Imeandikwa na Fatma Abrahman - Pemba

Waalimu Kisiwani Pemba wametakiwa kuzitumia fursa za kujiunga na Mifuko ya Bima ili kuweza kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili katika maisha ikiwemo, Afya mali, Ajali pamoja na majanga mengine mbali mbali.
Ushauri huo umetolewa na mkuu wa wilaya ya Chake chake Abdalla Rashid Ali alipokuwa akizungumza na waalimu katika ufunguzi wa mafunzo maalumu ya utowaji wa elimu ya bima yalioandaliwa na mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania TIRA kwa wanachama wa Saccos ya walimu Pemba yaliofanyika katika ukumbi wa Tibirinzi Chake Chake Mapema leo.
Amesema kujiunga na Bima mbali mbali ni moja kati ya hakiba zitakazosaidia kukabiliana na majanga yasioepukika kwa mtu mmoja mmoja au kikundi na kuweza kupata usaidizi wa kujikimu pindi yanapotokea.
Aidha Rashid Ameitaka mamlaka hiyo kuendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoendelea kulalamikiwa na wanachama wanaojiunga na bima mbali mbali ikiwemo kucheleweshewa fidia wanapopatwa na majanga pamoja na kuchelewa kupatiwa bima mpya kwa baadhi ya bima ambazo zimemaliza muda wake.
Naibu kamishna wa Mamlaka hiyo zanzibar Khadija Issa Said amewataka Walimu hao kisiwani Pemba kuanzisha uwakala wa bima katika Taasisi zao Ili kurahisisha kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo kwa urahisi.