JUMUIYA ya wanafunzi wa wa Saikolojia Chuo Kikuu Zanzibar (ZUPCSA) wameiomba Serikali kuajiri walimu wa saikolojia ambao watawasaidia wanafunzi na watoto waliofanyiwa udhalilishaji kuwapa ushauri nasaha.
Walisema kuwa, wakati wanapita skuli kutoa elimu ya saikolojia, waligundua kuwa, kuna uhitaji mkubwa kwa walimu wa saikolojia, kwani waliopo ni wale tu waliopatiwa mafunzo ya muda mfupi, jambo ambalo halikidhi mahitaji ya kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Naibu Mwenyekiti wa Jumuiya ya wanasaikolojia Zanzibar na Mwenyekiti mstaafu wa jumuiya ya ZUPCSA ya ZU, Ramadhan Mohamed Hassan alisema kuwa, hali hiyo hupelekea umahiri wa kazi kuwa ni mdogo sana, kwa sababu kunakuwa na changamoto nyingi za kisaikolojia kwa wanafunzi.
"Walimu waliopo ni wale waliopata mafunzo ya wiki mbili, hivyo inakuwa kazi hazifanyiki vizuri, kwa hiyo ni tunapendekeza waajiriwe walimu hasa waliosomea kada hiyo, ili kuondosha matatizo yaliyopo, kwa sababu waliopo hawajui njia ya kuyatatua kwa vile si maalumu kwa fani hiyo", alisema.
Aidha alisema kuwa, katika utafiti wao mdogo walioufanya kwenye vituo vya mkono kwa mkono pia waligundua kwamba, watoto wanaodhalilishwa hawapati elimu ya saikolojia ipasavyo, hivyo wanashauri madaktari kisiwani Pemba waanzishe umoja wa saikolojia, kwa ajili ya kuwasaidia watoto hao kupata tiba ya saikolojia ili wasiathirike zaidi kiakili.
Ramadhan alisema kuwa, wamekuwa wakitoa elimu kwa vijana na wanafunzi ambapo kwa mwaka huu wamezifikia skuli 12 kisiwani Pemba, hospitali mbili na nyumba ya kurekebisha tabia (soba house) moja.
Alisema, wanawasaidia wanafunzi kwa kuwapa elimu ya saikolojia na afya ya akili kuanzia skuli za msingi hadi vyuo vikuu pamoja na vijana mbali mbali, ili wapate uwelewa wa kupambana na changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo.
Alisema kuwa, pia kuna baadhi ya wanafunzi wanafeli mitihani yao na si kwa sababu hawafahamu lakini wakati mwengine wamefikwa na madhila makubwa ambayo yanawasabaishia kufeli, hivyo wanapokwenda wanaibua changamoto na kuwapa elimu ya saikolojia, hivyo hatimae wanafaulu vizuri katika masomo yao.
"Wakati mwengine unafika skuli unawauliza walimu kuhusu udhalilishaji wanakwambia hakuna, lakini tunapowachukua wanafunzi na kuwahoji, wanafunguka kila kitu kwa sababu sisi ni vijana wenzao hivyo wanajua kuwa ni sehemu nzuri ya kuleta changamoto zao", alisema.
Naibu huyo pia aliiomba Serikali kuwawekea bodi itakayosimamia harakati za Saikolojia sambamba na kupewa leseni ya kufanya kazi, ili wakipeleka mapendekezo yao kuwe na watendaji wa kuyashughulikia.
Skuli 12 walizozifikia Pemba kutoa elimu ya saikolojia na afya ya akili ni Fidel Castro, Uzalendo, Ng'ambwa, Mchangamdogo, Chasasa, Utaani, Kengeja, Samia Suluhu Hasaan, CCK, Konde, Madungu na Kojani, hospitali ya Chake Chake na Micheweni pamoja na Soba House ya Mkoroshoni.
chanzo: pembatoday
0 Comments