NA - KHAULAT SULEIMAN RASHID
Bado Wanawake wanaojaribu kujikomboa kuwania nafasi za uongozi ,maeneo mbali mbali Unguja na Pemba ngazi ya siasa husuan ni uchaguzi ndoto zao zinaishia kufifia kutokana na changamoto ya fedha hususan ni vyama ambavyo havina ushindani mkali.
Ambapo moja kati ya changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa fedha zinazowawezesha kufanya kampeni kwa usawa na wagombea wanaume ambazo kikawaida hutambulisha mtu na dhamira yake kwa jamii.
Mazingira haya ya kukosa fedha yameathiri kwa kiasi kikubwa uwiano wa kijinsia katika siasa, licha ya Zanzibar kuwa na sera na sheria zinazolenga kuimarisha ushiriki wa wanawake katika kuufikia usawa wa kijinsia .
Sera ya Maendeleo ya Wanawake Zanzibar (2001) na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 (Marekebisho ya 2010), inayosisitiza haki sawa za kisiasa kwa wanawake na wanaume.
Changamoto ya Fedha katika Kampeni za Siasa
Kampeni za uchaguzi zinahitaji gharama kubwa kuanzia uchapishaji wa mabango, usafiri, mikutano ya hadhara, malazi, mawakala, hadi uhamasishaji wa wapiga kura.
Hata hivyo, tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa wanawake wengi wanaingia kwenye siasa wakiwa na uwezo mdogo kifedha.
Akizungumza na Makala haya mgombea wa uwakilishi jimbo la Mtambile kupitia chama cha Ada Tadea anasema chanagamoto ya kukosa ruzuku imemfanya kutofikia malengo ya kutangaza sera zake kwa weledi.
Kama ningepata feha maalum za kutengwa naamini ningefika mbali katika kupiga kampeni zangu,anasema
Kwa mujibu wa Ripoti ya TAMWA-Zanzibar (2021), zaidi ya asilimia 70 ya wagombea wanawake walikiri kuwa ukosefu wa fedha ulikuwa sababu kuu ya kushindwa kufanya kampeni kwa ufanisi.
Wengi wao walitegemea michango midogo ya kifamilia, wakati wagombea wanaume walipata misaada mikubwa ya kifedha kutoka kwa wafanyabiashara, marafiki au ndani ya vyama vyao.
Ripoti hiyo inaeleza kwamba baadhi ya wagombea wanawake walishindwa kufika vijiji vyote katika majimbo yao, wengine walishindwa kulipa mawakala, na baadhi walitumia njia za uhamasishaji za jadi kama mikutano midogo au nyumba kwa nyumba, ambazo hazikuwa na athari kubwa kwa wapiga kura.
Mgombea wa nafasi ya uwakilishi kupitia chama cha CUF jimbo la Mtambile Asha Siasa Ame anasema kuwa mapambano yake ya kutafuta kura yalikuwa ni makubwa lakini ukosefu wa fedha ulipunguza nguvu ya kupiga kampeni jimboni.
Uhusiano Kati ya Ukosefu wa Ruzuku na Usawa wa Kijinsia
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC, 2020), vyama vingi vya siasa havina utaratibu maalumu wa kutoa ruzuku au kugawa rasilimali kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.
Hii inamaanisha kuwa wanawake hawapati fursa sawa za kifedha ndani ya vyama vyao vya kisiasa.
Zaidi ya hapo, tafiti za Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA) zinaonyesha kuwa baadhi ya wagombea wanawake huogopa hata kuomba msaada wa kifedha.
Hofu yao kubwa ni kuonekana wanategemea huruma, jambo linaloonesha athari za kijamii na kitamaduni zinazozuia ushiriki wao.
Kwa hivyo, ukosefu wa fedha hauathiri tu kampeni, bali unadumisha mfumo wa kisiasa usio na usawa, unaowapa wanaume nafasi ya kuendelea kutawala vyombo vya maamuzi.
"Sasa kama hawajapata ni bahati mbaya na ni mapungufu makubwa Kwa vyama vya Siasa kwani tuliwaambia mapema Kwa vile vyama ambavyo vinapata ruzuku waweke fungu maalum na Kwa vile ambavyo havipati waanze kutafuta fedha mapema ili wanawake wasipate shida"alisema.
Anasema Moja katika jambo muhimu ni kuwatambuwa wale wanawake wanaoweza kuwa viongozi na kuwapa nafasi na mashirikiano ya Hali na mali ili kuweza kutekeleza.
Bi mzuri anasema wanawake ni kundi maalum ambalo Kwa miaka mingi limerejeshwa nyuma, hivyo lazima vyama viwe na sera ya kijinsia na kutekelezwa Kwa vitendo.
Haya ni mannen ya bimzuri
Kaimu mratib Tamwa Zanzibar kwa upande wa Pemba Amina Ahmed Mohamed anasema juhudi ambazo zinachukuliwa na chama hicho ni kuhakikisha wanawake hao wanapaza sauti zao na kuzisemea chanagamoto zinazowakumba katika harakati mbalimbali ikiwemo za uchaguzi.
Athari za Kijamii na Kisiasa
Ukosefu wa ruzuku kwa wagombea wanawake una madhara ya muda mrefu kwa Zanzibar, hasa katika maeneo matatu muhimu ikiwemo kupungua kwa uwakilishi wanawake katika vyombo vya maamuzi.
Kwa mujibu wa takwimu za ZEC mwaka 2020, idadi ya wanawake walioingia Baraza la Wawakilishi haikuzidi asilimia 15, licha ya jitihada za serikali kupitia viti maalum.
Hii ni dalili kwamba mfumo wa kisiasa bado haujawa rafiki kwa wanawake wagombea wa moja kwa moja.
Nyengine ni kudidimiza sauti za wanawake katika sera za kijamii, wanawake ni watendaji wakuu katika nyanja kama elimu, afya, na ustawi wa jamii, lakini kushindwa kwao kupata nafasi za uongozi kunafanya sera nyingi zisitilie mkazo mahitaji yao.
Kukwamisha malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), lengo Namba 5 la SDGs linahimiza usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake katika uamuzi wa kisiasa. Bila ruzuku na usaidizi wa kifedha, Zanzibar inaweza kushindwa kufikia kipengele hiki muhimu cha kimataifa.
Mitazamo ya Wadau na Wachambuzi
Mwenyekiti wa TAMWA-Zanzibar, Asha Abdi anasema wagombea wanawake pamoja na kuhitaji maneno ya kutia moyo, bali wanahitaji msaada halisi wa kifedha kwani bila fedha, hata sera nzuri hazitawafikia wapiga kura.
Anasema vyama vya siasa visijiweke nyuma badala yake vijiwezeshe ili kuhakikisha vinawasaidia wanawake hasa ukizingatia ni jukumu lao kuwalea ,kuwasapoti katika harakati za kugombea.
Kwa upande mwingine, UN Women Tanzania kupitia mpango wake wa Women in Political Participation (WiPP), imependekeza serikali ya Zanzibar na vyama vya siasa kuweka utaratibu wa mfuko wa usaidizi wa kifedha kwa wagombea wanawake, kama sehemu ya jitihada za kuleta usawa wa kisiasa.
Mapendekezo ya Kitaalamu
Ili kuimarisha nafasi ya wanawake katika siasa za Zanzibar, wachambuzi wa kisiasa na taasisi za kijinsia wanapendekeza hatua ikiwemo kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa ruzuku kwa wagombea wanawake.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi na wadau kama UN Women, iweke utaratibu wa kisheria wa kutoa ruzuku ndogo kwa wagombea wanawake wanaojitegemea au kupitia vyama vya siasa.
Vyama vya siasa kutunga kanuni za usawa wa kijinsia katika mgao wa fedha, kila chama kipokee ruzuku ya serikali kwa masharti kwamba sehemu yake inatengwa kwa wagombea wanawake na vijana.
Kutoa mafunzo ya usimamizi wa fedha na ujasiriamali wa kisiasa, wanawake wanaojitosa katika siasa wapewe elimu ya kupanga bajeti za kampeni, kuvutia wafadhili, na kutumia mbinu bunifu za mawasiliano.
Kuhamasisha jamii kuondoa mitazamo hasi, jamii ifundishwe kuona wanawake kama viongozi kamili, si wapambanaji wa muda. Vyombo vya habari vizingatie uwiano wa kijinsia katika taarifa za kampeni na mahojiano ya kisiasa.
Katibu Mkuu Taifa wa chama cha UDP Juma Khamis Faki anasema kupitia chama hicho wanajitahidi kuwashirikisha wanawake katika shughuli mbalimbali isipokuwa suala la ruzuku anasema si la chama badala yake ni la serikali amabayo iko madarani kupitia tume ya uchaguzi.
ni vizuri tunapoingia katika masuala ya uchaguzi serikali ilioko madarakani itowe haki sawa kwa wote katika kutowa ruzuku ili kuwe na usawa wa kunadi sera zakeanasema.
Hitimisho
Ukosefu wa ruzuku umekuwa ni kikwazo kikubwa kinachowanyima wanawake Zanzibar fursa sawa ya kushiriki katika siasa.
Changamoto hii imekuwa ikirudisha nyuma juhudi za muda mrefu za kuhakikisha usawa wa kijinsia katika vyombo vya uamuzi.
Ili Zanzibar ifikie demokrasia jumuishi, vyama vya siasa, serikali na taasisi za kiraia lazima viweke mifumo endelevu ya kifedha na kisheria ya kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika kampeni.
Bila kufanya hivyo, siasa zitabaki kuwa uwanja wa wachache wenye uwezo wa kifedha, huku wanawake wengi wakiendelea kubaki pembezoni.
0 Comments