Mkurugenzi Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria
Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, amelitaka
Shirika la Msaada wa Kisheria na Haki za Binaadam Zanzibar (Zanzibar Legal Aid
and Human Rights Organization-ZALHO) kuzidisha mashirikiano na serikali katika
utekelezaji wa majukum yao mbalimbali kwa lengo la kukua zaid na hatimae
kufikia malengo ya shirika hilo.
Kauli hiyo aliitoa juzi katika ukumbi wa mikutano wa ZALHO
Kwaalimsha Mkoa wa Mjini Maghribi Unguja alipokua akizungumza na watendaji wa
shirika hilo kufuatia ziara maalum ya kuwatembelea na kujadiliana masuala mbali
mbali kuhusiana na utendaji kazi.
Mkurugenzi Hanifa alisema “kwa ninavyo wajua watendaji wa
shirika hili, naamini ndani ya miaka mitano mbele, shirika litakua kubwa na
litafanya mambo makubwa kuisadia jamii” alisema.
Akizungumza na Muandishi wa habari hizi Mkurugenzi Hanifa alisema, ingawa Shirika la ZALHO ni changa kwa kuanzishwa lakini watendaji wake ni wazoefu wa muda mrefu, pia ni wenye kujitolea katika mambo mbali mbali, hivyo kulitabiria kukua shirika hili si jambo zito.
Katika hatua nyengine Hanifa
amelipongeza shirika la ZALHO hasa kwa wanavyoshughulika na mashauri ya
watoto “kama unavyojua, ZALHO imefunguliwa hivi karibuni na kama Idara tuliwahi
kumpokea mtoto aliekinzana na sheria na sisi moja kwa moja tukawasiliana na
Mkurugenzi Mtendaji wa ZALHO na wakampokea hatimae wakamsimamia Mahkamani mpaka
kesi kumalizika vizuri” Mwisho wa kunukuu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ZALHO Bi Jamila
Masoud alisema, ujio wa Mkurugenzi Hanifa katika Shirika lao umeleta tija kubwa
hasa baada ya kushauriana mambo ya uboreshaji wa huduma za Msaada wa kisheria
Zanzibar “Tumefarajika na ujio wake, kwasababu tumejadili mengi na tunaahidi tuliyoyazungumza tutayafanyia
kazi ili jamii izidi kuimarika katika misingi ya haki” alisemaJamila.
Nae Wakili kutoka ZALHO Thabit Abdulla alisema, ujio wa
Mkurugenzi huyo alieambatana na watendaji wengine wa Idara umekua ni dira ya mafanikio
“Mazungumzo baina yetu na Mkurugenzi wa idara yataleta
mafanikio makubwa, kwasababu tunakwenda kutekeleza kwa vitendo dira na dhamira
ya ZALHO katika kutoa msaada wa kisheria na usimamizi wa haki za binaadamu kwa
jamii ya wazanzibari ambao kwa kiasi kikubwa wanahitaji msaada huo” alisema.
Huu ni muendelezo wa ziara za Mkurugenzi wa Idara ya Katiba
na Msaada wa Kisheria Zanzibar kuzipitia taasisi mbali mbali
zinazojishughulisha na masuala ya kisheria.
0 Comments