Imeandikwa na Maryam Nassor
WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa sheria mpya ya habari kutokana na kuwa bado ni kitendawili.
Akizungumza katika kikao cha majadiliano ya sheria kandamizi za habari , katika ofisi kuu ya TAMWA ZNZ , huko Tunguu Unguja mjumbe wa bodi hiyo Bi Hawra Shamte alisema bado kuna utata mkubwa kuhusu sheria hiyo.
Alisema, kiukweli hiyo sheria haijulikani imefikia hatua gani na iko wapi kwasasa, kutokana na kuwa kila mmoja anasema la kwake.
“ Tulitegemea siku ya uhuru wa habari tungeambiwa kuhusu sheria hiyo kuwa, imefikia wapi au lini itazinduliwa lakini bado hatujui hatua iliyofikiwa”, Alisema.
Aidha, aliwataka wandishi wa habari kuendelea kufanya uchechemuzi juu ya upatikanaji wa sheria mpya ya habari nchini.
Mratibu wa baraza la habari Tanzania kwa upande wa Zanzibar,Bishifaa said Mohamed, alisema kuwa, waandishi waendelee kupaza sauti zao kudai sharia mpya ya habari.
Alisema kuwa,kutokana na kuwepo haja ya sheria rafiki kwa wandishi, hali hiyo imezidi kwasasa kutokana na kuwa wandishi wahabari wanakosa uhuru wa kujieleza, hata katika siku ya uhuru wa habari.
“ Hii hali ni mbaya kwasasa wandishi wa habari wanakosa uhuru wa kujieleza hata katika siku ya uhuru wa habari, wakajieleze wapi’’ alisema.
Nae, Salum Said ambae ni mwandishi wa habari mkongwe , alisema kuwa sheria zilizopo haziumizi tu, uhuru wa habari bali zinawaumiza wananchi kwa ujumla.
Alisema kuwa, uhuru wa habari hauwezi kupatikana endapo kutakuwa na sheria kandamizi ambazo zinawakandamiza wandishi na wananchi.
Aidha, aliwasihi wandishi wa habari nchini kuendelea kufanya ufuatiliaji ili sheria mpya ya habari ipatikane kutokana na kuwa ni zaidi ya miaka 20 sasa wamekuwa wakiifuatilia sheria hiyo.
Wakichangia katika kikao hicho, baadhi ya waandishi wa habari walisema kuwa. Wamekuwa wakikutana na vikwazo vingi katika kufanikisha majukumu yao, hali inayowasababishia kukosa uhuru na kuwajibika ipasavyo.
Kikao hicho cha siku moja, kimeandaliwa na TAMWA ZNZ kwa wandishi na wadau wa habari kwa lengo la kuendelea kufanya ufuatiliaji wa sheria mpya za habari nchini.
0 Comments