MKE WA RAISI MAMA MARIAM MWINYI APANIA KULETA MABADILIKO YA WATOTO ZANZIBAR


MKE wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mama Mariam Mwinyi amesema ana imani kuwa malezi na makuzi bora ya awali ya mtoto ni msingi imara wa kujenga taifa lenye raia wenye afya, elimu, nidhamu na maendeleo endelevu.
Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo Agosti 13, mwaka 2025, wakati alipozindua Kampeni ya Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto wa Zanzibar (ECD) katika viwanja vya Kisonge, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Amesema kuwa, ni vyema kwa jamii kuhakikisha inawapatia watoto malezi na makuzi bora ya awali, ili kuwajengea mustkbali wa maisha bora ya baadae.
Mama Mariam Mwinyi ameeleza kuwa, ZMBF imekuwa mstari wa mbele kusaidia maendeleo ya makuzi ya mtoto, hususan katika programu za lishe pamoja na huduma za afya ya mama na mtoto, ambapo kupitia jitihada hizo, imeweza kuwafikia wanufaika zaidi ya 50,000 katika Shehia 67 na vijiji 644 vya Unguja na Pemba.

Alisema kuwa, kupitia kampeni ya Afya Bora Maisha Bora, kambi za matibabu bure zilizoendeshwa na ZMBF zimewafikia wananchi 21,000 na huduma hizo zimejumuisha elimu ya lishe, elimu ya malezi na makuzi, matibabu kwa watoto wenye utapiamlo, utoaji wa chanjo, pamoja na huduma za afya ya mama na mtoto.

Aisha amefahamisha kuwa, uzinduzi wa kampeni hiyo haipaswi kuwa tukio la siku moja, bali iwe ni harakati ya muda mrefu na endelevu ili kuhakikisha kila mtoto wa Zanzibar, kuanzia hatua ya mama katika ujauzito hadi umri wa miaka minane, anapata haki zake za msingi ikiwemo afya bora, lishe sahihi, ulinzi, malezi na mazingira salama ya ukuaji kwa ajili ya kufikia utimilifu wake.

Kwa upande mwingine, Mama Mariam Mwinyi ametoa wito maalum kwa sekta binafsi na mashirika ya maendeleo kuendeleza ushirikiano na Serikali katika uwekezaji wa malezi na makuzi ya awali ya mtoto.

Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui alisema, siku ya uzinduzi huo ni ya kihistoria kwa Zanzibar kwani inaanza hatua mpya ya kuhakikisha watoto wanapata mwanzo bora maishani.         

Amesema kuwa, utafiti wa kisayansi na uzoefu wa kitaifa na kimataifa vinaonesha bayana kuwa, miaka ya mwanzo ya maisha ya mtoto ndio msingi wa afya, akili na utu wa mtu mzima wa baadae, hivyo jamii ikiimarisha vizuri itapata kizazi chenye afya njema, ubunifu na maadili mema.
Waziri huyo alisema, Wizara imedhamiria kasi ya utekelezaji wa mikakati ya kupambana na changamoto za lishe na malezi chanya, kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto, kupanua huduma za uchunguzi na ufuatiliaji wa afya ya watoto, kuweka mazingira rafiki ya watoto kupata huduma na kucheza katika vituo na hospitali.

Nae Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Riziki Pembe Juma alieleza, Wizara ina jukumu la kuhakikisha watoto wote wanakuwa katika ustawi mzuri wa maisha yao yote, hivyo watashirikiana na taasisi zote zinazotoa huduma kwa mtoto, ili kufikia lengo.

‘’Kama tunavyofahamu ili mtoto akue vizuri pamoja na muelekeo sahihi katika makuzi yake, basi anahitaji kupatiwa vitu vyake vyote muhimu ili aweze kukua timilifu ambavyo ni afya bora, lishe nzuri, ulinzi na usalama, uchechemuzi wa awali na kujifunza kwake pamoja na malezi yenye mwitiko chanya kutoka kwa wazazi na jamii,’’ alisema Waziri huyo.

Alieleza kuwa, wamekuwa wakisimamia vyema Sheria ya mtoto ikiwemo nambari 6 ya mwaka 2011, sera na miongozo iliyopo, ili kuhakikisha sekta zote zinatekeleza utoaji wa huduma bora kwa watoto, ili kuwakuza katika muelekeo sahihi wa makuzi yao.

Mwakilishi kutoka Shirika la kuhudumia Watoto UNICEF Laxmi Bhawany alifafanua kuwa, uwekezaji wa mapema kwa watoto wadogo haswa katika siku 1,000 za mwanzo ikijumuisha miezi tisa ya ujauzito hadi kufikia miaka miwili ya kwanza, ni muhimu sana kwani asilimia 80 ya ukuaji wa mwili na ubongo unakamilika.
Alisema sayansi inaonesha kuwa, nyakati za awali za mtoto sio muhimu kwa maisha ya mtu binafsi pekee, bali huchangia katika mustakbali wa jamii, hivyo uwekezaji katika ukuaji wa watoto wachanga unaleta manufaa ya kudumu ambayo ni matokeo bora ya elimu, familia zenye afya na uchumi imara.

‘’Wakati wa mabadiliko ni sasa na yanaanza na sisi, kwa pamoja sisi ni chachu ya mabadiliko haya muhimu, tunaweza kubadilisha maisha,’’ alifafanua.

Ikisomwa risala katika kampeni ya uzinduzi huo, imeelezwa kuwa, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar inatambua kuwa, miaka ya awali ya mtoto ni kuanzia kuzaliwa hadi umri wa kuanza skuli, kwani ndio msingi wa maendeleo yake yote ya baadae.
Alisema kuwa, Wizara imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kila mtoto anapata huduma bora za malezi na makuzi kupitia programu za elimu ya maandalizi katika skuli za Serikali na binafsi.


‘Afya ya mtoto ni afya ya taifa. Lishe bora ni kinga bora. Malezi bora ni msingi wa amani na maendeleo’.

                                         MWISHO.

Post a Comment

0 Comments