Na Salmin Juma, Unguja

Ni takribani miezi 12  sasa wadau wa habari hapa Zanzibar wamekuwa wakikutana katika vikao mbalimbali kujadili na kutoa maoni yao katika kurekebisha na kuboresha sheria mbalimbali zinazoigusa sekta ya habari nchini,

Kuna sheria nyingi ambazo kwa namna moja ama nyingine, zinaathiri uhuru wa habari na haki ya kujieleza kwa mfano sheria ya Usalama wa Taifa, Sheria ya magazeti ya Zanzibar, Sheria ya Takwimu, sheria ya tume ya uchaguzi na nyenginezo.

SHERIA YA USAJILI WA WAKALA WA HABARI, MAGAZETI NA VITABU NAMBA 5 YA MWAKA 1988 KAMA ILIVYOREKEBISHWA NA SHERIA NAMBA 8 YA MWAKA 1997

Sheria hii imekua na mapungufu mengi, yanayokwamisha haki ya uhuru wa vyombo vya habari na uandishi wa habari Zanzibar.

Kwa mfano kifungu cha 27(1),(2) na (4) kinachoelezea uwezo wa kukamata magazeti na kupekua majengo.

Kifungu kidogo (1) ofisa yeyote wa Polisi anaweza kukamata gazeti lolote, popote litakapoonekana, lililochapwa au kuchapishwa, au ambalo kwa maoni yake atalituhumu kwamba limechapwa au kuchapishwa, kinyume na sheria hii.

Kifungu kidogo(2) hakimu yoyote anaweza kwa hati, kumruhusu ofisa yoyote wa polisi wa cheo cha mkaguzi au cheo cha juu yake, akiwa na msaada au bila ya msaada, kuingia na kuepuka sehemu yoyote ambayo kwa maoni yake anadhani kwamba limo gazeti lililochapwa kinyume na sheria hii.

Aidha kifungu kidogo (4) gazeti lolote lililokamatwa chini ya kifungu litapelekwa haraka iwezekanavyo kwa hakimu, ambaye anaweza, ikiwa atajitosheleza kwamba gazeti lilichapwa au kuchapishwa kinyume na sheria hii.

Mwandishi wa habari kutoka Mwanahalisi mtandaoni, Jabir Idrissa anasema kumpa mamlaka ofisa polisi au chombo chengine cha sheria ili kwenda kufanya upekuzi ni kuwadhalilisha waandishi na tasnia ya habari kwa ujumla na hasa ukizingatia kuwa tasnia hiyo inaenda kuwa mhimili wa nne usio rasmi.

“Hayo ni mamlaka makubwa sana kwa kupewa ofisa wa polisi, kwani ofisa anaweza kutumia mamlaka hayo kukamata gazeti muda wowote tu atakaojisikia na wala sio kwa sababu kuna kosa”. Alisema Habiba Zarali ambae ni Mwandishi wa habari kutoka Gazeti la Zanzibar Leo Pemba.

Kuhusiana na Uteuzi wa Msajili Kifungu cha 3 – Waziri, kwa taarifa katika Gazeti la Serikali, atamteua Msajili wa Vitabu na Magazeti kutekeleza majukumu na kutekeleza mamlaka aliyopewa Msajili na Sheria hii na kanuni zozote zitakazotungwa chini yake, na anaweza kuteua Naibu Msajili ambaye atapatikana kwa maelekezo ya Msajili. Lakini hapo hapo bado sheria ipo kimya kuhusiana na sifa na uzoefu wa msajili mteule.

Mwandishi veteran Salim Said alisema kwa maoni yake  msajili asihusishwe kabisa katika uteuzi wa naibu msajili wake na kuwa nafasi ya Msajili itangazwe na achaguliwe kwa mujibu wa sifa na uzoefu alonao. Mfano msajili awe mwanasheria au mtu mwenye taaluma ya habari na mawasiliano ya umma na sifa hizo ziainishwe ndani ya sheria.

Nae mkufunzi wa masuala ya habari Zanzibar bi  Imane Duwe, anasema maneno kama ‘uwezo wa Mkurugenzi, Waziri akiona inafaa, akihisi, kwa maoni yake’ kwenye sheria mpya ya habari yasitumike kwani yanampa uwezo mkubwa waziri wa kukubali au kukataa kibali, na hiyo itapelekea kufika wakati Zanzibar kukosa waandishi wa habari kutokana na kukosa vibali.

Mhariri mtendaji wa shirika la Magazeti ya serikali Zanzibar, Ali Haji Mwadini anasema kuwa Kama bado kuna sheria inaelekeza kuwa waziri anaweza, mkurugenzi akiona, kwa maoni yake au akihisi hiyo sio demokrasia, na inaathiri uwepo wa waandishi huru wa habari na hivyo kuzorotesha ukuaji wa maendeleo ya taifa.

Kimsingi kuna mapungufu mengi katika sheria zinazoihusu sekta ya habari ambayo  yanahitaji kufanyiwa kazi kwa weledi kabisa ili kuona ni kwa namna gani uhuru wa habari unapatikana  ili kuwapa uhuru waandishi kufanya kazi zao kwa weledi na hatimae kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu.