NA HAJI NASSOR, PEMBA
WAHANGA wa maradhi ya mripuko shehia
ya Kojani wilaya ya Wete Pemba, wamewashauri wananchi wenzao shehiani humo, kufanya
usafi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kuchoma moto vichaka, vilivyozunguka
makaazi yao, ili kujikinga na maradhi ya mripuko.
Wakizungumza
na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, walisema wapo baadhi ya
wananchi wamekuwa wakipuuzia maagizo ya wataalamu wa afya, kupelekea kusambaa
kwa magonjwa ya mripuko.
Walisema,
wakati huu wa mvua zikiendelea kunyesha, ndio hasa wa kufanya usafi wa majaa
yaliokaribu nao na kurekebisha mitaro ya maji machafu, ikiwa ni hatua moja wapo
ya kujikinga na magonjwa ya mripuko wa kama vile matumbo ya kuharisha.
Walieleza,
suala la usafi lazima liwe tabia kwa wananchi wenzao wa shehiani humo, maana
limekuwa ndio chanzo kikuu cha kusambaa kwa magonjwa hayo usipofanyika.
Mmoja kati
ya wahanga hao Makame Hamasd Ali, alisema mwaka 2017, watoto wanne walikumbwa
na maradhi ya mripuko ya kipindu pindu, kutokana na kutofuata maagizo ya wataalamu
wa afya, juu ya ujenzi wa vyoo vya kisasa.
“Suala la
usafi wa mazingira na matumizi ya vyoo vya kisasa, ni miongoni mwa maagizo ya
wataalamu wa afya, ambayo kwa njia moja ama nyingine, ni sababu kujikinga na
kipindu pindu na magonjwa mengine ya mripuko,’’alieleza.
Nae muhanga
Othman Haji Ussi, alisema aliwahi kulazwa kwenye kambi ya wagonjwa wa kipindu
pindu, ingawa baada ya kupewa tiba na taaluma, sasa amezingatia usafi.
Hivyo, aliwashauri
wananchi wenzake, kuhakikisha wanazingatia maagizo na ushauri wa wataalamu wa
afya, ili kuhakikisha wanaishi bila ya kukumbwa na magonjwa ya mripuko.
Afisa
Mdhamini Wizara wa Afya Pemba dk. Yakoub Mohamed Shoka, akizungumza kuelekea
siku ya unawaji mikono duniani, ambapo
ilifanyika kisiwani Pemba, alisema usafi ni njia moja wapo ya kuyashinda
magonjwa kadhaa.
Alieleza
kuwa, usafi kwa wananchi hasa katika maeneo yao kama vile kufukia vidimbwi vya
maji machafu, ikiwa ni njia moja wapo ya kujikinga na maradhi ya maripuko,
linahitajika.
“Ni kweli
kipindi kama hichi ni nafasi ya wananchi kufanya usafi kwenye maeneo yao, iwe
ni kusafisha majaa au kufukia vidimbwi vinavyotuwama maji machafu,’’alieleza.
Moja ya njia
zinazotajwa kuwa ni sababu ya kuenea kwa magonjwa ya mripuko kama vile kipindu
pindu na homa za mapafu, ni kutoafuata maagizo na ushauri wa watalaamu wa afya.
Mwisho
0 Comments