SHUGHULI ZA KIJAMII ZINAVYOTATIZWA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI


NA-HABIBA ZARALI-PEMBA 

Dunia ya leo inapitia kipindi kigumu cha mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea kuathiri maisha ya watu katika nyanja mbalimbali.

Kupanda kwa joto duniani, kuongezeka kwa ukame, mafuriko, kupungua kwa vyanzo vya maji na kuharibika kwa mazingira ni miongoni mwa changamoto zinazoikumba dunia kwa sasa.

Athari hizi hazibaki katika mazingira pekee, bali zinaingia moja kwa moja katika maisha ya kijamii, uchumi na maendeleo ya taifa.

Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, wananchi wengi wameanza kushuhudia mabadiliko hayo kupitia kupungua kwa mavuno, kuongezeka kwa magonjwa, kuharibika kwa miundombinu na hata kushuka kwa shughuli za kiuchumi zinazotegemea mazingira.
Hali hii imeifanya dunia kuendelea kutoa tahadhari kuwa ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa sasa, kizazi kijacho kitaingia katika hatari kubwa zaidi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ya mwaka 2024, kiwango cha joto duniani kimeendelea kuongezeka kwa kasi kutokana na shughuli za kibinadamu zinazochangia hewa ya ukaa.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa mwaka 2023 ulikuwa miongoni mwa miaka yenye joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa duniani.

Aidha, Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa zaidi ya watu milioni 733 duniani walikumbwa na uhaba wa chakula mwaka 2023 kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi pamoja na migogoro ya kiuchumi na kisiasa.

Kwa upande wa Afrika Mashariki, wataalamu wa mazingira wanaeleza kuwa ongezeko la ukame na mvua zisizotabirika limekuwa likisababisha changamoto kubwa kwa sekta za kilimo, afya, elimu na uchumi wa buluu ambao ndio uti wa mgongo wa maisha ya wananchi wengi wa Zanzibar.

WAKULIMA WALALAMIKIA KUPUNGUA KWA MAVUNO

Wakulima wengi Zanzibar wameanza kuhisi madhara ya mabadiliko ya tabia nchi kupitia kupungua kwa mavuno ya mazao yao.
Mkulima wa mwani kutoka Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba, Asha Ali Kombo anasema kuwa hali ya joto la bahari imeathiri uzalishaji wa mwani kwa kiwango kikubwa.

“Miaka ya nyuma tulikuwa tukivuna mwani kwa wingi sana, lakini sasa joto la maji limeongezeka na mwani wengi wanaharibika kabla ya kukua vizuri, kipato chetu kimeshuka sana,” alisema.

Amina Mbarouk mkulima wa mpunga Gando Wilaya ya Wete Pemba anasema baada ya kuingiwa na maji chumvi katika mashamba yao wamekuwa na hali duni za umasikini.

Naye mkulima wa mpunga kutoka Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba, Salim Haji, anasema mvua zisizotabirika zimekuwa changamoto kubwa kwa wakulima.

“Tunategemea mvua kwa ajili ya kilimo chetu, lakini sasa mvua zinachelewa au zinanyesha kwa nguvu na kuharibu mashamba, wakulima wengi tunaingia hasara,” alisema.

SEKTA YA KILIMO INAATHIRIKAJE

Mtaalamu wa kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Dk. Hamad Suleiman, alisema mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri moja kwa moja usalama wa chakula na uchumi wa wananchi.

Alisema kutokana na kupungua kwa mvua na kuongezeka kwa joto, ardhi nyingi zimeanza kupoteza rutuba na kusababisha mazao kutokua vizuri.

“Mabadiliko ya tabia nchi yanaathiri sekta ya kilimo kwa kiwango kikubwa. Serikali inaendelea kuhamasisha matumizi ya mbegu zinazostahimili ukame pamoja na teknolojia za kisasa za umwagiliaji ili kupunguza athari hizi,” alisema.

SEKTA YA AFYA NAYO YAATHIRIKA

Mbali na kilimo, sekta ya afya pia imeanza kuathirika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Mtaalamu wa afya kutoka Wizara ya afya ambae ni mkuu wa kitengo cha afya na mazingira Khalfan Shaha Bakar Mmoja, alisema ongezeko la joto pamoja na mafuriko limekuwa likichangia kuenea kwa magonjwa ya mlipuko.

“Tunashuhudia ongezeko la magonjwa kama malaria, kipindupindu na maambukizi ya mfumo wa upumuaji kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, mafuriko yanachafua vyanzo vya maji na kuongeza hatari ya magonjwa,” alisema.

Aliongeza kuwa watoto na wazee ndio huathirika zaidi kutokana na uwezo mdogo wa miili yao kukabiliana na mabadiliko hayo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kati ya mwaka 2030 hadi 2050 watu zaidi ya laki mbili na hamsini elfu wanatarajiwa kufariki kila mwaka duniani kutokana na magonjwa yanayochangiwa na mabadiliko ya tabia nchi.

ELIMU YATIKISWA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Mabadiliko ya tabia nchi pia yanaendelea kuathiri sekta ya elimu.

Mtaalamu wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dk. Khadija Othman, alisema wanafunzi wengi wamekuwa wakikosa masomo kutokana na majanga ya mafuriko na ukame.

“Katika baadhi ya maeneo, skuli zimeharibika kutokana na mvua kubwa na mafuriko ambapo baadhi ya watoto hushindwa kuhudhuria darasani,” alisema.

Alifahamisha elimu ya mazingira inapaswa kupewa kipaumbele ili kuwajengea vijana uelewa wa namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

UCHUMI WA BULUU WATAJWA KUWA HATARINI

Kwa Zanzibar, uchumi wa buluu ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia maendeleo ya taifa.

Hata hivyo, wataalamu wanaeleza kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanaweka sekta hiyo katika hatari kubwa.

Mtaalamu wa uchumi wa buluu, Profesa Abdalla Kombo, alisema kuongezeka kwa joto la bahari na uchafuzi wa mazingira ya baharini kunaathiri uvuvi pamoja na utalii.

“Bahari inapopata joto kupita kiasi, viumbe wa baharini huathirika na baadhi yao kuhama, hali inayopunguza samaki na kuathiri kipato cha wavuvi. Aidha, kuharibika kwa fukwe na matumbawe kunaathiri sekta ya utalii ambayo ni chanzo kikubwa cha mapato Zanzibar,” alisema.

WATAALAMU WA MAZINGIRA WATAKA HATUA ZAIDI

Mtaalamu wa mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Saada Mohammed, alisema bado kuna haja kubwa ya kuongeza juhudi za uhifadhi wa mazingira.

Mkuu wa Divisheni ya Mazingira Ofisi ya Pemba, Mwalimu Khamis, anasema ukataji wa miti, matumizi mabaya ya ardhi na uchafuzi wa mazingira vinaendelea kuongeza kasi ya mabadiliko ya tabia nchi.

“Jamii lazima ibadili mtazamo wake kuhusu mazingira. Kupanda miti, kutunza vyanzo vya maji na kuepuka uchafuzi wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi,” alisema.

SERIKALI YASEMA INAENDELEA KUCHUKUA HATUA

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekuwa akisisitiza umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari kupitia sera ya uchumi wa buluu.
Katika maelezo yake kuhusu maendeleo endelevu, Dk. Mwinyi anasema serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya mazingira, uhifadhi wa bahari na matumizi ya nishati safi ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Naye Afisa Mdhamini wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar anayesimamia mazingira, Ahmed Abubakar Mohamed, alisema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

“Tunaendelea kuimarisha sera, sheria na mikakati ya uhifadhi wa mazingira pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya rasilimali za asili,” alisema.
SERA, SHERIA NA MIKAKATI YA SERIKALI

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.

Kupitia Sera ya Mazingira ya Zanzibar ya mwaka 2013 pamoja na Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi, serikali imeweka msisitizo katika uhifadhi wa mazingira, matumizi ya nishati safi na ulinzi wa vyanzo vya maji.

Aidha, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar Na. 3 ya mwaka 2015 imeendelea kuhimiza matumizi endelevu ya rasilimali za asili ili kupunguza uharibifu wa mazingira.

Serikali pia imeendelea kuhamasisha upandaji miti pamoja na matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.

Kwa upande mwingine, Sera ya Uchumi wa Buluu Zanzibar ya mwaka 2020 inalenga kuhakikisha rasilimali za bahari zinatumika kwa njia endelevu bila kuharibu mazingira ya baharini.

KAIMU WAZIRI OFISI YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS ATOA RAI

Kaimu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Hamza Hassan Juma, anasema mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi yanahitaji ushirikiano wa kila mmoja.
Anafahamisha serikali pekee haiwezi kushinda vita hiyo bila wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira.

“Tunapaswa kutambua kuwa mazingira ni msingi wa maisha yetu. Tukiharibu mazingira, tunaharibu maisha yetu wenyewe. Hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika kuyatunza mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.

HITIMISHO

Mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa tishio kubwa kwa shughuli za kijamii duniani na Zanzibar kwa ujumla.

Athari zake zinaonekana katika sekta ya kilimo, afya, elimu, uchumi wa buluu na maisha ya wananchi kwa ujumla.

Wakulima wanalia kwa hasara, wagonjwa wanaongezeka hospitalini, wanafunzi wanakosa elimu na uchumi unaanza kuyumba kutokana na uharibifu wa mazingira.

Hata hivyo, bado ipo nafasi ya kuokoa hali hiyo ikiwa jamii, serikali na mashirika mbalimbali yataendelea kushirikiana katika kulinda mazingira.

Kupanda miti, kutumia nishati safi, kutunza bahari na vyanzo vya maji pamoja na kutoa elimu kwa jamii ni baadhi ya hatua muhimu zitakazosaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Ni wakati sasa kwa kila mmoja kutambua kuwa mazingira ni uhai wetu. Tusipochukua hatua leo, kesho inaweza kuwa ngumu zaidi kwa vizazi vijavyo.

Mwisho

Post a Comment

0 Comments