WANDISHI wa Habari nchini wametakiwa kuwa walinzi wazuri kwa wanawake watakaogombea nafasi mbali mbali za uongozi ili kuripoti na kukemea ukatili dhidi yao katika kipindi cha Uchaguzi.
Ameyasema hayo, Mkurugenzi wa chama cha wandishi wa Habari wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA ZNZ ) Dk Mzuri Issa katika mafunzo ya siku moja, yaliyofanyika katika Ofisi ya chama hicho huko Tunguu,na kuwashirikisha wandishi wa vyombo mbali mbali vya Habari.
Dk Mzuri, amesema kuelekea kipindi cha uchaguzi wandishi wa Habari wana jukumu kubwa la kufanya kazi yao ya ulinzi ili kuwalinda wagombea wanawake watakaogombea nafasi mbali mbali za uongozi dhidi ya vurugu na udhalilishaji unaotokea katika kipindi hicho.
“ Tuna sheria nyingi ambazo zinamtaka mwanamke ashiriki katika kugombea nafasi za uongozi hasa sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2023 ambayo imeongezwa kifungu cha 10 C ambacho kinavitaka vyama vya siasa kuwa na sera ya jinsia na madawati katika vyama vyao” amesema Dk Mzuri.
Aidha amewataka wandishi wa Habari kuendelea kuandika Habari za wanawake waliopata mafanikio katika nafasi za uongozi ili iwe mfano mzuri kwa wanawake wanaotia nia ya kugombea nafasi mbali mbali za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
“ Tunao wanawake wengi waliofanya vizuri katika nafasi za uongozi na wakaleta maendeleo na mabadiliko ya kisiasa lakini pia katika mashirika na makampuni mbali mbali ni vizuri tukawaandikia Makala ili jamii iwajuwe” amesema.
0 Comments