Waandishi wa Habari Zanzibar wameiomba Serikali kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa Sheria mpya na rafiki ya habari ambayo itawawezesha waandishi na wamiliki wa vyombo vya habari kuwa huru na kujiamini kutoa taarifa mbalimbali kwa jamii.
Wameeleza hayo katika mkutano wa kupeana mrejesho baina ya waandishi na Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) juu ya kuendeleza utetezi na uchechemuzi kwenye masuala ya habari Zanzibar.
Wanasema iwapo Sheria zilizopo zitafanyiwa marekebisho ya haraka kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, zitaweza kuondoa hofu ya kukusanya na kutoa taarifa mbali mbali na kuiwezesha jamii kupata habari kwa wakati.
"Kwa kipindi kirefu tumeendelea kufanya uchechemuzi lakini marekebisho ya sheria mbili kuu yaani Sheria ya Wakala wa Habari Magazeti na Vitabu (1988) na Sheria ya Tume ya Utangazaji Zanzibar (1997) ambazo waathirika wakubwa ni Waandishi, vyombo vya habari na jamii iliyotuzunguka”, wanaeleza waandishi hao.
Wameongeza kuwa, Licha ya juhudi za wadau mbali mbali wa sekta ya habari ikiwemo ZAMECO na waandishi wahabari kuendelea kufanya uchechemuzi kwa kutayarisha Makala na vipindi mbalimbali vinavyoonesha mapungufu yaliyomo katika sheria za habari lakini bado matumaini ya kupatikana Sheria mpya yanaendelea kusuasua kila uchao.
Kwa upande wao baadhi ya wajumbe wa ZAMECO walioshiriki katika kikao hicho wamewahimiza waandishi kuendelea kupaza sauti zao kwa kuandika kazi ambazo zitaleta athari kwa jamii sambamba na kupatikana kwa sheria mpya ya habari isiyokua na vifungu vinavyokandamiza uhuru wa habari.
0 Comments