UAJ YAHITIMISHA KOZI YA 63 CAIRO KWA WITO WA KUZINGATIA UKWELI NA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA VYOMBO VYA HABARI BARANI AFRIKA



CAIRO- FATMA SULEIMAN 

 Muungano wa Waandishi wa Habari wa Afrika, UAJ, umehitimisha rasmi Kozi yake ya 63 ya Mafunzo "Mahfouz El-Ansary" huko Cairo  huku waandishi wachanga wakihimizwa kuzingatia uandishi wa habari wa kweli na kuimarisha umoja wa kitaaluma Afrika nzima.
Kozi hiyo ya wiki tatu ambayo ilifadhiliwa na Serikali ya Misri kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ambapo iliandaliwa na UAJ kwa kushirikiana na Baraza Kuu la Udhibiti wa Vyombo vya Habari ilishirikisha waandishi na wataalamu wa vyombo vya habari kutoka nchi mbalimbali za Afrika .

Akifunga kozi hiyo, Rais wa UAJ na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Al-Ahram, Dkt. Mohamed Fayez Farhat, alisisitiza kuwa mafunzo na mawasiliano kati ya waandishi wa habari wa Afrika ni njia muhimu zaidi ya kujenga madaraja ya ushirikiano kati ya nchi za Afrika.
"Tunashukuru Misri kwa ukarimu na fursa hii kwani tumeshuhudia udugu na ushirikiano kati ya waandishi wa habari wa Afrika, Tunatarajia matokeo haya yaonekani katika vyombo vyetu vya habari," alisema Dkt. Farhat.

Aliongezea kuwa ni muhimu kuendeleza ujuzi waandishi ili kuendana na mabadiliko ya haraka sekta ya vyombo vya habari, hasa kwa kuzingatia maendeleo ya kiteknolojia na matumizi yanayoongezeka ya akili bandia.

Mshauri Reem Hindi, Mwanachama wa Sekretarieti Kuu ya Baraza Kuu la Udhibiti wa Vyombo vya Habari, alisisitiza umuhimu wa kuendelea na ushirikiano kati ya Baraza na UAJ ili kuimarisha uwezo wa kitaaluma waandishi na kukuza uzingatiaji wa maadili ya vyombo vya habari. 

Alithibitisha kuwa Misri ina hamu ya kuunga mkono mawasiliano na ushirikiano wa vyombo vya habari na nchi  zote za Afrika. 


Rais wa Muungano wa Waandishi wa Habari wa Côte d’Ivoire , Marie-Louise, akitoa shukrani  kwa jukumu la Misri katika kuunga mkono waandishi wa habari wa Afrika. 
Alisema mafunzo hayo yamefungua awamu mpya ya ubora na utaalamu kwa waandishi wa habari Afrika na kusisitiza kuwa changamoto kubwa sasa ni kuhakikisha waandishi wanakuwa wabebaji wa ukweli na watetezi wa maslahi ya umma.

Akiisoma wosia wa marehemu mume wake, ambae ni mwandishi mkongwe Mhfouz El  ansary Bi. Nangwa Khalil alisema El-Ansary aliongoza UAJ kwa miaka 64 na katika wosia wake aliwataka vijana kuheshimu muda, kusema ukweli, kulinda vyanzo vya habari, na kufanya kazi ya kuunganisha watu. 
"Heshima hii ina maana kubwa kwetu, hasa kwa kutambua miaka yake zaidi ya 35 ya utumishi wa kujitolea katika uandishi wa habari wa Afrika," alisema.
 Aliongeza kuwa UAJ umelea viongozi wengi wa vyombo vya habari na siasa barani Afrika, na sasa jukumu liko kwa kizazi kipya.

 "Tutarudi Kubadilisha Taswira ya Uandishi wa Habari"

Kwa niaba ya wahitimu wa kozi ya 63, mwandishi kutoka Zambia, Rudith Nalumbaya Namusukuma, akisoma  hutuba alisma kuwa  waandishi wako tayari kubeba jukumu hilo na kuwa sauti ya mabadiliko.
"Ndoto yetu ni kubwa zaidi ni kurudi nchi zetu na dhamira ya kubadilisha taswira ya uandishi wa habari Afrika.
 Mafunzo haya ya wiki tatu tuliyopata Misri yatajidhihirisha katika utoaji wetu wa habari na kuleta athari chanya kubadilisha simulizi la Afrika," alisema Rudith.
Kozi hiyo ilishughulikia masuala ya kitaaluma ya kisasa ikiwemo mabadiliko ya kidijitali na akili bandia ambapo ilihudhuriwa na Abdullah Hassan, Amall Abdel-Motaleb Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Mafunzo, Dkt. Samia Abbas Katibu Mkuu wa UAJ, Maher Abdel Aziz, Ayman Adl, na Zeinab Helmy Mkurugenzi wa Kozi za Mafunzo.
UAJ ilihitimisha kwa ahadi ya kuendelea na mafunzo kama hayo na kuimarisha uhusiano wake na Misri, katika juhudi za kuimarisha jukumu la vyombo vya habari kujenga mawasiliano na uelewa kati ya watu wa Afrika.

Post a Comment

0 Comments