Na Salmin Juma, Unguja
Wadau mbali mbali wa
masuala ya habari wakiwemo wahariri, waaandishi wa habari wakongwe na waandishi
wa habari chipukizi wamekutana kujadili sheria mbali mbali zilizopitwa na wakati
ambazo kwa kiasi kikubwa zinaminya uhuru wa habari hapa Zanzibar.
Wadau hao wamezitaja
sheria kama Sheria ya Usajili wa
Wakala wa Habari, Magazeti na Vitabu namba 5 ya mwaka 1988 iliyofanyiwa
marekebisho na Sheria No.8 ya 1997 sambamba na Sheria ya Tume ya Utangazaji ya
Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka
2010 kuwa ni sharia ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho ili kuendana na
wakati uliopo na kutoa uhuru wa kujieleza kwa wananchi.
Haki ya Uhuru wa kujieleza Ibara ya
18 ya katiba ya Zanzibar 18(1) imesema kuwa ; Bila ya kuathiri sheria
zinazohusika za nchi, kila mtu anayo haki ya uhuru wa maoni na kutafuta,
kupokea, kutoa au kusambaza habari na mawazo yake kupitia chombo chochote cha
habari bila ya kujali mipaka ya nchi na pia ana haki ya mawasiliano yake
kutoingiliwa.
Kutokana na maoni ya wadau akiwemo mwanahabari mkongwe Zanzibar Salim
Said Salim wanasema kwamba neno hili la “bila
kuathiri sheria za nchi” linapaswa lirekebishwe kwani linaondosha uhuru na haki
ya kujieleza na haki ya kupata habari.
“kifungu hichi kinaonesha ni namna gani
sentensi hii ya “bila kuathiri” inavyokiuka uhuru wa kujieleza kuhusiana na
sheria nyingine za nchi”.
Katika moja ya mikutano iliyofanyika kujadili
sheria mpya ya habari, Mkurugenzi wa Tamwa Zanzibar Dk Mzuri Issa, alisema
ingawa kwa sasa hapa Zanziabr tunao uhuru wa habari lakini namna ya utolewaji wake ni wa kuminywa
kwani unatolewa kwa njia moja na kunyang’anywa kwa njia nyengine.
Kwa upande wa sheria ya Tume ya Utangazaji ya
Zanzibar namba 7 ya mwaka 1997 kama ilivyorekebishwa na sheria namba 1 ya mwaka
2010 wa Muundo wa Tume Kifungu cha 6(1) Tume ya Utangazaji ni
lazima ioneshe vyombo vya habari na mambo yote ya kijinsia.
“katika sheria mpya tunapendekeza tume iweze
kuwachukulia hatua wote wanaodhalilisha wanawake kwenye televisheni kwani ziko
picha zinaoneshwa kwenye huko ambazo maudhui yake yanadhalilisha sana
wanawake”. Alisema dokta Mzuri.
Dokta Mzuri aliongeza kuwa suala la jinsia
lina umuhimu wake, hivyo katika sheria hiyo waziri amepewa mamlaka ya kuteua
wajumbe zaidi ya wanne wa Tume lakini hakuna pahali palipopendekezwa uwakilishi wa
wadau wa jinsia, ni vizuri kabla ya waziri hajateua wajumbe wa Tume apate mapendekezo
ya wadau wa masuala ya jinsia na pia sifa za wajumbe wa tume hiyo ziainishwe
kwenye kanuni”.
Hizo ni baadhi ya sheria
ambazo zinahitaji kufanyiwa marekebisho ili kupatikana kwa uhuru kamili wa
kujieleza lakini pia kwa ujumuishaji wa masuala ya jinsia katika masuala yote
yanayohusu habari ili kupatikana kwa usawa wa kijinsia katika jamii.
0 Comments