Na-Fatma Suleiman-Pemba
Kwa mtoto, familia ndiyo mazingira ya kwanza anayojifunza ndani yake kuhusu upendo, heshima, usalama na namna ya kuwasiliana na watu wengine.
Ni mahali ambapo anatarajiwa kupata ulinzi na malezi yanayomsaidia kukua akiwa na kujiamini, Lakini kwa baadhi ya watoto na wasichana huko Pemba, mazingira haya yamekuwa tofauti, Badala ya usalama, wamekuwa wakikabiliana na matusi, dharau, vitisho, kubezwa na kuitwa majina yanayowavunjia heshima, mara nyingi kutoka kwa watu wa karibu wanaowategemea.
Tatizo hili limekuwa likifichika kwa muda mrefu kwa sababu udhalilishaji wa kisaikolojia hauachi alama inayoweza kuonekana kwa macho. Mtoto anaweza kutukanwa nyumbani, kudhalilishwa mbele ya ndugu au kutishiwa kwa muda mrefu, lakini kesho yake akaenda shule na kuendelea na shughuli zake bila mtu wa nje kujua kinachoendelea. Hali hiyo imeifanya jamii katika baadhi ya maeneo kuuchukulia udhalilishaji huu kama sehemu ya kawaida ya malezi badala ya kuutambua kama aina ya ukatili inayoweza kumuathiri mtoto kiafya na kijamii.
Katika baadhi ya familia, mzazi anapomuita mtoto jina baya au kumdhalilisha mbele ya wengine anaweza kuamini kuwa anatumia njia ya kumrekebisha. Wazazi wengine wanaamini kuwa kumtisha mtoto au kumfanya aone aibu kutamfanya abadili tabia.
Lakini kwa wataalamu, malezi yanapofikia hatua ya kumvunja mtoto heshima na kumfanya aishi kwa hofu, madhara yanaweza kuwa makubwa kuliko kosa ambalo mzazi alitaka kulirekebisha.
Hamad Abdallah, anayefuatilia masuala ya malezi katika jamii kutoka Micheweni Pemba, anasema baadhi ya wazazi bado hutumia maneno ya dharau kama njia ya kumfundisha mtoto.
“Wazazi wamekuwa wakiwaita watoto majina mabaya wakiamini kuwa wanawabadilisha katika tabia njema na kwamba hiyo ni adhabu ili watoto wajirekebishe. Lakini badala yake, maneno hayo yanawaathiri kisaikolojia,” anasema.
Kauli hii inaonyesha changamoto iliyopo katika malezi, ambapo nia ya mzazi kumfundisha mtoto inaweza kuchanganywa na matumizi ya lugha inayomdhalilisha.
Mtoto anayekosea anahitaji kuonyeshwa kosa lake na kusaidiwa kuelewa namna ya kulirekebisha, lakini anapopewa majina ya kumdhalilisha mara kwa mara anaweza kuanza kuamini kuwa yeye mwenyewe hana thamani.
Kwa baadhi ya watoto, madhara hayo huanza kuonekana katika tabia zao. Mtoto anaweza kuwa mkimya, kuanza kujitenga na wenzake, kuogopa kuzungumza mbele ya watu au kupoteza hamu ya kushiriki katika shughuli ambazo awali alikuwa akizipenda.
Wakati mwingine mabadiliko haya hayatazamwi kama dalili ya tatizo, bali mtoto huonekana kuwa mkaidi au mwenye tabia mbaya.
Huko Konde, hali hii imekuwa ikiwakabili baadhi ya watoto na wasichana ambao wamefika kwa viongozi wa jamii wakihitaji msaada baada ya kupitia mazingira ya udhalilishaji wa kisaikolojia.
Semeni Ali, Mratibu wa Shehia ya Konde, anasema tatizo moja kubwa ni kwamba baadhi ya wananchi bado hawajaona umuhimu wa kutoa taarifa wanapokutana na udhalilishaji wa aina hii.
“Watu wengi hawajaripoti. Wanafikiri ni mambo ya kawaida, wengine wanasema ni majini,” anasema.
Semeni pia amewahi kushughulikia kesi ya binti aliyefika akiwa amepitia udhalilishaji wa kisaikolojia. Kisa hicho kinaonyesha namna tatizo hili linavyoweza kufichika ndani ya familia kwa muda mrefu kabla ya mtoto kupata msaada.
"Nilipokea kesi ya msichana ambae alikua anachagawa na kupelekwa kusomewa lakini ilikua akifanyiwa udhalilishaji wa kisaikolojia na msomeaji kwa kumshika maeneo tofauti na alikua hajijui ama hasemi kabisa mpaka mwenzake ambae aliekua na tatizo kama lake kuona hilo ndio kumwambia kua asikubali huo ni udhalilishaji na ni kweli binti aliathirika sana juu ya mkasa huo"
Changamoto ya kutoripoti ndiyo inayofanya iwe vigumu kupata picha kamili ya ukubwa wa udhalilishaji wa kisaikolojia katika jamii.
Wapo watoto wanaoendelea kuvumilia kwa sababu wanamuogopa mzazi au ndugu anayewadhalilisha.
Wengine huogopa kuwa wakisema wataonekana kuwa wamewasaliti wazazi wao, huku baadhi wakiamini kuwa hakuna mtu atakayewaamini.
Lakini takwimu za matukio yaliyoripotiwa zinaonyesha kuwa tatizo hili haliwezi tena kuchukuliwa kama jambo dogo la kifamilia.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali kupitia taarifa ya Jeshi la Polisi Zanzibar ya mwaka 2025 iliyotolewa Januari 2026, matukio 213 ya udhalilishaji wa kisaikolojia yaliripotiwa Zanzibar. Kati ya hayo, matukio 47 yalihusu lugha za matusi, huku 166 yakihusu shambulio la aibu na kukashifu.
Katika matukio hayo, wasichana 122 walitajwa kuwa waathirika, huku wanawake wakiwa 84.
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa wanawake na wasichana wameendelea kuwa miongoni mwa makundi yaliyoathirika zaidi katika matukio yaliyofikishwa kwenye mamlaka.
Hata hivyo, idadi hiyo haiwezi kutafsiriwa kuwa ndiyo ukubwa halisi wa tatizo kwa sababu inahusu matukio yaliyofikishwa na kuripotiwa.
Nyuma ya takwimu hizo kuna swali ambalo bado halina jibu kamili, ni watoto na wasichana wangapi wamepitia hali kama hiyo lakini hawajawahi kutoa taarifa?
Kwa sababu udhalilishaji wa kisaikolojia unaweza kutokea kila siku ndani ya nyumba bila jirani, mwalimu au hata ndugu mwingine kujua. Mtoto anaweza kuendelea kuishi na mzigo huo huku watu wanaomzunguka wakiamini kwamba kila kitu kiko sawa.
Hapo ndipo madhara ya udhalilishaji huu yanapoanza kuwa makubwa zaidi Kwa sababu kadiri mtoto anavyoendelea kuishi katika mazingira ya matusi, dharau na vitisho, ndivyo uwezekano wa kuathirika katika hali yake ya kujiamini na afya ya akili unavyoongezeka.
Na kwa wataalamu wa afya ya akili, hilo si jambo la kupuuzwa.
JERAHA LISILOONEKANA
Madhara ya udhalilishaji wa kisaikolojia hayaishii katika maneno yanayotamkwa wakati wa ugomvi. Kwa mtoto anayekutana na hali hiyo mara kwa mara, maneno yanaweza kuanza kuathiri namna anavyojiona, anavyowasiliana na wengine na anavyokabiliana na changamoto za maisha.
Mtaalamu wa afya ya akili Pemba, Omar Said Othman, anasema watoto wanaokabiliwa na udhalilishaji wa kisaikolojia wanaweza kuonyesha mabadiliko mbalimbali ya kitabia na kihisia, hasa pale wanapokosa mtu wa kuwaeleza wanachopitia.
"Kuna hali tofauti ambayo mtoto huyo huweza kupitia wengine wanaweza tuu ghafla uwezo wake wa kimasomo kushuka, kua mkali ama wakati mwengine kua mnyonge, kua mpole sana, kua na woga, kujitenga, ama hata kushindwa hata kufanya shughuli zake za kila siku na hali hii ndio hupelekea tatizo afya ya akili ".
Ushuhuda wa mtaalamu huyo unaendana na takwimu za Wizara ya Afya zinazoonyesha ukubwa wa changamoto za afya ya akili. Mwaka 2023, wagonjwa 1,240 wa afya ya akili walisajiliwa, huku asilimia 58 ya changamoto hizo zikihusishwa na migogoro na udhalilishaji ndani ya familia.
Hizi ni takwimu za mwaka 2023 na hazipaswi kuchukuliwa kuwa zinaonyesha idadi ya sasa ya wagonjwa. Hata hivyo, zinatoa picha ya namna mazingira ya kifamilia yanavyoweza kuhusishwa na changamoto za afya ya akili.
Wakati huo huo, kuendelea kuripotiwa kwa matukio ya udhalilishaji kunafanya suala la ufuatiliaji wa afya ya akili kuwa muhimu zaidi, hasa kwa watoto na wasichana walio katika mazingira hatarishi.
Changamoto kubwa ni kwamba dalili za mtoto aliyeathirika zinaweza kuchukuliwa kama tabia ya kawaida. Mtoto anayejitenga anaweza kuitwa mwenye majivuno, anayekataa kuzungumza anaweza kuonekana mkaidi, na anayeshindwa kuzingatia masomo anaweza kulaumiwa kwa kutokuwa na bidii.
Katika hali hiyo, sababu ya msingi ya mabadiliko yake inaweza kubaki bila kugundulika.
Wataalamu wanaeleza kuwa mtoto anapokuwa katika mazingira ya kudhalilishwa mara kwa mara, ni muhimu kuangalia mabadiliko yake kwa umakini na kutafuta chanzo badala ya kumhukumu kwa tabia anayoonyesha.
Hata hivyo, madhara ya udhalilishaji wa kisaikolojia hayapo kwa watoto pekee. Kwa wanawake wanaoishi katika mazingira yenye matusi, vitisho na dharau, hali hiyo inaweza kuathiri maisha yao ya kila siku, ikiwemo uwezo wa kufanya kazi na kujipatia kipato.
Rehema Jabu Khamis, mjasiriamali wa bidhaa za mwani, ni miongoni mwa wanawake wanaokabiliana na changamoto hizi huku akiendelea kutafuta maisha kupitia shughuli zake za kiuchumi.
“Kutafuta mwani kuna changamoto, akili haipo, Tunafanyiwa udhalilishaji, Uliza, nyumbani kumejaa matusi,” anasema Rehema.
Kauli yake inaonyesha upande mwingine wa tatizo ambao mara nyingi hauzungumzwi, Mwanamke anapokwenda kutafuta kipato, huenda akawa amebeba mawazo ya kile alichopitia nyumbani, Kazi anayofanya inaweza kuendelea, lakini uwezo wake wa kuzingatia shughuli hizo unaweza kuathiriwa na hali ya kisaikolojia aliyonayo.
Kwa Rehema, shughuli za mwani si suala la kujipatia kipato binafsi pekee, bali ni sehemu ya maisha ya familia na mahitaji ya kila siku.
Hivyo, changamoto inapomfanya ashindwe kufanya kazi kwa utulivu, athari zinaweza kuendelea hadi kwenye uchumi wa familia.
Hali kama hiyo inaonekana pia kwa Saumu Zume Juma, anayefanya biashara ndogo ndogo, ikiwemo kuuza malai kwa wanafunzi shuleni.
Mbali na changamoto za kutafuta wateja na kupata kipato, Saumu anasema amekuwa akikumbana na maneno ya dhihaka na kejeli kutoka kwa baadhi ya watu anaofanya nao shughuli za biashara na wengine katika jamii.
"Jike dume ,mshirikina, mwari kigego yote hayo yananikwaza sana kwani mara zote nikifika lazima naitwa majina mabaya wakati mwengine na wauza biashara wenzangu kwa choyo tuu pale wanaponiona nimeuza zaidi yao".
Ushuhuda wa wanawake hawa unaonyesha kuwa udhalilishaji wa kisaikolojia hauwezi kuangaliwa kama tatizo linalobaki ndani ya nyumba pekee.
Unapomuathiri mtu kisaikolojia, madhara yanaweza kuonekana katika maeneo mengine ya maisha, ikiwemo kazi, biashara, mahusiano na uwezo wa kushiriki katika shughuli za jamii.
Kwa mwanamke anayejitegemea kupitia biashara ndogo, kujiamini ni sehemu ya msingi ya shughuli zake. Anahitaji kuzungumza na wateja, kushirikiana na watu wengine na kufanya maamuzi kuhusu biashara yake. Lakini anapokuwa katika mazingira yanayomdhalilisha mara kwa mara, hali yake ya kujiamini inaweza kuathirika.
Hii ndiyo sababu wataalamu wanasisitiza kuwa afya ya akili inapaswa kuangaliwa pamoja na mazingira ambayo mtu anaishi. Kumpeleka mhanga kupata ushauri pekee hakutoshi ikiwa mazingira yanayomsababisha msongo wa mawazo bado yanaendelea.
Katika familia, kwa mfano, mtoto anaweza kupewa ushauri na kuanza kupata nafuu, lakini akirudi katika mazingira yale yale ya matusi, vitisho na dharau, tatizo linaweza kuendelea.
Kwa upande wa wanawake, hali inaweza kuwa ngumu zaidi ikiwa wanategemea mtu anayewadhalilisha kwa mahitaji ya msingi ya maisha. Hofu ya kupoteza msaada wa kifedha au kuvuruga familia inaweza kuwafanya wengi kuchagua kukaa kimya.
Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia Zanzibar ya mwaka 2017 inatambua udhalilishaji wa kisaikolojia miongoni mwa aina za ukatili ndani ya familia. Pamoja na utambuzi huo, bado kuna changamoto ya kuhakikisha jamii inauelewa udhalilishaji huu na wahanga wanapata njia salama za kutoa taarifa.
Hapa ndipo suala la sheria linapoingia.
Zanzibar ina mfumo wa sheria unaokataza vitendo mbalimbali vya ukatili na udhalilishaji.
Sheria ya Adhabu ya Zanzibar ya mwaka 2018 pamoja na marekebisho yake imeweka masharti yanayohusu vitendo vya ukatili na matumizi ya lugha au vitendo vinavyomdhalilisha mhanga.
Lakini kwa mhanga ambaye hajui haki zake, sheria iliyopo inaweza kubaki kuwa maandishi yasiyomsaidia.
Amina Ahmed Mohd, Kaimu Mratibu wa TAMWA Pemba ambapo kupitiamradi wa GBV, anasema kuongeza uelewa wa jamii na kuwafikia wahanga mapema ni sehemu muhimu ya kupunguza tatizo hili.
"Tamwa tunachukua hatua mbalimbali katika kuhakikisha Tunapambana na udhalilishaji ikiwemo kutoa elimu kupitia vyombo vya habari katika kuhakikisha vitendo hivi vinaondoka kabisa hivyo ni suala la wanajamii kuacha ili kumuacha mtoto wa kike na msichana kua salama lakini kikubwa jamii iache maneno ya dhihaka matusi kwani udhalilishaji huu huuchukulia kama ni kitu cha kawaida"
Kwa Amina, suala hili linahitaji jamii kuacha kuona matusi, vitisho na dharau kama migogoro ya kawaida ya familia. Pale vitendo hivyo vinaporudiwa na kuanza kumuathiri mtu, vinahitaji kuchukuliwa kwa uzito na mhanga apewe msaada unaostahili.
Changamoto nyingine ni namna jamii inavyotafsiri tabia ya mtoto. Katika mazingira ambayo adhabu kali na lugha za dharau zimezoeleka, mtoto anayelalamika anaweza kuonekana hana nidhamu badala ya kuonekana kama mtu anayehitaji msaada.
Hii ndiyo sababu mabadiliko ya malezi yanatajwa kuwa sehemu muhimu ya kupunguza udhalilishaji wa kisaikolojia.
Maryam Yusuf Saleh, Mhamasishaji wa Jamii kutoka Micheweni, anaamini wazazi wana nafasi kubwa katika kuhakikisha watoto wanalelewa bila kutumia lugha inayowavunjia heshima.
"Kumwita mtoto mbwa, mbuzi sio kumfundisha abadu ama kumkanya bali ni udhalilishaji wa wazi kabisa na inamvunjia heshima yake na kumuathiri kisaikolojia hicyo jamii tunaiharibu kesho ya watoto wetu wenyewe tubadilike"
Kwa upande mwingine, Hamad Abdallah anasema wazazi wanapaswa kuelewa kuwa kumrekebisha mtoto na kumdhalilisha ni mambo mawili tofauti. Mtoto anaweza kupewa mipaka na kuelekezwa bila kuitwa majina mabaya au kufedheheshwa mbele ya watu wengine.
Kwa mtazamo huo, mapambano dhidi ya udhalilishaji wa kisaikolojia hayawezi kuachwa kwa taasisi za sheria pekee.
Yanahitaji pia mabadiliko katika namna familia zinavyowalea watoto na namna jamii inavyotafsiri tabia za watoto na wanawake wanaoomba msaada.
Na wakati mjadala kuhusu sheria, afya ya akili na malezi ukiendelea, swali kubwa linabaki kwa familia yenyewe: je, mtoto anayekulia katika mazingira ya matusi ana nafasi gani ya kujenga maisha yenye kujiamini ikiwa watu wanaopaswa kumjenga ndio wanaomvunja?
Jibu la swali hilo linaweza kuamua kama tatizo hili litaendelea kuwa sehemu ya maisha ya kawaida au jamii itaamua kulichukulia kama suala la ulinzi wa mtoto na afya ya jamii.
SHERIA IPO, LAKINI NANI ATAMLINDA MTOTO?
Tatizo la udhalilishaji wa kisaikolojia linapofikishwa katika ngazi ya familia pekee, mara nyingi huishia katika mazungumzo ya kusuluhisha ugomvi bila kuchunguza madhara ambayo tayari yameanza kumpata mhanga.
Kwa mtoto au msichana anayepitia hali hiyo kwa muda mrefu, suluhu ya haraka inaweza isiwe ya kutosha ikiwa mazingira yaliyosababisha tatizo bado yanaendelea.
Hii ndiyo sababu wataalamu na watetezi wa haki za wanawake na watoto wanasisitiza umuhimu wa jamii kuelewa kuwa si kila jambo linalotokea ndani ya familia linapaswa kufichwa kwa kisingizio cha kulinda heshima ya familia.
Katika baadhi ya mazingira, wazazi au ndugu wanaweza kuamua kutoripoti tukio kwa kuhofia kuvuruga mahusiano ya kifamilia. Wengine huona kuwa mtoto akilalamika dhidi ya mzazi wake amekosa heshima, wakati wengine huamini kuwa matusi na vitisho ni sehemu ya kawaida ya malezi.
Mtazamo huu unaweza kumfanya mtoto asiwe na mahali pa kwenda anapopitia udhalilishaji.
Semeni Ali, Mratibu wa Shehia ya Konde, anaeleza kuwa changamoto ya kwanza ni kuwafanya wananchi waone umuhimu wa kutoa taarifa pale wanapokutana na matukio ya udhalilishaji.
Amesema baadhi ya wananchi bado wanaona matukio hayo kama migogoro ya kawaida ya familia au mambo ambayo yanapaswa kusuluhishwa nyumbani.
Hata hivyo, pale mhanga anapokuwa mtoto, suala hilo linahitaji kuangaliwa kwa mtazamo mpana zaidi kwa sababu mtoto hana uwezo sawa na mtu mzima wa kujilinda au kujiondoa katika mazingira yanayomuumiza.
Mtoto anayemtegemea mzazi kwa chakula, malazi, elimu na mahitaji mengine ya msingi anaweza kushindwa kusema ukweli kuhusu anachopitia kwa sababu anahofia madhara yatakayofuata.
Kwa sababu hiyo, jukumu la kumlinda mtoto haliwezi kuwekwa kwake mwenyewe. Wazazi, ndugu, walimu, viongozi wa jamii, wataalamu wa afya na taasisi za utekelezaji wa sheria wote wana nafasi katika kutambua na kushughulikia dalili za udhalilishaji.
SHERIA NA UTEKELEZAJI
Zanzibar ina sera na sheria zinazolenga kulinda wanawake na watoto dhidi ya ukatili na udhalilishaji. Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia Zanzibar ya mwaka 2017 inatambua changamoto ya ukatili wa kijinsia na umuhimu wa kulinda haki na usalama wa wanawake.
Aidha, Sheria ya Adhabu ya Zanzibar ya mwaka 2018 pamoja na marekebisho yake inaweka masharti kuhusu makosa mbalimbali yanayohusiana na ukatili na udhalilishaji.
Lakini uwepo wa sheria pekee hauwezi kumaliza tatizo ikiwa wahanga hawajui haki zao, familia hazijui wapi pa kutoa taarifa na jamii inaendelea kuhalalisha baadhi ya vitendo kwa kisingizio cha malezi.
Kwa upande wa wataalamu wa afya ya akili, hatua ya kwanza si kusubiri mtoto afikie kiwango cha juu cha msongo wa mawazo. Ni muhimu kutambua dalili mapema na kumsaidia mtoto kabla tatizo halijawa kubwa.
Mtoto anayebadilika ghafla katika tabia, anayejitenga na wenzake, anayekuwa na hofu isiyoelezeka au anayeshindwa kuendelea na shughuli zake za kawaida anahitaji kuangaliwa kwa umakini.
Haimaanishi kila mabadiliko ya kitabia yanatokana na udhalilishaji. Lakini mabadiliko makubwa yanahitaji mzazi au mlezi kuzungumza na mtoto na kutafuta sababu yake badala ya kumhukumu.
MALEZI YANAYOHITAJI MABADILIKO
Kwa jamii ya Pemba, ambako familia ina nafasi kubwa katika malezi ya watoto, mabadiliko yanapaswa kuanzia nyumbani.
Wazazi wanahitaji kuelewa kuwa nidhamu ni muhimu, lakini nidhamu haihitaji kumdhalilisha mtoto. Mtoto anaweza kuonywa, kupewa mipaka na kupewa adhabu inayofaa bila kutumia lugha inayomvunjia heshima.
Maryam Yusuf Saleh, Mhamasishaji wa Jamii kutoka Micheweni, anaona kuwa wazazi wanahitaji kuelimishwa zaidi kuhusu madhara ya maneno wanayotumia wanapowalea watoto.
Shuwekha Salum Kombo, mhamasishaji wa jamii, anasema familia inapaswa kuwa mazingira ya kwanza ya kumjenga mtoto.
“Familia ndiyo shule ya kwanza ya mtoto. Kama shule hiyo inafundisha matusi, tuibadili iwe shule ya upendo,” anasema.
Kauli hii inaweka wajibu mkubwa kwa wazazi na walezi, lakini pia kwa jamii inayowazunguka. Mtoto anayesikia matusi na dharau mara kwa mara anaweza kukua akiwa amejifunza kuwa lugha hiyo ni sehemu ya kawaida ya mahusiano.
Kwa hiyo, kubadilisha lugha inayotumika katika familia ni sehemu ya kubadilisha namna watoto wanavyokua na kujenga mahusiano yao ya baadaye.
TATIZO LINAHITAJI MWITIKIO WA PAMOJA
Udhalilishaji wa kisaikolojia hauwezi kumalizwa na taasisi moja. Polisi wanahitaji taarifa ili waweze kuchukua hatua pale sheria inapokiukwa. Wataalamu wa afya wanahitaji wahanga kufika kupata huduma. Viongozi wa jamii wanahitaji kutambua matukio na kuwaunganisha wahanga na huduma zinazofaa.
Familia nayo inahitaji kubadili mtazamo wa kuona matusi na dharau kama njia ya kawaida ya malezi.
Kwa upande wa shule, walimu wanaweza kuwa watu muhimu katika kutambua mabadiliko ya mtoto kwa sababu hutumia muda mwingi pamoja na watoto. Mtoto anayebadilika kitabia, kushuka ghafla katika masomo au kujitenga na wenzake anaweza kuwa anapitia changamoto ambayo hawezi kuieleza nyumbani.
Hivyo, ulinzi wa mtoto unahitaji mfumo unaowawezesha watu mbalimbali kushirikiana badala ya kila taasisi kufanya kazi peke yake.
TAKWIMU ZINAPASWA KUWA MWITO WA HATUA
Matukio 213 ya udhalilishaji wa kisaikolojia yaliyoripotiwa Zanzibar mwaka 2025 hayawezi kupuuzwa. Ndani yake kuna wasichana 122 na wanawake 84 waliotajwa kuwa waathirika.
Lakini takwimu hizo zinapaswa pia kutafsiriwa kwa tahadhari kwa sababu zinahusu matukio yaliyoripotiwa, si lazima yawe matukio yote yaliyotokea.
Hivyo, changamoto kubwa si kuangalia tu kama idadi ya kesi imeongezeka au imepungua, bali kuhakikisha mifumo ya kuripoti inafanya kazi, wahanga wanaamini taasisi zinazowahudumia na huduma za afya ya akili zinapatikana kwa wakati.
Takwimu za wagonjwa 1,240 wa afya ya akili zilizosajiliwa mwaka 2023, ambapo asilimia 58 zilihusishwa na migogoro na udhalilishaji ndani ya familia, nazo zinapaswa kuwa sehemu ya mjadala mpana kuhusu afya ya familia.
Ni muhimu pia kufuatilia takwimu hizo kwa miaka inayofuata ili kujua mwenendo wa changamoto za afya ya akili na uhusiano wake na mazingira ya kifamilia.Tatizo linapoanzia nyumbani, suluhisho lake pia linapaswa kuanzia nyumbani. Wazazi wanahitaji kujifunza namna ya kuwasiliana na watoto bila kuwavunjia heshima, huku jamii ikiendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya udhalilishaji wa kisaikolojia na umuhimu wa kutoa taarifa.
Taasisi zinazohusika nazo zinahitaji kuhakikisha kuwa mtu anayetoa taarifa anapata ulinzi, ushauri na huduma zinazohitajika bila kukatishwa tamaa na mchakato.
Kwa sababu mtoto anayekua katika mazingira ya hofu na dharau si tatizo linalohitaji kulaumiwa; ni mtoto anayehitaji msaada.
Na kama jamii inataka kujenga kizazi chenye kujiamini, afya njema ya akili na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo, basi namna tunavyowalea watoto leo haiwezi kutenganishwa na aina ya jamii tunayotarajia kuwa nayo kesho.
KUMSILIKIZA MTOTO NI HATUA YA KWANZA
Katika mapambano haya, mtoto anapaswa kuwa sehemu ya kwanza ya kusikilizwa. Si kwa sababu kila malalamiko yake yanapaswa kuchukuliwa bila uchunguzi, bali kwa sababu mtoto anayesema ana tatizo anahitaji mtu mzima wa kumsikiliza na kutafuta ukweli wa kinachoendelea.
Mzazi anapoona mtoto amebadilika kitabia, hatua ya kwanza haipaswi kuwa kumlaumu. Ni muhimu kuzungumza naye, kujua kinachomsumbua na kutafuta msaada pale inapohitajika.
Kwa upande wa jamii, ni muhimu kuacha kuwanyamazisha watoto na wanawake wanaojaribu kueleza wanachopitia. Kauli kama “vumilia kwa sababu ni familia yako” au “hayo ni mambo ya kawaida ya nyumbani” zinaweza kumfanya mhanga aendelee kuishi katika mazingira yanayomuumiza.
Familia inapaswa kulindwa, lakini ulinzi wa familia haupaswi kutumiwa kuficha vitendo vinavyomuumiza mtoto au mwanamke.
MWISHO
0 Comments