SHERIA MPYA YA ARDHI KUPUNGUZA MIGOGORO NA KUTOA UHAKIKA KWA UWEKEZAJI

NA-FATMA SULEIMAN-PEMBA. 
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Rashid Hadid Rashid amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara ya Ardhi inatayarisha Sheria mpya ya Sekta ya Ardhi yenye lengo la kupunguza migogoro ya ardhi inayoongezeka.
Amesema hayo leo katika Ukumbi wa wizara ya fedha gombani katika kikao cha majadiliano ya wadau wa  Serikali kuhusu Sheria ya Sekta ya Ardhi.

RC amesema ongezeko la migogoro hiyo linasababishwa na kasi ya uwekezaji unaoendelea Zanzibar tangu mwaka 1986  hivyo ni lazima kuwe na sheria madhubuti itakayolinda haki ya kila mtu na  kutoa uhakika kwa wawekezaji. 

"Sasa hivi migogoro ya ardhi imekuwa mingi sana Zamani haikuwa hivi Tunahitaji Sheria ambayo itaweka mstari," 

Aidha RC amesisitiza kuwa wadau wa serikali wana wajibu wa kuhakikisha rasimu hiyo inakamilika kwa wakati ili kupatikana suluhu za changamoto zilizopo.

 Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, Anad Bakar Hamad amesema lengo la kuwakutanisha wadau hao ni kuwapa uelewa kuhusu Sheria mpya ili kufika katika jamii kwa haraka

 Mwezeshaji na Mwanasheria Ali Ali Hassan amesema sheria zilizopo kwa sasa hazitoshi kukabiliana na changamoto zilizopo katika masuala ya ardhi kutokana na mahitaji ya uwekezaji wa kisasa ulivyokuwa.

 "Tulipokuwa tunataka kusimamia tuligundua sheria zetu za ardhi hazijakidhi haja Wawekezaji waliuliza mnasimamia kwa sheria gani? Tulikuwa hatuna jibu la kutosha," 

Ali Hassan ameongezea kuwa Sheria mpya ikipita itarahisisha upatikanaji wa hati za umiliki kupitia mfumo wa kidigitali na pia itapunguza kesi za migogoro ya ardhi.
 "Tumekusanyika hapa kama wadau wa serikali ili tupitie rasimu hii kwa undani na kutoa mapendekezo yatakayoiimarisha zaidi

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, Hamad Khatib Saleh amesema changamoto kubwa iliopo  ni ukosefu wa takwimu sahihi za ardhi.

Hamad amesema halmashauri zinajua majukumu yao lakini zinapata tabu katika utekelezaji kutokana na kukosa taarifa sahihi.

 "Tusipokuwa na takwimu sahihi tutaendelea kuwa na migogoro. Kwa hiyo ombi letu ni sheria hii iangalie namna ya kupata taarifa sahihi ngazi ya chini,"
Zawadi Saidi Ali ambaye ni mmoja wa wadau kutoka Serikalini amesema Sheria mpya ya Sekta ya Ardhi inapaswa kuwa na utaratibu maalum wa kumaliza migogoro ya ardhi haraka.

Zawadi amebainisha kuwa kwa sasa wananchi wengi wanateseka kutokana na migogoro ya ardhi inayodumu kwa muda mrefu bila ufumbuzi. "Tunapendekeza sheria hii iwe na utaratibu wa dharura wa kutatua migogoro. Mtu asikae miaka 5 kwenye kesi ya shamba," amesisitiza.

Post a Comment

0 Comments