Waziri lela (aliyevaa nguo nyekundu)akiwahoji wanafunzi
Imeandikwa na Fatma Abrahman - Pemba

Ikiwa ni katika kuelekea siku ya elimu bila ya malipo Zanzibar Waziri wa elimu Zanzibar Mh: Lela Muhammad Mussa amefanya ziara ya kutembelea na kukagua skuli tofauti kisiwani Pemba zilizoweka kambi za kuwaandaa wanafunzi kwa ajili ya mitihani ya taifa.

Kufuatia ukaguzi huo waziri Lela ameonesha kuridhishwa na jitihada za walimu pamoja wazazi  kutokana na muamko wao wa kuwahamsisha wanafunzi na kuhamasika katika kujipatia elimu usiku na mchana.

Amewataka wanafunzi kuendelea kuongeza bidii katika masomo yao Ili kuwa Viongozi bora wa baadae sambamba na kujiwekea misingi imara ya kiuchumi katika harakati zao za baadae.

“serekali ya Mapinduzi imeweka mfumo wa elimu bure Ili kuwapunguzia mzigo wananchi wake, hivyo nyinyi  wanafunzi na hata walimu musibeze juhudi hizi za serikali, someni kwa bidii, mafanikio ni yenu” amesema waziri huyo.

Katika hatua nyengine waziri Lela amewanasihi  wanafunzi kujitahidi kuelekea katika masomo ya sayansi ikiwemo hasa somo la fizikia Ili kuondosha mwanya ambao upo, mwanya wa kupungukiwa wataalamu hao  visiwani Zanzibar.

Nae Afisa Elimu mkoa wa Kusini Pemba Ndugu  Muhammad Shamte amempongeza waziri wa elimu kwa kuziara hiyo huku akisema kuwa imepelekea wanafunzi kuona viongozi wao wanawajali na ndio maana usiku na mchana wapo tayari kutaka kujua maendeleo yao.



Kwa upande wao wanafunzi wa skuli mbalimbali zilizotembelewa usiku wa jana wamesikika wakisema kuwa, hawakutarajia kupokea ugeni kama huo usiku, kwao imekbaki kuwa ni tukio la kushtukiza na kwa namna moja au unyengine limepelekea kujiweka tayari muda wote kuwa katika mchakato wa masomo.

Ziara iliyofanywa jana usiku na waziri Lela,  ilikutanisha baadhi ya skuli za Mikoa yote miwili ya Pemba ambazo ni skuli za Sekondari Madungu, Dokta Salim Ahmed Salim, Kiuyu Minungwini msingi na Sekondari, Mchangamdogo pamoja na Skuli ya Dokta Ali Mohammed Shein.