KAIMU Ofisa Mdhamini Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Pemba, Sharifa Hamad Shapandu, amezitaka kamati za kufanikisha tamasha la 31 la utamaduni wa mzanzibari, kuhakikisha zinafanyakazi kwa kushirikiana, ili kufanikisha tamasha hilo.
Ameyasema hayo August 18, 2026, ofisini kwake Gombani Chakechake Pemba, mara baada ya kuzizindua kamati hizo tano, kuelekea uzinduzi wa tamasha hilo mwishoni mwa mwezi ujao, kisiwani humo.
Alisema kuwa, kuwepo kwa kamati hizo anataka iwe ni njia rahisi ya kufanikiwa kwa tamasha hilo, ambalo kwa awamu hii, linatarajiwa kuwa la aina yake.
Alieleza kuwa, njia ya kuzigawa kwa kamati hizo, ni namna ya kuwa na na urahisi wa ufuatuliaji, ingawa isiwe chanzo cha kukosa kushirikiana.
‘’Najua kuwa zipo kamati tano, zinawajumbe wenye uwezo na maarifa yasiofanana, lakini hili sasa muwe na ushirikiano kwa pamoja, ili kulifanikisha hili,’’alifafanua.
Aidha Kaimu Ofisa Mdhamini huyo, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika tamasha hilo, tangu kuanza kwa uzinduzi wake wilaya ya Micheweni, ili kujionea mambo mbalimbali ikiwemo, utamaduni wa kizanzibar, michezo, maigizo na ngoma za asili.
"Wananchi wote nawaomba mushiriki kikamilifu, katika tamasha hili la utamaduni wa mzanzibari, ikiwa ni njia moja wapo ya kujionea utamaduni wetu na wingine kujikumbusha,’’alieleza.
Mapema Mkuu wa Divisheni na Utamaduni Pemba Hamad Ali Haji, alisema tamasha hilo litakuwa la aina yake kwa mwaka huu, kwa kuvishirikisha zaidi ya vikundi 10 vya ngoma asili, kutoka Unguja na Pemba.
Alisema, tangu kuanzishwa kwa tamasha hilo, kwa mwaka huu, ambalo ni 31, kwa wanachi watakaojitokeza wataniufaika na mambo makubwa, ikiwemo resi za ngalawa, Punda, msewe wa zamani na sasa, taarab asilia na mbio za baiskeli.
‘’Kwa mwaka huu wizara yetu ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, chini Waziri Riziki Pembe Juma Khamis na Katibu Mkuu Matar, tamasha hili, litakuwa la kuvutia na si la kukosa,’’alisisitiza.
Katika hatua nyingine, alisema tamasha hilo kwa kuanzia, litazinduliwa Septemba 19 hadi 23 mwaka huu kisiwani Pemba, wilaya ya Micheweni na mgeni rasmi akitarajiwa kuwa, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla.
Alifafanua kuwa, kwenye uzinduzi wa tamasha hilo, utafuatiwa na matembezi ya wajasiriamali, wasanii wa ngoma za asili, utenzi na shamra shamra nyingine za kulipamba.
Siku ya pili, tamasha litahamia wilaya ya Wete, litanogeshwa na maulidi ya home, nasheed, dufu na maigizo yanayohusiana na tamaduni wa kiislam na kizanzibari.
‘’Wananchi wa wilaya ya Wete, wanakaribishwa siku hiyo, ukumbi wa zamani wa baraza la Wawakilishi, ambapo hakutakuwa na kiingilio,’’alisema.
Aidha Mkuu huyo wa Divisheni ya Utamaduni Pemba, alisema Septemba 21, kutakuwa na mashindano ya ngalawa, yatakayoambatana na sarakasi na ngoma za asili Mkoani, na siku inayofuata ni mchezo Ng'ombe uwanja Pujini.
‘’Niwaarifu wananchi wa Pemba, tamasha hili litahitimishwa Septemba 23, kwa usiku wa sanaa, pamoja na wajasriliamali, wakionesha shughuli mbalimbali, zikipambwa na kwa taarabu, uwanja wa Gombani, kabla ya kilele Septemba 25 Unguja,’’alieleza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya Habari na Burudani Adam Ramadhani Kombo, ameipongeza wizara, kwa kuendeleza tamasha hilo na kuahidi kamati yake, itafanyakazi kwa karibu na wizara, ili kufanikisha shughuli hiyo.
Aidha aliwataka wajumbe wa kamati hiyo, kuhakikisha, kazi na majukumu waliyopewa wanayafanya kwa ufanisi, ili kuhakikisha wananchi wote wanapata taarifa.
Hili ni tamasha la 31, la utamaduni wa mzanzibari, kufanyika Unguja na Pemba, ambapo kwa mwaka huu, uzinduzi wake unatarajiwa kufanyika Micheweni Septemba 19 mwaka huu.
MWISHO.

0 Comments