Ukiambiwa kuhusu ufugaji wa viumbe hai baharini wakiwamo samaki, moja kwa moja utahisi ni lazima shughuli hiyo ifanyike nje ya bahari, ziwani au mto
Mtu anapotembelea Zanzibar hususan katika kisiwa cha Uzi, huko kuna shughuli adimu ya ufugaji wa majongoo bahari. Ni moja ya mradi mikubwa inaotarajiwa kuwa chanzo cha mapato, ajira visiwani.
Pia, ni fursa muhimu ya uhifadhi wa viumbe bahari ambao katika siku za hivi karibuni wanahofiwa kutoweka.
Zanzibar sasa inakuwa ni ya pili katika Ukanda wa Afrika kuanzisha ufugaji viumbe bahari, wakiwamo majongoo bahari.
\Nchini Madagascar, kuna miradi ya namna hiyo iliyopiga hatua kubwa, ikiwamo kama kinachofanyika Zanzibar, suala la ufugaji majongoo bahari.
Utafiti wa awali wa Shirika la Misaada la Korea (KOICA) mwaka 2012, ulipendekeza kuendelezwa kwa sekta ya uvuvi, kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya vyakula vya mazao ya baharini.
Katika kuendana na mtazamo huo, inajenga dhana muhimu ya mfumo wa uchumi wa namna hiyo, unaoendana na kutetea baadhi ya viumbe hai bahari waliopo hatarini kutoweka.
Homoud Talib, ni Mkazi wa Kisiwa cha Uzi anayefuga majongoo bahari. Anasema, awali kabla ya kupatiwa stadi za ufugaji kutoka Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO), kupitia ufadhili wa KOICA, hawakuwa na stadi za kuyafuga majongoo bahari, ambayo tayari yalishaanza kuwa adimu.
''Siye wala hatujui kabisa. Unaweza kufuga majongoo bahari, basi tukawa tunayachukua baharini, lakini baadaye yakaanza kuwa adimu. Lakini, kwa sasa sababu tunayazalisha wenyewe na uzazi wake mkubwa sana ni matumaini yangu kuwa idadi itaongezeka sana,'' anasema Talib.
Katika orodha hiyo ya wadau, mwingine ni Harusi Said Ally, mama anayejitambhulisha kaingia katika kazi hiyo ya kufuga majongoo bahari kutokana na hamasa aliyoipata kutoka kwa mumewe.
Anaunga mkono kwamba kazi hiyo imembadilishia maisha kuelekea katika heri zaidi, ingawaje namna ya kuitumikia imekuwa changamoto kubwa kwake.
Harusi anakiri maisha yamembadilisha sana, lakini wanalazimika kuamka usiku kwenda kuwahudumia majongoo yao kabla ya maji ya bahari kujaa katika eneo wanalofugia viumbe hao.
MTAALAMU VIUMBE
Said Juma Shabaani ni mtaalamu wa viumbe hai bahari na ufugaji wa majongoo kutoka Shirika la Chakula Duniani FAO, anaelezea tabia za majongoo bahari ambazo zinarahisha ufugaji wake na udhibiti hivyo kusalia katika eneo lile lile walipohifadhiwa.
''Majongoo bahari kwanza wao hawatembei,bali wanazama kwenye mchanga. Hivyo, ukimuweka mahala utamkuta hapo hapo vinginevyo ingelikuwa vigumu udhibiti wake,'' anaeleza.
Pierre Philippe Blanc, ni Mshauri Mkuu wa Mradi kutoka FAO, aliyebobea katika uzalishaji wa majongoo, anasema kuwa mradi huo uliopo kisiwani Uzi ni moja ya miradi mkubwa na unaweza kuleta mageuzi makubwa na fursa ya ajira ndani ya Zanzibar, hadi Ukanda wa Afrika.
Kuhusu kituo cha uzalishaji vifaranga vya samaki na viumbe hai wakiwamo majongoo bahari, anasema wana uwezo wa kuzalisha hadi ziada ya majongoo wadogo anaowaita kitaalamu kwa jina ‘seeds’ na kuwasambaza katika soko la kisiwani Madascar na maeneo mengine ya Ukanda wa Bahari ya Hindi, kunakohitajika.
Mradi huo unaoendeshwa kwa ubia wa wafadhili KOICA na FAO, hadi sasa una matarajio makubwa kwamba, huenda ukaleta mageuzi makubwa katika uchumi wa Zanzibar, kutokana na kuwapo soko kubwa la majongoo katika nchi za Bara Asia na Ulaya.
Credit by www.ippmedia.com
0 Comments