NA-FATMA SULEIMAN -PEMBA
UTANGULIZI
Mabadiliko ya tabia nchi sasa hayapo kwenye vitabu tuu bali ni ukweli unaoguswa kila asubuhi na mwanamke wa visiwa vya Unguja na Pemba (Zanzibar) pale anapotembea kutafuta maji, na mtoto anapokosa kwenda skuli kwa sababu ya mafuriko.
Joto kali, ukame mrefu, mvua zisizotabirika na kupanda kwa usawa wa bahari vimekuwa vikitikisa maisha ya Unguja na Pemba. Na anayebeba mzigo mkubwa zaidi ni mwanamke na mtoto – nguzo ya familia na taifa.
Wataalamu wanasema ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa, mzigo huu utazidi kuwa mzito kwa vizazi vijavyo.
WANAWAKE NA MZIGO WA MAJI
Kwa desturi nyingi za Zanzibar, mwanamke ndiye “mtoaji wa maji”. Ukame na kupungua kwa vyanzo vya maji safi kumefanya kazi hii kuwa ngumu zaidi.
Asha Khamis, mkazi wa kijiji cha Kidemeni, Wilaya ya Chake Chake Pemba aliyezungumza na Zenjiupdate Blog alisema:
“Mambo mengi sana, lakini kuja kuangalia latizo la maji ni zitoo wanawake wana changamoto kubwa ya kutafuta maji nyumbani” alisema.
Kwa mujibu wa UNICEF 2023, wanawake na wasichana duniani wanatumia zaidi ya masaa milioni 200 kwa siku kukusanya maji. Masaa hayo yangeweza kutumika maskulini au kufanya biashara.
AFYA YA MAMA NA MTOTO YATIKISWA
Wataalamu wa afya wanasisitiza kuwa mabadiliko ya tabia nchi sasa ni "mgonjwa mpya" hospitalini Unguja na Pemba.
Mtaalamu wa afya kutoka Wizara ya Afya, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Afya na Mazingira, Khalfan Shaha Bakar Mmoja, alisema:
“Ongezeko la joto pamoja na mafuriko limekuwa likichangia kuenea kwa magonjwa ya mripuko kama kipindupindu, kuhara na malaria. Wanawake wajawazito na watoto chini ya miaka 5 ndio wanaopata athari kubwa zaidi. Joto kali linasababisha upungufu wa damu kwa mama mjamzito, mimba kuharibika na vifo vya watoto wachanga. Maji machafu baada ya mafuriko ndio chanzo kikuu cha magonjwa haya vijijini” alisema.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO, mabadiliko ya tabia nchi yanatarajiwa kusababisha vifo vya ziada 250,000 kwa mwaka kati ya 2030-2050 duniani, na watoto na wanawake wajawazito wataathirika zaidi.
WASICHANA NA WATOTO WAKIKOSA ELIMU
Mabadiliko ya tabia nchi pia yanavuruga ratiba za wanafunzi mashuleni. Mafuriko na mvua kubwa zimekuwa zikizuia wanafunzi kufika skuli kwa wakati.
Mwalimu kutoka Skuli ya sekondari Mgogoni connecting, Wilaya ya Chake Chake Pemba Mussa Ali anasema:
“Wasichana wamekua wakichelewa kufika skuli pale mvua kubwa zinapoanza kwani maji yamekua ni mengi njiani na kulazimika wanafunzi kusubiria yapite ili waende skuli. Skuli yenyewe ipo Mgogoni” alisema.
Hali ni mbaya zaidi Kidemeni. Wanafunzi wa maandalizi wamekosa kabisa madarasa ya kusomea.
Mkazi wa Kidemeni aliongeza:
“Wanafunzi waliopo kijiji cha Kidemeni wakosa madarasa ya kusomea kabisa na kulazimika kusoma katika nyumba ya mtu. Hawa ni wanafunzi wa maandalizi” alisema.
Ripoti ya UNESCO 2022 inaonesha majanga ya hali ya hewa yanasababisha wasichana milioni 4 kukosa skuli kila mwaka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
UCHUMI WA NYUMBANI UMEYUMBA
Wanawake wengi Zanzibar wanategemea uvuvi mdogo, kilimo cha mboga, mwani na ufundi wa mikono. Sekta zote hizi zinaathirika.
Bi. Mwanaidi Hassan, mfanyabiashara wa samaki Kidoti Unguja, anasema: “Bahari imekuwa na dhoruba nyingi. Siku nyingi hatuwezi kutoka. Samaki pia wamepungua kwa sababu ya joto la bahari. Biashara imepungua nusu.”
Wataalamu wa kilimo wanasema mabadiliko ya tabia nchi sasa yanathiri moja kwa moja chakula na kipato cha familia za Zanzibar.
Mtaalamu wa kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Dk. Hamad Suleiman, alisema:
“Mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri moja kwa moja usalama wa chakula na uchumi wa wananchi. Mvua zisizotabirika zinaharibu mazao, ukame unapunguza mavuno, na joto la bahari linapunguza samaki. Wanawake ndio wanaobeba mzigo kwa sababu wengi wanategemea kilimo na uvuvi mdogo kwa ajili ya lishe ya familia na kipato” alisema.
WATAALAMU: MISITU NI UHAI
Wataalamu wa mazingira wanasema uharibifu wa misitu umezidisha athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa wanawake na watoto wa Zanzibar.
Akizungumzia mchango wa jamii katika uhifadhi wa mazingira, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Uhifadhi wa Misitu Pemba CFP, Mbarouk Mussa, anasema:
“Changamoto za mabadiliko ya tabianchi haziwezi kutenganishwa na uharibifu wa misitu. Tunapokatakata miti bila kupanda mingine, tunaharibu vyanzo vya maji, tunaruhusu mmomonyoko wa udongo na kuongeza joto. Haya yote yanawapata zaidi mama anayetafta kuni na mtoto anayekosa maji safi” alisema.
Wataalamu wa mazingira Ali Abdi Mohamed kutoka Kitengo cha Tabianchi, Idara ya Mazingira Pemba wanaeleza kuwa:
“Misitu ina mchango mkubwa katika kufyonza hewa ya ukaa ambayo ndiyo chanzo kikuu cha ongezeko la joto duniani. Tunapohifadhi na kupanda miti mingi, tunapunguza joto kali linalowasumbua mama na watoto, tunalinda vyanzo vya maji na tunapunguza mafuriko” alisema.
SERIKALI NA VIONGOZI WACHUKUA HATUA
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imebainisha kuwa ushiriki wa wananchi, hasa wanawake, ndio ufunguo wa kushinda vita dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.
Kaimu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Mheshimiwa Hamza Hassan Juma, amesema:
“Ushiriki wa wananchi katika kampeni za upandaji miti, uhifadhi wa misitu na matumizi bora ya ardhi ni msingi muhimu wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Wanawake ndio walio mstari wa mbele kuhifadhi mazingira nyumbani, hivyo ni lazima wawekewe mazingira wezeshi na kupatiwa elimu” alisema.
Serikali kupitia Sera ya Mazingira ya Zanzibar ya mwaka 2013, Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi na Sera ya Uchumi wa Buluu ya 2020 inaendelea kutekeleza miradi ya nishati safi, maji salama, upandaji miti ya mikoko na majiko ya nishati mbadala.
HITIMISHO: NI WAJIBU WETU SOTE
Mabadiliko ya tabia nchi yana uso ambapo ni uso wa mama anayepika kwa kuni kwa sababu ya kukosa nishati mbadala, ni uso wa mtoto anayekaa na kusoma nyumbani na kukosa kabisa darasa.
Bado ipo nafasi ya kuokoa hali. Kupanda miti, kutumia nishati safi, kutunza bahari na vyanzo vya maji, na kutoa elimu kwa jamii ni hatua muhimu.
Ni wakati sasa kwa kila mmoja kutambua kuwa mazingira ni uhai wetu. Tusipochukua hatua leo, kesho itakuwa ngumu zaidi kwa mama na mtoto wa Zanzibar.
Mwisho
0 Comments