Imeandikwa na Haji Nassor Pemba.

MWAKILISHI wa Jimbo la Wingwi wilaya ya Micheweni Pemba, Kombo Mwinyi Shehe, amesema mwakani anatarajia kuandaa mashindano maalum, kwa ajili kukuza vipaji kwa wanafunzi wa ngazi zote, zilizomo jimboni humo.
Alisema, michezo ni moja ya njia ya kuwapa ufahamu wanafunzi kwa kule, miili yao kuchangamka, ambapo hilo litaibua ari na uhamasishaji wa kujisomea zaidi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mwakilishi huyo alisema kwa kuanzia, ataanza na mchezo wa mpira wa miguu, kwa wanafunzi wa skuli za msingi na sekondari, na mshindi kukabidhiwa zawadi maalum.
Alisema, anatashirikiana na wizara ya elimu, ili kupata baraka juu ya jambo hilo, ili mwakani atakapobakadhi zawadi kwa wanafunzi waliofaulu, iwe sambamba na kukabidhi kikombe na zawadi nyingine kwa washindi.
“Inaonekana vipaji vya wanafunzi havionekani skuli, na hili linasababishwa na kulala kwa michezo, lakini mwakani nitaanzisha mashindano maalum,’’alieleza.
Aidha Mwakilishi huyo, aliwataka wanafunzi kuanza kujiandaa na atangaalia uwezekano wa kuwapatia vifaa kama vile jezi na mipira, ili kuwa na matayarisho ya uhakika.
Kuhusu michezo ya kwa ajili ya wanawake, alisema atalizingatia, na hata kwa hatua za awali, kuanza na mchezo wa mpira wa mikono na kuvuta kamba.
“Wanafunzi wote wanahaki sawa, hivyo hata kwa upande wa wanafunzi wanawake, nao hawataachwa nyuma, kushiriki kwenye michezo,’’alieleza.
Afisa elimu msingi wilaya ya Micheweni, Tarehe Khamis Hamad, alisema wazo hilo ni zuri, na wameahidi kutoa kila aina ya ushirikiano na Mwakilishi huyo.
Alieleza kuwa, michezo imeruhusiwa skulini, kwani huwapa wanafunzi ari na hamu ya kujisomea zaidi, na hata akili hupanuka na kuchangamka.
“Wazo la Mwakilishi wa Jimbo la Wingwi ni zuri, na sisi wizara tutampa kila aina ya ushirikiano, ili kuona tunazalisha vipaji na vyengine kuviendeleza,’’alieleza.
Mratibu wa chama cha ACT-Wazalendo Pemba Said Ali Mbarouk, alisema michezo ni sehemu ya utamaduni wa Zanzibar hivyo ipo haja ya kuendelezwa.
Mwanafunzi Hamad Juma Hamad wa skuli ya Simai, alisema wazo hilo wamelipokea kwa furaha kubwa, na wanachosubiri ni kuanza kwa mashindano hayo.
Nae mwanafunzi Aisha Hassan Ali wa skuli ya Wingwi, alisema mashindano hayo, yatamasha umoja, mshikamano na kujuana zaidi kati ya wanafunzi wa skuli moja na nyingine.
Mwisho



Haji Mohamed and 2 others
1 Share
Like
Comment
Share