Imeandikwa na Tatu Juma - Zanzibar
Chama cha Waandishi wa Habari
Wanawake Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kimetoa mafunzo maalum ya siku moja kwa watoa
huduma za usafirishaji wa umma kutoka Wilaya ya Kaskazini A, Unguja, ikiwa ni
sehemu ya juhudi za kuimarisha mapambano dhidi ya udhalilishaji na ukatili wa
kijinsia katika sekta ya usafirishaji visiwani Zanzibar.
Mafunzo hayo yamewakutanisha
wadau mbalimbali wakiwemo waendesha bodaboda, , madereva wa magari ya abiria,
madereva wa bajaji, askari wa usalama barabarani pamoja na Afisa Takwimu kutoka
Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Lengo la mafunzo hayo ni
kuwajengea uelewa na kuwashirikisha watoa huduma wa usafiri usio rasmi katika
kuzuia na kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake
na watoto wa kike, pamoja na kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata huduma
za usafiri katika mazingira salama na yenye heshima.
Akizungumza katika mafunzo hayo
yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkokotoni, Afisa
Programu kutoka TAMWA-ZNZ, Asia Hakim Makame, amesema mafunzo hayo yataongeza
uwajibikaji kwa watoa huduma za usafiri, kubadili mitazamo hasi kuhusu wanawake
na kusaidia kuifanya sekta ya usafiri kuwa sehemu salama kwa wanawake
wanaotumia usafiri huo na jamii.
0 Comments