Habari nzito zilizotokea katika mlima wa Lewotobi Laki Laki, Indonesia

Indonesia, Juni 18, 2025 — Mamlaka nchini Indonesia zimethibitisha kutokea kwa mlipuko wa volkano kutoka Mlima Lewotobi Laki-laki ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo, mnamo saa 11:35 jioni kwa saa za eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wakala wa Jiolojia wa Indonesia, mlipuko huo ulisababisha moshi mzito wa majivu ya kijivu kupaa hadi urefu wa takribani futi 32,000 angani. Tukio hilo limetajwa kuwa miongoni mwa milipuko mikubwa ya hivi karibuni katika eneo hilo la volkeno.

Katika saa chache kabla ya mlipuko, taasisi hiyo ilirekodi ongezeko lisilo la kawaida la mitetemeko ya ardhini ya asili ya volkano, ambapo jumla ya mitetemeko 50 ilishuhudiwa ndani ya saa mbili pekee, ikilinganishwa na wastani wa mitetemeko 8 kwa siku moja.

Hadi kufikia sasa, hakuna taarifa rasmi za vifo, majeruhi, au uharibifu mkubwa wa mali zilizotolewa. Hata hivyo, kijiji kimoja kilicho karibu na mlima huo tayari kimehamishwa kwa ajili ya tahadhari, huku mamlaka zikiendelea kufuatilia hali ya eneo hilo kwa karibu.

Wataalamu wa jiolojia wameshauri wakazi wa maeneo jirani kuchukua tahadhari na kufuata maelekezo ya usalama yatakayotolewa na serikali, endapo hali ya mlima huo itaendelea kuwa hatarishi.

Post a Comment

0 Comments