Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuzingatia Afya ya mtoto hasa katika makuzi ya awali imezindua programu ya makuzi na malezi ya awali ya mtoto itakayowaunganisha wazazi na walezi katika kuziendea afua mbalimbali za mtoto.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika hafla ya uzinduzi wa Programu jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto Zanzibar sambamba na ufunguzi wa Kituo cha kulelea watoto katika Soko la Mwanakwerekwe.
Amesema Serikali inaamini kuwa uwekezaji katika malezi na makuzi ya awali ya mtoto ni uwekezaji wenye tija kubwa kwa maendeleo ya Taifa na kuleta manufaa makubwa katika afya, elimu, ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Mhe. Hemed amefahamisha kuwa Serikali imepiga hatua zaidi katika kuhakikisha watoto wanapata mwanzo bora wa maisha yao ambapo wazazi na walezi wakipata mazingira yanayowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali bila ya kuwa na wasiwasi kuhusu usalama na ustawi wa watoto wao.
Sambamba na hayo amesema kuwepo kwa vituo vya kulelea watoto katika masoko, mahospitalini na skuli za awali vitasaidia watoto wote wa Zanzibar kupata haki ya kukua katika mazingira salama yenye afya, lishe bora, ulinzi na fursa za kujifunza tangu wakiwa wadogo.
Hata hivyo, ametoa angalizo kuwa kituo hicho sio jengo tu bali ni uwekezaji katika kizazi sasa na kijacho hivyo ameitaka jamii, wafanyabiashara, viongozi wa Soko na taasisi zote kuhakikisha kituo hicho kinatunzwa vizuri ili kiendelee kutoa huduma bora kwa watoto kwa miaka mingi ijayo.
Nae Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar Mhe. ANNA ATANAS POUL amesema Wizara yake itahakikisha vituo vya kulelea watoto ( EARLY CHILDHOOD ) vinakuwepo kwa wingi kuanzia ngazi ya Shehia hadi Mkoa kwa lengo la kuhakikisha watoto wanalelewa katika malezi bora na salama na kupata Taifa lenye wataalamu bora katika kila fani.
Mhe. ANNA amesema kabla ya kuanzishwa kwa program hio wazazi walikuwa na changamoto ya kukosa eneo maalum kwa ajili ya kulelewa watoto wao pindi wanapokuwa katika majukumu yao ya kazi hivyo uwepo wa kituo hicho ni fursa kwa watoto wote waliofikia umri wa miaka miwili kupelekwa katika vituo hivyo jambo litakakalowasaidia wazazi na walezi kufanya kazi kwa utulivu wa hali ya juu.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Mhe. Dkt. SAADA MKUYA SALUM amesema safari ya Maendeleo ya Zanzibar kufanikiwa kwake kunahitaji kumuangalia mtoto katika kupata haki ya kulelewa na kukuzwa katika mazingira mazuri yatakayomjenga kiafya, kielimu, kifikra na kumuwezesha kukiwa katika mazingira bora na salama.
Dkt. Mkuya amesema Serikali katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa imezindua programu maalamu ya malezi, makuzi na maendelelo ya awali ya mtoto ambayo yanahitaji mashirikiano makubwa na utayari wa Serikali, washirika wa maendeleo, Taasisi mbalimbali, wazazi na walezi katika kufikia mpango huo wa malezi na makuzi bora ya watoto.
Akizungumza kwa niaba ya washirika wenzake waliofadhili Program hiyo Meneja wa Stanbic Benki Bwana DERICK LUGEMALA amesema wameamua kuekeza katika miradi ya kimkati ikiwemo suala la kumuwezesha mtoto aweze kukua katika mazingira mazuri na salama ili wazazi wao wapate muda mzuri wa kufanyakazi zao.
Amesema nchi nyingi bado hawajalipa kipaombele suala la makuzi ya awali ya mtoto hivyo kupitia programu hio watahakikisha watoto wote wa Zanzibar wananufaika na kushiriki kikamilifu katika program hiyo itakayowakuza na kuwapatia ulinzi Imara wa maisha yao.
0 Comments