Kunguru ni ndege ambao kisayansi wamepangwa katika kudi la Passerine, wanaopatikana kwa wingi katika bara la Ulaya na Mashariki mwa bara la Asia .

Hata hivyo kama ilivyo kwa aina nyingine za ndege, kunguru nao wamegawanyika katika makundi mengi.

Leo tutaangalia zaidi maisha ya kunguru weusi, ambao hapa Tanzania wanapatikana zaidi katika maeneo ya mwambao wa Bahari ya Hindi.

Kwa mara ya kwanza wataalamu walianza kufanya utafiti wa kunguru hawa katika karne ya 18 na kubaini kuwa na ndege hawa pia wamegawanyika katika familia ndogondogo za aina tofauti.

Licha ya kuwepo kwa aina nyingi za ndege hawa, kunguru weusi kwa lugha ya kiingereza wanaitwa ‘Carrion crow’ ingawa Tanzania wanajulikana zaidi kwa jina la Kunguru wa Zanzibar.

Kunguru hawa kwa kawaida wana rangi nyeusi na baadhi yao wana rangi ya kijani au kijivu kifuani na shingoni, pia wakiwa na miguu mieusi.

Kimaumbile kunguru huwa na urefu wa kati ya sentimeta 48 na 52 (Inchi 18 hadi 52), Hata hivyo wanatofautiana kidogo ukubwa kulingana na mazingira wanayoishi, ambapo wanaopatikana katika bara la Ulaya, baadhi yao wana ukubwa wa kati ya sentimeta 50 hadi 56 (Inchi 19 hadi 22).

Kunguru weusi kwa kawaida ni ndege wenye kelele, wanaopendelea kukaa juu ya miti mirefu, lakini wasiokuwa na uwezo wa kuruka umbali mrefu bila kupumzika.

Pamoja na ndege hawa kula kila aina ya chakula wanachokiona, kunguru weusi pia wanapendelea kula wadudu jamii ya insekta, minyoo, punje ngumu za mazao (kama vile mahindi, karanga, njugumawe, na mengineyo), wanyama wadogowadogo jamii ya mamalia (kama vile Panya, panya buku na mengineyo) na uchafu utokanao na mabaki ya vyakula mbalimbali.

Pia inadaiwa kuwa kunguru wanaweza kuiba hata mayai na kuyavunja kabla ya kuyala, hivyo kuonekana kama adui kwa jamii nyingi za ndege wenzake waishio porini na hata wale wanaofugwa.

Kwa asili yao, kunguru weusi ni wawindaji na ndio sababu hupendelea kutembelea maeneo ambayo wanaishi binadamu kwa lengo la kupata mabaki ya vyakula na uchafu mwingine wa majumbani kwa ajili ya chakula.

Kunguru weusi pia ni wakorofi na wanao uwezo wa kuwanyang’anya mawindo baadhi ya ndege wengine na hata wanyama wadogo wadogo jamii ya paka na kula wao.

Pamoja na ukorofi wao, kunguru wamekuwa msaada kwa binadamu kutokana na kutumika kwenye baadhi ya miji na majijiji kupunguza uchafu.

Mathalani katika nchi ya Japani, kunguru weusi walipelekwa katika majiji ya nchi hiyo kwa ajili ya kushambulia uchafu na viumbe wasiohitajika ambao ilikuwa vigumu kupambana nao.

Hata hivyo kutokana na tabia ya kunguru ya kula na kukwapua kila kitu wanachokiona, kila mahali wanakokuwa wengi huonekana kuwa kero kwa binadamu na hivyo kuwepo kwa mikakati ya kuwapunguza au kuwaangamiza kabisa.

Njia mojawapo ambayo imekuwa ikitumika kuwapunguza au kuwaangamiza ndege hawa huwa ni kudondosha vipande vya mizoga au chakula chenye sumu barabarani ambapo kunguru huwa ni wepesi kuishukia mizoga hiyo na kuila kabla ya kufa.

Hata hivyo wataalamu wanadai kuwa, njia hiyo ya kuwaangamiza kuguru haifai kwa kuwa inaweza kuwadhuru hata viumbe wengine wakiwemo watoto wa binadamu, ikiwa kunguru watachelewa kuifikia mizoga au vyakula hivyo vyenye sumu na hivyo kuliwa na viumbe ambao hawakukusudiwa.

Kama ilivyo kwa ndege wengine, kunguru nao wanahitaji kuzaliana ili kuendeleza kizazi chao. Kabla ya kuzaliana, ndege hawa huandaa makazi yao kwa kujenga viota ambavyo huvitumia kwa malazi na kutagia mayai.

Kwa kawaida kunguru weusi hujenga viota vyao juu ya miti mirefu, juu ya miamba ya majabari au miamba mirefu iliyo ufukweni mwa bahari, majumba au magofu ya zamani na hata minara mikubwa na nguzo za umeme pia inaweza kutumiwa na ndege hawa kujenga makazi yao.


Kwa kawaida viota vya kunguru hujengwa juu au jirani na ardhi na huwa na ukubwa wa kutosha kuingia kunguru wote wawili (dume na jike ) pamoja na makinda yatakayoanguliwa.

Kunguru jike hutaga mayai yenye rangi ya kijani au bluu ambayo huyaatamia kwa muda wa siku kati ya 17 na 19 kabla ya kuanguliwa.

credit by ippmedia.