MARIAM MWINYI:MALEZI NA MAKUZI BORA YA AWALI KWA MTOTO NI MSINGI IMARA

.
Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), Mhe. Mama Mariam Mwinyi, amesema ana imani kuwa malezi na makuzi bora ya awali ya mtoto ni msingi imara wa kujenga taifa lenye raia wenye afya, elimu, nidhamu na maendeleo endelevu.
Mama Mariam Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 13 Agosti 2025, alipozindua Kampeni ya Malezi na Makuzi ya Awali ya Mtoto wa Zanzibar (ECD) katika viwanja vya Kisonge, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha, Mama Mariam Mwinyi ameeleza kuwa ZMBF imekuwa mstari wa mbele kusaidia maendeleo ya makuzi ya mtoto, hususan katika programu za lishe pamoja na huduma za afya ya mama na mtoto. Amesema kupitia jitihada hizo, imeweza kuwafikia wanufaika zaidi ya 50,000 katika Shehia 67 na vijiji 644 vya Unguja na Pemba.
Mama Mariam Mwinyi amesema kupitia kampeni ya Afya Bora Maisha Bora, kambi za matibabu bure zilizoendeshwa na ZMBF zimewafikia wananchi 21,000. Ameeleza kuwa huduma hizo zimejumuisha elimu ya lishe, elimu ya malezi na makuzi, matibabu kwa watoto wenye utapiamlo, utoaji wa chanjo, pamoja na huduma za afya ya mama na mtoto.
Vilevile, Mama Mariam Mwinyi amefahamisha kuwa kampeni aliyoizindua haipaswi kuwa tukio la siku moja, bali iwe ni harakati ya muda mrefu na endelevu ili kuhakikisha kila mtoto wa Zanzibar, kuanzia hatua ya mama katika ujauzito hadi umri wa miaka minane, anapata haki zake za msingi ikiwemo afya bora, lishe sahihi, ulinzi, malezi na mazingira salama ya ukuaji ili kufikia utimilifu wake.
Kwa upande mwingine, Mama Mariam Mwinyi ametoa wito maalum kwa sekta binafsi na mashirika ya maendeleo kuendeleza ushirikiano na Serikali katika uwekezaji wa malezi na makuzi ya awali ya mtoto.

Post a Comment

0 Comments