Vita wafanyabiashara, machinga yaanza upya Iringa, wafanyabiashara wagomea tozo

WAFANYABIASHARA wa Manispaa ya Iringa, wakiongozwa na Shirikisho la Machinga, Umoja wa Masoko Manispaa ya Iringa, na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT-Iringa), wameazimia kutolipa tozo na ushuru wa manispaa kama hatua ya kushinikiza kuondolewa kwa wafanyabiashara holela waliovamia maeneo yasiyo rasmi.

Akisoma azimio hilo mbele ya wafanyabiashara wanaopinga biashara holela katika mtaa wa mashine tatu mjini Iringa, Katibu wa JWT-Iringa, Corla Benito, alisema:

“Hali ya biashara katika maduka yetu imekuwa mbaya na yenye hasara kutokana na wafanyabiashara holela kuziba milango ya maduka ya wafanyabiashara rasmi.

Alisema uamuzi huo utaendelea hadi pale mamlaka husika zitakapohakikisha kuwa wafanyabiashara hao holela wamerudishwa katika maeneo walioyopangiwa kufanyia biashara zao.

“Tumechoshwa na hali hii. Kuanzia leo April mosi tunasitisha malipo ya leseni za biashara, ushuru wa huduma, ushuru wa mazao yanayoingia na kutoka, ushuru wa taka, pamoja na tozo nyingine zote za manispaa hadi pale haki yetu itakapotekelezwa,” alisema Benito.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Machinga Iringa Mjini, Kessy Dandu, alisema kuwa wafanyabiashara waliopangwa katika masoko rasmi kama Mlandege na Olophefa wamepata hasara kubwa kwa sababu wateja wao wameelekeza manunuzi kwa wafanyabiashara holela waliorudi na kuvamia maeneo yasiyo rasmi.

“Na sisi hatutaendelea kukaa katika masoko yaliyotengwa wakati wenzetu wanaendelea kufanya biashara kiholela barabarani. Kuanzia sasa, tunarejea maeneo yasiyo rasmi hadi pale serikali itakapotekeleza makubaliano ya awali ya kuwaondoa wafanyabiashara holela,” alisema Dandu.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Masoko Manispaa ya Iringa, Raphael Ngulo, alisema kuwa hali ya biashara katika masoko rasmi imezorota kutokana na wimbi la wafanyabiashara holela wanaotumia barabara, maeneo ya wazi, na hata milango ya masoko rasmi kufanya biashara zao.

Hali hiyo alisema imesababisha wafanyabiashara waliopangishwa maeneo rasmi kupata hasara kubwa.

“Tunalazimika kusitisha kulipa tozo zote za manispaa hadi pale mamlaka husika zitakapochukua hatua madhubuti za kuwaondoa wafanyabiashara holela,” alisema Ngulo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JWT-Iringa, Peter Mtalo, alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wafanyabiashara wengi wanaoathiriwa na wafanyabiashara hao holela.

Alisema walichelewa kuchukua uamuzi huo kwa kuwa waliamini mamlahka zinazohusika zingeyafanyia kazi malalamiko yao kwa wakati, na kwamba sasa ni wakati wa kuchukua msimamo madhubuti.

“Wafanyabiashara holela wameathiri biashara zetu kwa kiasi kikubwa. Tumefanya vikao zaidi ya 40 kabla ya kufikia hatua hii,” alisema.

Alisema Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa kupitia Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Exaud Kigahe iliahidi kwamba ifikapo Februari 28, 2023, suala la machinga kufanya biashara katika maeneo yasio rasmi litakuwa limetatuliwa.

Hata hivyo alisema baada ya machinga kutengewa maeneo yao na kupelekwa huko hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa, na badala yake wameendelea kuongezeka katika maeneo yasio rasmi.

Katika hatua nyingine, viongozi wa mashirika haya wametangaza kuwa wanawasilisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa ili suala hili lishughulikiwe haraka na kurejesha utaratibu wa biashara wenye haki kwa wote.

“Biashara ndio maisha yetu, zinatufanya tulipe kodi na kuendesha familia zetu. Tunahitaji mazingira ya biashara yaliyopangwa na yenye tija,” alisema

Hatua hii ya wafanyabiashara inatoa shinikizo kwa mamlaka kuhakikisha kuwa kila mfanyabiashara anafanya biashara katika eneo rasmi alilopangiwa, huku wakisisitiza kuwa hawatarudi nyuma hadi haki yao ipatikane.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada hakuweza kupatika kujibu hatua iliyochukuliwa na wafanyabiashara hao na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Chanzo:habarileo.co.tz

Post a Comment

0 Comments