IMEANDIKWA NA
ZUHURA JUMA, PEMBA
SERIKALI
ya awamu ya nane inayoongozwa na Dk. Hussen Ali Mwinyi imelichukua suala la
uwekezaji wa visiwa vidogo vidogo Zanzibar katika hatua nyengine ambayo ni
nzuri na yenye manufaa kwa nchi.
Agosti hadi Septemba mwaka 2021, Serikali ilitangaza awamu
ya kwanza ya uwekezaji, ambapo visiwa vinane (8) vilipata wawekezaji kati ya
kumi (10) vilivyotangazwa.
Visiwa hivyo ni Changuu, Pwani, Bawe, Pamunda A na B, Kwale,
Chumbe, Misali, Njau na Matumbini A, ambapo kisiwa cha Njau na Matumbini A
wawekezaji walishindwa masharti.
Serikali imeweka vigezo maalumu kwa wawekezaji wa visiwa na
ikiwa hakufikia, hatopatiwa kwani Serikali iko makini kwenye suala hilo.
Anasema Mkurugenzi Uwekezaji Pemba Al-haji Mtumwa Jecha,
awamu ya pili ilitangazwa mwaka huu, ambapo kwa Pemba ni kisiwa cha Matumbini,
Jombe na Kwata Kusini na Kashani, Njau na Fundo Kaskazini.
Visiwa hivyo vitakodishwa muda mrefu ili vijengwe hoteli za
kitalii zitakazotoa huduma mbali mbali na utakuwa uwekezaji mkubwa utakaoipatia
Serikali mapato na kuwanufaisha wananchi wake.
Hiyo ni njia bora ya kuimarisha Utalii kwa sababu itakuwa ni
miradi mikubwa na endelevu, hivyo Serikali imeamua kukodisha kama zinavyofanya
nchi nyengine ikiwemo Morishias.
Dk. Hussein
Mwinyi alitaja miongoni mwa masharti yaliyowekwa kwa muwekezaji ni kuilipa
Serikali kwanza kabla hajaanza ujenzi wa mradi wake na aeleze ataweka mradi
gani na wenye ukubwa kiasi gani, ili Serikali ijiridhishe kuwa mradi husika
hautaharibu mazingira na uwe mkubwa.
Makala haya inaelezea jinsi gani miradi ya kitalii katika
visiwa vidogo vidogo Pemba, inaweza kuimarisha maisha ya watu…
Ukodishwaji huo utasaidia maendeleo ya Zanzibar, kwani fedha
ziakazopatikana zinatumika katika huduma za kijamii pamoja na kuzalisha ajira
kwa wazawa.
Suala
la Ajira
Ali Hamad Ali (40) wa Kitambuu Wete anasema, ipo haja kwa
wazazi kuelekeza watoto wao mambo ya kitalii, ili mradi ukianza vijana wapate
ajira.
“Ni watu watakavyojipanga tu, lakini ikiwa hawatajipanga
mapema, watakuja watu wa nchi nyengine, kuchukua nafasi hizo na baadae tubaki
kulalamika”, anafahamisha.
Anaeleza, ukodishwaji wa visiwa ni muhimu sana kwani
itaimarisha maisha yao kwa namna tofauti kutokana na kutakuwepo huduma za
kijamii ikiwemo elimu, maji safi na salama, umeme, afya na barabara.
“Wataajiriwa katika hoteli hizo na kujiajiri wenyewe kwa
kuuza bidhaa mbali mbali na kutembeza watalii”, anafahamisha Kauthar Abeid Omar
(20) wa Chasasa Wete.
Zuhura Mgeni Othman Afisa Mdhamini Wizara ya Utalii na Mambo
ya Kale Pemba anaeleza, wajamii waliopo ndani na nje ya visiwa hivyo
watafaidika na ajira.
“Mwekezaji atahitaji rasilimali kutoka kwa wanajamii ili
kuweza kufanyakazi, kuna rasilimali watu na pia vitu wanaozalisha vitahitajiwa
na wawekezaji, hivyo watajiajiri”, anaeleza.
Upatikanaji
wa masoko ya bidhaa
Hadia Hamad Shehe (35) mkaazi wa Micheweni anaeleza,
Serikali na taasisi binafsi zinaimarisha vikundi vya wanawake na vijana katika
shughuli za ujasiriamali, ingawa wanakosa soko la uhakika.
Anasema, uwekezaji huo utasaidia upatikaji wa soko la
uhakika, kwani watalii watakuja kwa wingi kutembea katika visiwa hivyo.
“Wavuvi wanapewa boti lakini hawana sehemu ya kuuzia samaki
wao, lakini zitakapojengwa hoteli za kitalii watauza huko, wajasiriamali
watauza mikoba, mboga, matunda na bidhaa nyengine”, anaeleza
Mkaazi wa Jadida Wete Halima Mzee Khamis (27) anasema,
miradi hiyo itaimarisha kipato cha wananchi na uchumi utakuwa zaidi.
“Uwekezaji huu unaweza kuipa nchi umaarufu kutokana na
watalii wanaoingia, wataitangaza na kuongeza urafiki na mataifa makubwa ambayo
yataweza kutoa misaada ya moja kwa moja”, anaeleza.
“Hapa wazawa watapata fursa ya kuuza bidhaa tofauti, ikiwemo
za vyakula, mikoba, mafuta na dawa zinazotengenezewa karafuu, mkaratusi,
mwani”, anafahamisha Mohamed Khamis Shehe (44) wa Uweleni Mkoani.
Khamis Ali Juma Mratibu wa Idara ya Makumbusho na Mambo ya
Kale Pemba anaeleza, mwekezaji hawezi kuimarika kwenye shughuli zake ikiwa
hakuwategemea wajasiriamali, kwani wageni watakaofika lazima watahitaji vitu.
“Wajasiriamali watapata tija na manufaa kwa sababu kuna
wanaolima bidhaa tofauti, pia wavuvi watauza samaki kwa wawekezaji hao”,
anaeleza.
“Wananchi wawe makini na hili, kwa mfano mwekezaji anahitaji
tani moja ya tungule kila siku, ikiwa wananchi watajikubalisha kulima, kutakuwa
na soko la kudumu”, anaeleza Mkuu wa Wilaya ya Wete dk. Hamad Omar Bakar.
Mjasiriamali wa ushonaji wa makawa ya kindu nzima, Khadija
Sleyum (47) mkaazi wa Tumbe anasema, watanufaika sana kwani watalii wataingia
kwa wingi na watanunua bidhaa zao kwa vile ni za kipekee.
“Makawa, vipepeo na mikoba tunayotengeza inawavutia sana
watalii na ni mambo ya utamaduni, hivyo soko litakuwa na sisi tujikwamua
kiuchumi”, anasema Khadija.
Fat-hiya Mussa Said Mratibu wa TAMWA Pemba anaelezea,
watalii wanapoongezeka nchini na wajasiriamali wataongeza soko la bidhaa zao
ndani na nje ya nchi.
“Mtalii anapoona bidhaa ni nzuri, anaweza kununua na
kusafirisha kwenye nchi yao, hivyo soko la wajasiriamali litaimarika na
wananchi watanufaika kwa ujumla”, anasema.
Haji Khamis Haji Mratibu Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi Pemba watahakikisha wajasiriamali wanakidhi vigezo vya kupata mikopo
ili waongeze mtaji utakaowasaidia kuzalisha bidhaa nyingi na zenye ubora.
“Mikopo itawasaidia kuzalisha bidhaa nyingi, hivyo
wawekezaji watazipata za kutosha, hii itawainua sana wajasiriamali wetu”,
analeza.
Utunzaji
na Uhifadhi wa mazingira
Mkurugezi wa Uwekezaji Pemba Al-haji Mtumwa anasema, kati ya
masharti yaliyowekwa kwa muwekezaji ni lazima aielezee Serikali namna gani
atazingatia uhifadhi wa mazingira.
“Mchakato mzima wa ukodishwaji tunashirikiana na wadau wa
taasisi mbali mbali ikiwemo ya mazingira (ZAEMA) katika kuhakikisha mazingira
yanatunzwa kwa hali ya juu”, anafahamisha.
Anafafanua kuwa, Serikali na wananchi hawatokuwa radhi
baadha ya miaka kadhaa kupotea viumbe vya baharini ikiwemo matumbawe, hivyo
watakuwa makini katika suala uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
Mkuu wilaya ya Wete dk. Hamad Omar Bakar anasema, ikiwa kuna
mazingira hayako sawa katika maeneo yao, wasaidie upatikanaji wa uhifadhi wa
mazingira na faida hizo ziwafike wananchi, ili wajisikie kwamba uwepo wa utalii
hauko katika mazingira ya kuwaathiri.
Fatma Hassan Kombo (38) wa Msingini Chake Chake anaeleza,
ili utalii uwe nzuri ni lazima mazingira ya karibu yawe mazuri, hivyo
wawekezaji watalinda mazingira yanayowazunguka ili waendelee kuwa na soko la
muda mrefu.
“Ili kuendelea kuvutia wawekezaji wetu hatuna budi kuisaidia
Serikali kuyatunza mazingira yetu, ili yawavutie watalii wanaoingia”, anasema
mkaazi wa kisiwa cha Fundo Khamis Faki Mjaka (47).
Ali Juma (32) wa Chake Chake wanashuhudia visiwa vyote kuwa
vichafu, hiyo ni kwa sababu wananchi wanashindwa kutunza mazingira, lakini
watakapokuwepo wawekezaji itakuwa ndio mwarubaini wake.
“Itasaidia usafi wa mazingira ya visiwa vyetu kwa sababu
mwekezaji atalazimika kuboresha na kutunza mazingira ili aweze kufikia malengo
yake”, anafafanua kijana huyo.
Alitolea mfano kisiwa cha Chumbe Unguja na Misali Pemba
jinsi wawekezaji hao wanavyojitahidi kuyaweka mazingira ya visiwa hivyo katika
hali ya usafi.
Fat-hiya Mussa Said anasema, utalii wa sasa ni wa kutunza
mazingira, kitu ambacho wanatakiwa wawarithishe watoto wao, ili mabadiliko ya
Tabianchi yasiathiriwe.
“Tunapohifadhi mazingira tunasaidia kuendeleza ule uhalisia
wa visiwa vyetu ili visipotee na kuufanya utunzaji huo, uwe ni endelevu”,
anaeleza.
Wawekezaji wanakuwa na majukumu yao, hivyo watawaongoza
wananchi katika suala zima la uhifadhi wa mazingira, ili waendelee kufaidika na
uwekezaji huo.
Jinsi
inavyoweza kuwasaidia watu wa karibu
Wananchi wa karibu watafaidika zaidi na utalii huo visiwani
mwao katika masuala ya ajira na kwenda kuuza bidhaa zao pamoja na kuongeza
mashirikiano baina ya wao na wawekezaji.
“Watu wa karibu ni wa mwanzo kunufaika katika Nyanja mbali
mbali, kuongeza mashirikiano katika kuchangia maendeleo kwenye visiwa hivyo,
ikiwa ni pamoja na kupata huduma za kijamii”, anasema Asha Ali Khamis (30) wa
Kipangani Wete.
Faida Suleiman Ali (36) wa kisiwa cha Njau Wete anaeleza,
uwekezaji huo utawasadia kunyanyua kipato chao, kwani watakuwa wanafanya
biashara na kuuza kwenye hoteli”, anasema.
Fadhila Haji Makame (39) mkaazi wa Makombeni Mkoani
anaeleza, utasaidia kunawirisha maisha ya wakaazi wa visiwa hivyo kwa kupata
mahitaji yao ya lazima ikiwemo chakula.
Al-haji Mtumwa Mkurugezi Uwekezaji anasema, wananchi wa
visiwa hivyo na maeneo ya karibu watanufaika kuanzia hatua ya ujenzi
utakapoanza, kwani watapata ajira na kujiajiri wenyewe kwa kuuza biashara zao.
Moja ya kigezo cha maombi ya mwekezaji ni kuhakikisha namna
gani watawashirikisha wananchi waliopo katika visiwa hivyo na maeneo ya karibu
na ikiwa hakueleza hayo, hatopatiwa visiwa hivyo.
Anawataka wananchi waelewe kwamba, visiwa hivyo haviuzwi na
vinakodishwa kwa maslahi ya Taifa, kwani kuna faida nyingi zitapatikana.
“Visiwa vitapata kutunzwa, wawekezaji wanakuja na fedha
nyingi ambapo wanapojenga wanahitaji vibarua, wanaajiri wananchi na pia baadhi
ya vitu watanunua kwetu, hivyo kutakuwa na mzunguko wa biashara kati ya
mwekezaji na wananchi”, anafahamisha.
Anataja zaidi ya dola milioni 200 zimepangwa kuekezwa katika
visiwa vile vya awali, ambapo kwa Pemba ni Misali, hivyo fedha zitakazopatikana
zitasaidia kuimarisha nchi.
Uimarishaji
wa miundombinu
Mkurugeni huyo anaeleza, watatumia miundombinu tofauti
kufikia visiwa hivyo ikiwa ni pamoja na kujenga bandari ndogo ndogo na pia
kutakuwa na matumizi ya herikopta.
“Tumechelewa kidogo katika uwekezaji huu, hivyo hata kama
muwekezaji atajenga bandari tutamruhusu kwa kuzingatia sheria na taratibu za
nchi”, anafafanua.
Kwa upande wa maji na umeme, mamlaka hizo zitashirikiana
kikamilifu na wawekezaji katika kuhakikisha huduma hizo zinafika katika visiwa
vilivvyokodishwa.
Afisa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja kutoka ZECO Pemba
Haji Khatib Haji anasema, wamejipanga kufikisha huduma ya umeme katika visiwa
vyote, ambapo visiwa kama Fundo, Kisiwa Panza, Makoongwe, Kojani tayari
vimeshapata huduma hiyo na sasa watafikisha umeme kisiwa cha Njau na Kokota kwa
kutumia umeme wa nguvu za jua.
Suleiman Anas Massoud ambae ni Afisa Uhusiano ZAWA Pemba
anasema hawawezi kuchimba visima kwenye visiwa kutokana na maji chumvi ingawa
wana utaratibu ulazaji wa bomba mpaka kwenye kisiwa wenyewe.
“Siku zote uwekezaji huwa ni mkubwa hivyo, tunaweza
kuchangaza visima katika kuwapelekea maji ama tukaachimbia vyao, siku hizi kuna
teknologia ya kuyabadilisha maji ya bahari kuwa maji ya kawaida lakini ni
gharama kubwa”, anasema.
Upatikanaji
wa kodi kwa Serikali
Anasema Mkurugenzi Al-haji kuwa, kama ilivyo kawaida ya
kulipia kodi nyumba, vivyo hivyo kwenye visiwa, wawekezaji watalipa kodi kila
mwaka.
Mwananchi Khairat Khamis Saleh (27) wa Gombani Chake Chake anasema,
ukodishwaji huo utaongeza pato la Serikali kwani watakaokodishwa watalipa kodi
na tozo mbali mbali zitakazoisaidia Serikali kupata mapato yake.
“Wenye hizi hoteli watalipa pesa nyingi tena za kigeni,
hivyo hata uingiaji wa pesa za kigeni utaongezeka na kusababisha kuikuza
thamani ya shilingi ya Tanzania”, anasema.
Mdhamini Utalii na Mambo ya Kale anasema, kwa vile
watawekeza ni lazima watavutia wageni na watakapokuja watanufaisha Serikali
kwani watalipia namna mbali mbali, hivyo kodi ya Serikali itaongezeka.
“Tutapata kodi kutokana na uwekezaji utakaokuwepo kwenye
visiwa vyetu na nchi itaongeza mapato yake kwani wawekezaji wana uwezo mkubwa”,
anasema Jamal Hassan Jamal Mkuu wa Utawala ZRB Pemba.
Nini
kifanyike ili kuimarisha zaidi utalii na maisha ya wananchi.
Anasema Khadija Shehe (55) mkaazi wa Tumbe Mashariki,
wananchi wasijilemaze zinapokuja fursa na wazitumie kwa lengo la kuwanufaisha.
Salma Hamad Ali (49) Shengejuu Wete, anasema ipo haja wananchi
waunge mkono juhudi za Serikali kuhakikisha nchi inapata maendeleo kila kona,
kwani uwekezaji ni dhana pana ya kiuchumi.
Salim Said Salim Mkurugezi Dhamana Taasisi ya Viwango Pemba
(ZBS) anawataka wajasiriamali kuzalisha bidhaa zenye ubora ambazo zitawapatia
alama ya ubora, ili watalii wanunue kwa haraka.
“Alama ya Ubora ni muhimu sana katika bidhaa tunazozalisha,
kwani wageni wakiziona itakuwa hawana wasiwasi wa kutumia, hivyo wazingatie
vigezo vyote vinavyotakiwa”, anafahamisha.
Hamad Amini Ali Mdhamini Kamisheni ya Utalii Pemba anawataka
wananchi waukubali utalii kuwa ni biashara na ni ajira, kwa hiyo waendelee
kufaidika kwa kufanya yale ambayo yatawaletea manufaa.
Dk. Mwinyi katika hotuba yake anasema, juhudi
za Serikali zimewawezesha kuongeza idadi ya watalii kutoka 260,644 mwaka 2020
hadi kufikia 393,512 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 50.97 pamoja na idadi
ya Kampuni za Ndege zinazofanya safari za kuja Zanzibar kutoka 27 hadi 34,
Ndege hizo zilizoongezeka zinakadiriwa kuleta zaidi ya watalii 50,000 kwa
mwaka.
MWISHO.
0 Comments