Imeandikwa na Fatma Abrahman - Pemba

WAANDISHI wa habari kisiwani Pemba wametakiwa kufuata maadili ya kazi zao, ili kuepuka kuingia kwenye makosa mbali mbali.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari, juzi Mei 18, 2024 uliofanyika ukumbi wa Chuo cha Samail Gombani Chake chake Pemba, , Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud alisema, mwandishi wa habari aliesomea fani ya habari hawezi kuvunja miiko na maadili.
Alisema kuwa, tasnia ya habari sasa imevamiwa na watu ambao hawakusomea fani hiyo, jambo ambalo linaweza kusababisha migogoro katika jamii hivyo ipo haja kwa waandishi wa habari kuzingatia maadili wakati wa kazi zao ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza.

Aidha aliwataka waandishi kuelimisha jamii juu ya kuhifadhi mazingira, ili yawe safi na kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa yakiathiri maisha ya wananchi.
Kwa upande wake Afisa Mdhamini Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau amesema, waandishi wa habari wana wajibu wa kuwatumikia wananchi, hivyo ni vyema kuibua kero zinazowakabili wananchi wa maeneo mbali mbali.
Nae Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC) Bakar Mussa Juma amesema, wame viongozi mbali mbali na jamii Kwa ujumla kuendelea kuwapa ushirikiano ili wapate habari na kuzisemea kwani waandishi wa jumuiya hiyo Wanafanya kazi Vizuri na kuzingatia maadili ya habati.
Amesema kuwa klabu ina malengo makubwa ya kuanzisha radio na television ili waajiri waandishi wao, ambapo kwa sasa wameanza na blogi ambayo inawapatia mafanikio makubwa katika tasnia hiyo.

Akiwasilisha mada katika maadhimisho hayo mwandishi wa habari na Mjumbe kutoka PPC Gaspar Charles alisema, waandishi wa habari wana jukumu la kulinda na kuelimisha jamii kuhifadhi mazingira ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Maadhimisho hayo ya siku ya Uhuru wa Habari yamefanyika katika Ukumbi wa Samaail Gombani Chakechake Pemba ambayo yameandaliwa na Clabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC) kwa ufadhili wa Umoja wa Vilavu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC)