Watu Kumi (10) wakiwemo wanaume wawili na Wanawake nane wamejeruhiwa baada ya Treni ya abiria ya Mjini ambayo iliyotoka Stesheni ya KAMATA leo Mei 13, 2025 majira ya saa 10:00 jioni kuelekea Pugu Jijini Dar es Salaam kupata ajali kwenye makutano ya reli na barabara ya Kawawa majira ya saa 10:05 jioni.
Kufuatia ajali hiyo iliyohusisha mabehewa 12 yaliyobeba abiria takribani 1,200, wataalamu wa Shirika pamoja na timu ya afya ya Shirika, walifika na kutoa msaada wa huduma ya kwanza ambapo majeruhi hao wamekimbizwa hospitali ya Rufaa ya Amana kwa matibabu zaidi.
Taarifa ya leo iliyotolewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) imeeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ambayo imesababisha mabehewa 6 kuathirika bado hakijafahamika huku Shirika hilo likiuarifu umma kuwa huduma ya usafiri wa treni ya mjini kwenda Pugu, utaendelea kesho kama kawaida.
0 Comments