Imeandikwa na Mwandishi wetu.
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake
Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ), Dkt. Mzuri Issa, amewashauri wanawake na Vijana kujiamini na kuondosha woga wakati wa
kugombea nafasi za Uongozi ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Dkt. Mzuri ameyasema hayo jana wakati akifungua mafunzo ya
siku mbili ya uongozi kwa vijana wa kike, yenye lengo la kuwajengea uwezo wa
kuungana pamoja na kuleta ushawishi katika maendeleo ya agenda mbalimbali za
kitaifa.
Amesema kwa sasa dunia imetambua umuhimu wa mwanamke na imeamini
kwamba mwanamke ni Kiongozi kutokana na maendelo tofauti yaliyoletwa na
viongozi wanawake duniani.
“Mwanamke ni kiongozi bora, na nyinyi vijana ndio
tunawategemea muwe na maono ya mbali katika kuleta uongozi ulio imara na
kuibeba nafasi ya mwanamke katika
uongozi, mwanamke anaweza kuwa mama, mke, mfanyakazi na kiongozi na wakati
huohuo na akaweza kutekeleza majukumu
yote hayo na akafanya vizuri katika kila sekta”, Dkt. Mzuri Issa , Mkurugenzi TAMWA ZNZ.
Akitoa mafunzo hayo kwa vijana wa kike 15, Mkufunzi wa
masuala ya Uongozi, Imelda Lulu Urrio amesema lengo la mafunzo hayo ni
kuwajengea uwezo kujitambua na kutambua nafasi zao ili kufikia ndoto zao katika
harakati za Uongozi.
“Nafasi ya wanawake kwa sasa inazidi kuongezeka kwa sababu
kuna ukuwaji wa Elimu kwa jamii na hata watoto wa kike wenyewe wameanza
kujitambua na kujielewa, tumeona baadhi ya jamii inavyowajenga watoto wa kike
kujitambua na kupelekea ongezeko kubwa la viongozi wanawake”, alisema mkufunzi
huyo.
Nae Maryam Ame, mratibu wa mradi wa kuwawezesha wanawake
kushika nafasi za Uongozi (SWIL) unaotekelezwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway amesema
mda mrefu imeonekana wanawake wameachwa nyuma katika ngazi za maamuzi hivyo kwa
sasa wanawake watumie fursa na haki yao ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa
ili kufikia dhamira ya 50/50 katika
masuala ya uongozi.
Aidha washiriki wa mafunzo hayo wamesema wamefarijika kupata
mafunzo hayo kwani yanawajenga kuwa viongozi bora na kuahidi kuwatakuwa
mabalozi wazuri kwa wanawake na kupambana kugombania nafasi za ngazi za juu ili
kuondosha mfumo dume uliotawala katika jamii.
“Matarajio yangu baada ya mafunzo haya ni kuwa Kiongozi
mwenye kujiamini, na nitapambana kuwa kiongozi wa ngazi za juu zaidi katika
chuo changu,” alieleza Hudhaimat Haji Juma, mwanafunzi wa Shahada ya Pili ya
Uhasibu katika Chuo Kikuu cha Taifa, (SUZA).
Mafunzo hayo yameendeshwa ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji
wa mradi wa kuwawezesha wanawake kushika nafasi za uongozi (SWIL),
unaotekelezwa kwa pamoja na TAMWA ZNZ, PEGAO NA ZAFELA kwa mashirikiano na
Ubalozi wa Norway.
0 Comments