Imeandikwa na Salmin Juma - Zanzibar  

Zanzibar ni katika mataifa yaliyojaaliwa neema nyingi, ambazo kwa mkusanyiko wake zimezaa msemo mashuhuri wa “Zanzibar ni njema atakae naaje.”


Mbali na kujuulikana kwake kimataifa kwa zao la karafuu, visiwa hivi pia ni kituo cha ustaarabu wa kale ambao ni mchanganyiko wa tamaduni mbalimbali duniani, zikiwemo za Kiafrika, Kiarabu, Kihindi, Kiajemi na hata Kichina na Kizungu.

Makala haya yanalenga kuangalia athari za utamaduni mkongwe wa Zanzibar katika vyakula vya kujiburudisha, ambapo leo tutaiangalia zaidi tende na haluwa, ambavyo sio tu ni sehemu ya utambulisho wa Zanzibar, bali pia kielelezo cha ustaarabu wa siha.

Vitamu kama vilivyo, vyote viwili hivi vimejengewa utaratibu wa kunywewa kwa Kahawa ambayo ni chungu kwa ladha yake tena ikiwa imoto. Mizania hiyo ina maana kubwa ya kiafya na pia ya kifalsafa katika maisha ya watu wa visiwani, ambayo haiwezi kufahamika ila kwa wenyeji na wajuwao mambo.

Asili ya tende, haluwa na kahawa, ni nchi za Kiarabu na vyote viliingia Zanzibar katika karne ya 7,  na tangu hapo vimezoewa na kuchukuliwa kuwa sehemu muhimu ya maisha ya watu.

Hafla za harusi, matanga, maulid au mikusanyiko mingine huwa haionekani kufana kama tende, haluwa na kahawa haikuwa sehemu yao. Kote Zanzibar, yaani Pemba na Unguja, mijini na vijijini kuna “barza” – maskani maalum za watu wazima kukaa na kuzungumza nyakati za jioni, ambazo kiunganisho kikuu cha mazungumzo ni kahawa na tende ama haluwa. (ingawa wapo wanaopendelea kashata).

Hapana shaka, msisitizo wa tende kwenye dini ya Kiislamu inayofuatwa na takribani asilimia 99 ya Wazanzibari, nao una sehemu yake katika kuifanya tende kuwa na umuhimu mkubwa kwenye visiwa hivi.

Sheikh Khalfan Tiwany wa ChakeChake Pemba anasema kuwa, tende ni katika vyakula vilivyotajwa katika Qur-an Tukufu, ikielezwa, ni mojawapo ya matunda ya Peponi. Katika kisa maarufu cha kuzaliwa kwa Mtume Issa, Bi Maryam (mama yake Nabii Issa) aliamriwa kutikisa kigogo cha mtende na akala tende mbivu zilizoanguka.

Hili, anasema Sheikh Khalfan, linathibitisha umuhimu wa tende, maana, amri ya kuila imetoka kwa Mwenyezi Mungu mwenyewe. “Tende ina manufaa makubwa sana ya kiafya na ndio maana Mwenyezi Mungu akamuamuru Bibi Maryam ale mara baada ya kujifungua ili arejeshe damu yake na apone haraka.”

Dokta Ally Khamis wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja anathibitisha hilo la kwamba tende ni chakula cha afya.

“Ndani ya tende munapatikana Vitamin A ambazo zinaongezea nuru ya macho. Pia muna  madini ya Calcium yanayosaidia kujenga mifupa kuwa na uzito mzuri na wa kuhumili maradhi. Lakini pia kunapatikana Vitamin B6 na B12 ambavyo vinasaidia usagaji na ufyonzaji mzuri wa chakula kuingia katika mishipa ya damu na katika utaratibu unaotakikana.”

Kwa ushauri wa Dokta Ally, basi hata wale wagonjwa wenye michubuko tumboni, wanashauriwa kula angalau kokwa tatu za tende kila asubuhi, ambazo huenda moja kwa moja kusababisha utelezi tumboni na huondosha ule mkwaruzo. “Kokwa tatu za tende na gilasi moja ya maji kwa muda wa miezi sita zinaweza kabisa kuondoa vidonda vya tumbo.”

Hayo ni ya upande wa tende.

Tuje sasa kwenye Haluwa, ambayo hata kwa jina lake ina maana ya utamu kama ilivyo yenyewe. Kama ambavyo Waswahili wa Pwani walivyopokea misamiati ya lugha kutoka Kiarabu na lugha nyengine za dunia na kuitohoa ili ifanane na mazingira yao, nao upishi wa Haluwa umetoholewa na sasa umekuwa zaidi wa Kizanzibari kuliko kuwa wa Kiarabu. Ndio maana kuna halua zilizopewa majina kwa mujibu wa vitu vilivyotumika kuitengeneza kama vile lozi, ufuta na njugu, au ilipotengenezwa kama vile Wete, ChakeChake au kwa Bakhressa.

Kwa Zanzibar, haluwa bora kabisa inayosifika ni ya Wete ambayo ama hutayarishwa kavu ama kuwekwa lozi, ingawa kisiwani Unguja, haluwa inayopendelewa zaidi ni ya ufuta.

Kama ilivyo kwa Tende, na Haluwa nayo ina ada na kawaida zake katika jamii za Kizanzibari. Kwa mfano, adabu za kuila Haluwa ni tafauti na vyakukula vyengine.

Yussuf Hemed Hamed, ambaye ni mpishi mashuhuri wa halua mjini Wete, anasema: “Haluwa hailiwi kama wali kwa kuikamata na kuijaza kiganja tele, bali huliwa kwa ncha za vidole, tena kwa idadi maalum ya vidole, uzuri viwe viwili ama vitatu. Hapo ndipo utakapouona utamu wa haluwa.”

Haluwa nayo, kama ilivyo tende, huliwa ikisindikizwa na Kahawa chungu na imoto. Mizania hii ina maana kubwa, kama nilivyotangulia kusema hapo awali, kwenye maisha ya kila siku ya watu wa Zanzibar. Ni alama ya ukweli kuhusu maisha, kwamba ni mchanganyiko wa utamu na uchungu.

Ni ishara pia ya uwiano wa siha na mwilini, kwamba inapoingia sukari nyingi, basi inapaswa kuwahiwa kwa kitu kinachoiyeyusha haraka, ambacho ni kahawa. Kemikali ya Caffeine iliyomo kwenye kahawa inavunja kasi ya sukari mwilini na kuigeuza haraka kuwa maji. Ndio maana wanaokula haluwa, tende na kahawa huwa wanapata wepesi wa kupata haja ndogo (mkojo).

Lakini maana kubwa zaidi ya mchanganyiko wa haluwa na kahawa au kahawa na tende umo kwenye mjengeko wa kijamii. Mzee Subra wa Mkungumalofa Pemba kwenye baraza ya kahawa anasema “Kahawa si kama maji au kinywaji chengine. Kahawa haifanani na kinywaji chochote duniani. Huwezi kukaa peke yako eti ukawa unakunywa kahawa. Hapo itakuwa unajidanganya tu na utakuwa unakunywa maji yako machungu. Kunywa kahawa lazima ujumuike na wenzako. Stori ziwe zimepamba moto kama ilivyo kahawa yenyewe , huku unapuliza taratiibu na chubuo moja moja mdomoni. Hapo ndio utakua unakunywa kahawa.”

Ladha hii ya kijamii kwenye Kahawa, ndiyo iliyomo kwenye Tende na Haluwa pia. Mtu hawezi kujifungia nyumbani kwake na sahani ya Haluwa mbele yake, akasema anaifaidi Haluwa. Atakuwa tu anakula sukari yake. Lakini utamu wa Haluwa hasa ni shughulini, kwenye Harusi au Maulid, ambako sahani hupitishwa na waandaaji na kila mtu akachukua kitonge kidogo huku akizungumza na wenziwe.

Tende ni halikadhalika. Ukiacha mbali manufaa yake ya kiafya, utamu wake haupo kwenye kukusanya bakuli la Tende na kuanza kula kwa matonge kama wali, bali ni kwa kudondoa kokwa moja moja katika mikusanyiko ya kijamii, huku ukizungumza na kunywa kahawa.

Mambo haya ukiyapita bila ya kuyafikiria, utadhani hayana maana yoyote kwa Wazanzibari. Lakini ukiyafuatilia, utajua kwa nini Wazanzibari wanapenda tende, haluwa na kahawa, na si vyenginevyo zaidi ya ilivyoelezewa katika makala haya.