HONGERA DR MWINYI! WATUMISHI WAPATA LAKI 5 - WAZIRI HAROUN AMESEMA HAKI IMETENDEKA NA POSHO TENGEFU ZAZINGATIWA



NA-FATMA SULEIMAN-PEMBA 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora,Zanzibar, Haroun Ali Suleiman,  amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ametekeleza ahadi yake ya kupandisha mshahara wa kima cha chini kwa watumishi.
Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa ZRA Gombani Chake Chake Pemba.
 amesema hatua hiyo imefanyika kwa kuzingatia maslahi ya watumishi katika Mihimili yote mitatu ya Dola, pamoja na kuzingatia ulipaji wa Posho za Maeneo Tengefu kwa watumishi wanaofanya kazi katika mazingira magumu.

"Serikali imefanya mazingatio makubwa kwa watumishi wote ili kuwatia ari katika kufanya kazi kwa ufasaha,ni vyema sasa watumishi kujituma katika kuitumikia nchi yao," alisema Waziri Haroun.
Aliongeza kuwa katika  nyongeza hiyo, Serikali imezingatia kwa makini baadhi wakuu na watumishi kiujumla huku sekta ya ualimu ikizingatiwa kwa kiasi kikubwa kwa upande wa posho hasa walimu wanaofanya kazi maeneo tengefu pamoja na posho la walimu wanaofundisha wenye mahitaji maalum.
Aidha, Waziri Haroun ametoa wito kwa  wafanyabiashara nchini kuacha mara moja tabia ya kutumia mianya ya  kuongezeka kwa mishahara kupandisha bei za bidhaa kwa kisingizio cha kutozwa kodi, ili kuwapunguzia wananchi wenye hali duni.
Amesema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kupandisha bei za bidhaa kiholela na kisha kutumia mianya hiyo kujipunguzia mzigo wa kodi.
Katika hatua nyingine, Mh. Haroun amegawa Bajaji kwa Wasaidizi wa Sheria kwa mikoa yote miwili ya  Pemba, kwa lengo la kurahisisha huduma za usafiri na kuwawezesha kuwafikia wananchi kwa urahisi na kutoa huduma kwa ufasaha.

Akitoa shukrani kwaniaba ya wenzake wasaidizi hao washeria Mohammed Othman Abdallah, wamemshukuru Rais Dk. Mwinyi kupitia uongozi wa Waziri Haroun kwa kuwapatia vitendea kazi hivyo vitakavyowasaidia kuendesha shughuli zao katika shehia kwa urahisi.
Ikumbukwe kuwa utakelezaji huo wakuongeza mshahara umekuja baada ya ahadi iliyotolewa na Dk. mwinyi katika maadhimisho siku ya  wafanyakazi duniani mei mosi inayofanyika kila mwaka duniani kote.

Post a Comment

0 Comments