Waziri wa Kilimo Umwagiliaji na Mifugo Zanzibar Mhe, Shamata Shaame Khamis amesema, Wakulima, wizara ya Biashara na Wizara ya Kilimo wanawajibu wa kushirikiana na kuhakikisha wanalilinda na kulithamini zao la karafuu na kuendelea na upandaji miche hiyo hasa katika kipindi hiki cha mvua za masika zinazoendelea.
Akizungumza leo katika Uzinduzi wa Ugawaji wa miche ya mikarafuu Tangaani Mkoa wa Kusini Pemba katika hafla iliyoandaliwa na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) kwa mashirikiano na wizara hiyo Amesema kuwa wananchi wana dhima ya kuendeleza na kulinda karafuu ya Zanzibar kwani ndio uti wa mgongo wa uchumi wa nchi, hivyo Serikali kupitia wizara ya kilimo na Shirika la Biashara litaendelea kununua miche hiyo na kuitoa kwa wananchi bure ili kuweza kuendeleza zao hilo na kuleta tija kwa wananchi.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC). Nd, Soud Said Ali amesema kuwa Juhudi kubwa inayochukuliwa na Shirika la biashara kwa kushirikiana na wizara ya kilimo katika kuhakikisha linaendelea kuzalisha miche ya mikarafuu na kuitoa kwa wananchi ili kuongeza kasi ya uzalishaji wazao hilo ni chachu ya maendeleo na ukuwaji wa zao la karafuu nchini.
Aidha amesema kwasasa Shirika kwa kushirikana na wizara ya Kilimo limeandaa utaratibu maalum wa kufatilia miche yote inayotolewa ili kujua maendeleo ya ukuwaji ya miche hiyo kwa ustawi wa taifa.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu wizara ya Kilimo Umwagiliaji na Mifugo Nd, Ali Khamis Juma. Ameeleza kuwa mpango wa utoawaji wa miche ya mikarafuu ukiendelezwa na wananchi utaleta tija kwa taifa na kuongeza uzalishaji wa zao la karafuu nchini.
Nao wananchi waliokabidhiwa ,miche hiyo wameushukuru uongozi wa Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC). kwa mikakati wanayoichukua katika uzalishaji na utowaji wa miche ya Mikrafuu kwa wananchi bila ya malipo ili kendelea kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
0 Comments