Umuhimu wa Lishe Bora kwa Makuzi ya Awali ya Mtoto


Na-Fatma Suleiman

Je, unajua kwamba nusu ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinatokana na ukosefu wa lishe bora? Hapa Zanzibar, kiwango cha utapiamlo bado hakikubaliki. Lishe si suala la hiari bali ni uwekezaji muhimu kabisa kwa maisha ya mtoto wako na kwa mustakabali wa taifa zima.
Katika miaka mitano ya mwanzo, mwili na akili ya mtoto hukua kwa kasi ya ajabu. Kila sahani unayomwandalia mtoto wako ni hatua ya kujenga kesho yake.

Hali ya Lishe Zanzibar: Takwimu Zinazoshtua
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Zanzibar Multisectoral Nutrition Strategic Action Plan 2024/25 - 2028/29 inakiri kwamba viwango vya utapiamlo viko juu sana. Mpango huu wa miaka mitano umeandaliwa mahususi kushughulikia changamoto hii kwa kushirikiana na UNICEF. 

Utafiti wa hivi karibuni unaonyesha pia mzigo wa utapiamlo wa aina mbili na tatu kama udumavu pamoja na unene kupita kiasi  unaendelea kuathiri watoto na vijana wliomo katika maskuli  Zanzibar.

Kwa Nini Lishe Bora ni Muhimu Sana Katika Miaka ya Mwanzo?

1. Ukuaji wa Mwili
Protini, wanga, mafuta yenye afya, vitamini na madini ni matofali ya kujenga mifupa imara, misuli yenye nguvu, na viungo vyenye afya. Mtoto anayekula vizuri ana nguvu za kucheza, kukimbia, na kuchunguza dunia.

2. Maendeleo ya Akili 
“Siku 1,000 za dhahabu” — kutoka ujauzito hadi mtoto anafikisha miaka miwili  ni kipindi muhimu zaidi kwa ubongo. Virutubisho kama chuma, omega-3, na vitamini B huboresha kumbukumbu, umakini, na uwezo wa kujifunza. Mtoto mwenye lishe bora huanza shule akiwa tayari.

3. Kuimarisha Kinga ya Mwili
Vitamini A, C, D na madini ya zinc ni askari wanaolinda mwili wa mtoto dhidi ya magonjwa ya kuhara, homa, na malaria. Lishe duni hudhoofisha ngao hii na kumfanya mtoto augue mara kwa mara.

4. Kuzuia Utapiamlo na Madhara Yake ya Muda Mrefu
Utapiamlo hutokea kwa: 
-Upungufu wa virutubisho, mtoto anakula lakini chakula hakina protini, vitamini, au madini ya kutosha.
Lishe isiyo na uwiano kula wanga tu bila mboga na matunda.
- Ulaji mbaya kupita kiasi vyakula vya sukari na mafuta mengi vinavyosababisha unene. 

Madhara ya utapiamlo kama udumavu na upungufu wa damu mara nyingi hayawezi kurekebishika mtoto akikua.

Mfano wa Mlo Kamili kwa Mtoto Chini ya Miaka 5

Kiamsha Kinywa:
Uji wa ulezi au mtama uliopikwa kwa maziwa + tunda moja: ndizi, papai, au embe.

Mchana:
Wali au ugali mdogo + mboga za majani kama mchicha au kisamvu + kipande cha samaki, dagaa, au supu ya kuku. Malizia na glasi ya juisi safi ya matunda.

Jioni:
Viazi vilivyochemshwa au kipande cha mkate wa ngano + yai la kuchemsha au dengu + mboga za rangi tofauti kama karoti na nyanya.

Vitafunwa Bora Kati ya Milo:
Parachichi, karanga laini, mtindi, au tunda kama chungwa na apple.

Kumbuka: Lenga rangi nyingi kwenye sahani. Rangi tofauti humaanisha virutubisho tofauti.

Changamoto Halisi Zinazowakabili Wazazi na Walezi Zanzibar

1. Ukosefu wa Elimu ya Lishe: Wazazi wengi hawajui ni vyakula gani vinampa mtoto virutubisho sahihi.
2. Umaskini: Bei ya vyakula vyenye lishe kamili huwafanya wazazi wengi washindwe.
3. Mila na Desturi: Baadhi ya jamii huzuia watoto kula mayai au samaki, jambo linalowapunguzia protini muhimu.

Wajibu Wetu Sote
Kuhakikisha kila mtoto anapata lishe bora si kazi ya mama pekee. Ni jukumu la familia, jamii, na serikali — ndiyo maana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imezindua mpango maalum wa miaka mitano kushughulikia lishe.

Hitimisho: 
Lishe bora katika umri mdogo ni nguzo ya maisha yote ya mtoto. Inajenga mwili, inanoa akili, na inampa ngao ya kupambana na magonjwa. Tuwekeze kwenye sahani za watoto wetu leo — tunajenga Zanzibar yenye nguvu, yenye afya, na yenye wataalamu wa kesho.


Je, umeipenda makala hii? Share na mzazi mwenzako. Kama una swali au uzoefu wako kuhusu lishe ya watoto Zanzibar, tuandikie maoni yako hapo chini.

Post a Comment

0 Comments