KAMATI ya Wataalamu wa Masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) imeiomba Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuhakikisha usalama wa Waandishi wa Habari, Wanawake wagombea, na Wasimamizi wa Uchaguzi (Mawakala) katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi mkuu wa Zanzibar ambao utafanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu.
Kamati hiyo imesema inatambua kuwa mazingira salama kwenye masuala muhimu yenye maslahi mapana na mustakabali wa nchi hususan suala la uchaguzi, ni sharti la msingi ili kuhakikisha kila mdau anatekeleza majukumu yake kwa uhuru na bila ya hofu kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 15(1) ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984:
"(Kila mtu anastahiki kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na ya nyumbani kwake, na pia heshima, na hifadhi ya maskani yake na mmawasiliano yake)."
Aidha Kamati imesisitiza kuzingatiwa hatua mahsusi kwa mujibu wa sheria na kanuni za kulinda haki na usalama wa makundi haya wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi huku ikisisitiza kuwa waandishi na jamii kwa ujumla, wanahaki ya kupewa fursa ya kupata taarifa bila ya kuingiliwa kwani kila mmoja ana haki hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 18 ya Katiba ya Zanzibar 1984 sambamba na ibara ya 19 ya Tamko la Kimataifa la Haki za Binaadamu (UDHR-1948) inayoeleza “Kila mtu ana haki ya kuwa na maoni na mawazo yake bila ya kuingiliwa
Aidha ZAMECO, imesisitiza umuhimu wa Waandishi wa Habari kupewa nafasi sawa zisizo na ubaguzi katika kupata taarifa sahihi zinazohusu uchaguzi pamoja na kupatiwa vitambulisho maalum vinavyotolewa na Tume ya Uchaguzi na kuepuka kutoa fursa zaidi kwa vyombo vya Serikali na kuvikwepa vyombo visivyokuwa vya Serikali hali itakayopelekea kufuatilia na kuripoti matukio ya uchaguzi kwa weledi usawa bila ya kuathiriwa na vikwazo visivyo vya lazima.
Hata hivyo, kamati imetoa mapendekezo kwa Tume ya Uchaguzi kutoa mafunzo maalum kwa waandishi wa wabari kuhusu uandishi wa taarifa za uchaguzi kwa kuzingatia usawa wa kijinsia weledi na maadili ya taaluma kwani mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha uelewa wa waandishi katika kuripoti kwa kuzingatia wagombea wa jinsia zote.
Katika hatua nyengine, ZAMECO inapongeza ahadi iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ya kutoa na kuchapisha takwimu za jinsia za
washiriki wa uchaguzi, iikiwemo idadi ya wanawake na wanaume watakaogombea nafasi mbalimbali ikiwemo Irais, Uwakilishi na udiwani pamoja na wapigakura na washiriki wa mchakato mzima wa uchaguzi ambapo takwimu hizi zitakuwa nyenzo muhimu katika kufuatilia uwiano wa kijinsia na kkusaidia kufikia lengo la usawa wa asilimia 50/50 nchini.
ZAMECO inahitimisha kuwa, uchaguzi huru wa haki na jumuishi unahitaji mazingira salama taarifa sahihi, na upatikanaji sawa wa fursa kwa wanawake na wanaume ili kuimarisha demokrasia na mshikamano nchini.
0 Comments