Wananchi kisiwani Pemba wametakiwa kutowadharau na kuishi nao kwa wema
wananchi wenye mahitaji maalum wakiwemo mayatima na wenye ulemavu ili
nao kujihisi wanathamani katika jamii zao.
Hayo yalielezwa na Mwakilishi wa jimbo la Micheweni ambae pia ni
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji na Mifugo Shamata Shaame Khamis wakati
akitoa sadaka kwa watu wenye mahitaji maalumu Wilaya ya Micheweni .
Alisema ndani ya wilaya ya Micheweni watu wenye mahitaji maalum walio
wengi wamekuwa wakikosa msaada wowote na kufikiwa wachache hivyo
aliiomba Serekali na taasisi binafsi pamoja na wahisani kuwaona pamoja
na kuyasaidia makundi hayo ili kuwapunguzia maumivu walionayo.
Alifahamisha kuna kundi ambalo wameondokewa na wenza wao ni mayatima
hawa bila ya kuwasaidia wanakuwa na majonzi mara mbili zaidi na wale
wenye Ulemavu na wao wanajiona wanatengwa na jamii .
‘’ Ni vyema makundi haya tukawa na utamaduni wa kuyasaidia kwa kila
hali ili yasijione yametengwa na jamii ama wahisani wengine’’,
alisema.
Kwa upande wake kiongozi wa jumuiya ya watu wenye mahitaji maalumu
Juma Kombo Hija mara baada ya kupokea sadaka hio alisema bado Serekali
inahitajika kutoa msukumo katika kuwasaidia makundi haya hasa katika
mwezi wa Ramadhan na Sikukuu ili nao kuwa katika furaha kama wengine
Nao wahusika wa makundi hayo Tufe Ali Shapandu na Omar Hassan Omar
walitoa pongezi kwa Mwakilishi wao sambamba na kumtakia dua ili kuwa
na moyo wa kujitoa kwa wananchi wake hasa wenye mahitaji maalum.
Katika zoezi hilo ambalo limefanyika Wilayani humo liligusa kwa kina
hisia za watu wenye mahitaji maalumu na kumuomba Mwakilishi kuwa na
mwendelezo wa sadaka hizo hata katika miezi mengine.