananchi akiwa haoni.
Kwa Aisha, maswali hayo yalionyesha kuwa tatizo halikuwa uwezo wake bali mitazamo hasi iliyojengeka Hali hiyo si ya Aisha pekee.
Mwanaharakati wa wanawake na uongozi Fat-hiya Mussa Said anasema wanawake wenye ulemavu hukabiliwa na ubaguzi wa aina mbili.
" Kwanza kwa sababu ni wanawake, pili kwa sababu wana ulemavu. Mchanganyiko huo huwafanya washindwe kupata fursa sawa za kugombea nafasi za uongozi, kupata rasilimali za kampeni na hata kuaminiwa na jamii.
WASEMAJE WADAU KUHUSU AISHA.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa ZANAB Wilaya ya Chake Chake, Suleiman Mansour Suleiman, bado kuna ongezeko dogo la watu wenye ulemavu wanaojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Mwaka 2020 wanachama watatu wa ZANAB walijitokeza kugombea nafasi za uongozi, hatua aliyosema ilikuwa mwanzo mzuri lakini bado idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji halisi.
Mratibu wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Kisiwani Pemba, Mashavu Juma Mabrouk, anasema serikali imeendelea kuweka mazingira ya kuwawezesha watu wenye ulemavu kupitia mikopo, mafunzo na sera za ushirikishwaji.
Hata hivyo anakiri kuwa utekelezaji wake unahitaji kuongezwa ili wanawake wengi zaidi wanufaike.
KUMBUKUMBU NYARAKA NA WATU WENYE ULEMAVU.
Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Namba 8 ya mwaka 2022, kifungu cha 28, kinahakikisha haki ya watu wenye ulemavu kushiriki katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Aidha, Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2006 katika Ibara ya 29 unazitaka nchi wanachama kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika maisha ya kisiasa na ya umma bila ubaguzi.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 pia inalinda misingi ya usawa, haki na kutobaguliwa, wakati Mkataba wa Kutokomeza Aina Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake wa mwaka 1979 unazitaka nchi kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa katika kushiriki maamuzi ya kisiasa na maendeleo.
Licha ya uwepo wa mifumo hiyo ya kisheria, uchunguzi unaonyesha bado kuna pengo kati ya sheria na utekelezaji wake. Wadau wa watu wenye ulemavu wanasema kampeni nyingi za kisiasa bado hazijazingatia mahitaji ya wanawake wenye ulemavu, huku baadhi ya mikutano na taarifa za uchaguzi zikiendelea kutokuwa rafiki kwao.
Kwa upande wa uchumi, Aisha amethibitisha kuwa uwezeshaji wa wanawake wenye ulemavu unaweza kuleta matokeo makubwa.
Mbali na kujipatia kipato, biashara yake imekuwa chanzo cha ajira na imechangia kuinua kipato cha familia yake.
Hata hivyo, anasema upatikanaji wa mitaji, masoko na teknolojia rafiki bado ni changamoto kwa wanawake wengi wenye ulemavu.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, TAMWA Zanzibar kupitia programu ya Women Leadership for Equality, Accountability and Democracy (W LEAD) inaendelea kuwajengea uwezo wanawake vijana na wanawake wenye ulemavu kushiriki katika uongozi na michakato ya kufanya maamuzi.
Programu hiyo inalenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi na kuchochea usawa wa kijinsia katika uongozi.
Uchunguzi huu unaonyesha kuwa simulizi ya Aisha si hadithi ya mtu mmoja pekee. Ni kioo kinachoonyesha changamoto zinazowakabili wanawake wengi wenye ulemavu pamoja na fursa zinazoweza kupatikana pale ambapo sheria zinatekelezwa, jamii inabadilisha mtazamo na taasisi zinawekeza katika uwezeshaji wao.
Kwa wataalamu wa maendeleo ya jamii, njia ya kuongeza ushiriki wa wanawake wenye ulemavu si kutunga sheria mpya pekee, bali kuhakikisha sheria zilizopo zinatekelezwa, taarifa za uchaguzi zinapatikana kwa njia zinazowafikia wote, huduma za kifedha zinakuwa jumuishi, na jamii inaendelea kuelimishwa kuwa uongozi unapimwa kwa uwezo, maadili na maono, si kwa hali ya mwili wa mtu.
Safari ya Aisha Ali Abdallah inaacha swali moja muhimu kwa jamii na watunga sera.
Ikiwa mwanamke mwenye ulemavu wa macho ameweza kujenga biashara, kuajiri watu na kuthubutu kugombea nafasi ya uongozi licha ya vikwazo vingi, ni nini kinachozuia wanawake wengine wenye uwezo kama wake kupata nafasi sawa za kushiriki katika kujenga uchumi na kuamua mustakabali wa Zanzibar .
Makala hii iwe ni mabadiliko kwa watunga sera na wasaidizi wa watu wenye ulemavu kuwasimamia ili kuzifikia fursa mbali mbali ikiwemo za Uongozi , kuwezeshwa na kuwasimamia kupata fursa mbali mbali za maendeleo.
MWISHO
0 Comments