WAJUE NDEGE
NDEGE ni aina ya mnyama. Tofauti ya ndege na wanyama wengine ni kwamba ndege ana mabawa yanayomwezesha kuruka angani aidha ndege hutaga mayai
Ndege wako wa aina nyingi, wakubwa na wadogo ni kama Tai, Mbuni, Korongo, Bata mzinga, Bundi, Tausi, Mwewe na wengine wengi.
Ndege wadogo wengine ni kama tetere, Mbayuwayu, Jorohe, Kasuku, Charwe, Chiriku, Kwelea kwelea, na wengine.
MAISHA YA NDEGE
Maisha ya ndege hutegemea sana mazingira. Mazingira mazuri huwafanya ndege kuishi kwa amani, furaha mustarehe. Mazingira yakiharibiwa husababisha ndege huhamia mahali pengine au kuwa waharibifu.
Ndege hupendelea kuishi mahali pa utulivu na panapovutia. Idadi na aiana toafauti za ndege ni moja ya ishara zinazoonyesha kuwepo kwa mazingira bora. Umri wa kuishi ndege hutfautiana kama zilivyo aina zao, lakini kuna baadhi ambao hufikia kuishi miaka 15.
MAKAZI YA NDEGE
Ingawa ndege huishi kwenye mazingira tofauti kulingana na aina au jamii husika. Lakini wengi huishi misituni.
Ndege wengi hujenga viota hasa misimu ya kuzaliana. Viota hivi hujengwa kwa kutumia majani, dongo na vijiti. Vilevile wapo ndege waishio mapangoni.
Viota vya ndege hujengwa kwa ustadi mkubwa ili kuwakinga na baradi, mvua, maadui na upepo mkal wakati wa kuzaliana. Ndege wengi hutumia viota kwa kuzaliana si kuishi.
Ndege hupendelea kujenga viota vyao juu ya miti, ndani ya mapango, kwenye paa au kona za nyumba ili mradi tu sehemu hizo ziwe za usalama. Aidha mahali hapo ni lazima pawe pana maji, chakula, upepo, na pia mandhari mazuri.
Ndege wengine hupendelea kuishi majini, kwa mfano batamaji. Wengine hupenda kuishi kwenye ardhi owevu.
UZAZI WA NDEGE
Kwa kawaida ndege jike hutaga mayai ambayo huangaliwa na kup[atikana kwa kinda. Kabla ya hapo ndege dume na jike hujamiiana ili kurutubisha mayai. Ndege hawanyonyeshi hivyo makinda hukua kwa kuletewa vyakula na wazazi wao wanaovipata kwenye mazingira yanayowazunguka. Idadi ya mayai hutofautiana na aina ya ndege. Kuna wanaotaga mayai mawili kama njiwa na wengini mayai mengi kama mbuni.
Baada ya kutaga jike mara nyingi hulazimika kuatamia mayai kwa siku kadhaa kabla ya makinda kuanguliwa. Siku za kuatamia hutofautiana kulingana na aina ya ndege. Wapo wanaoatamia kwa siku 14, 21, 42 au zaidi. Walio wengi huatamia kwa siku 21.
Wakati wa kuatamia mayai ndege jike hulazimika kukaa kiotani bila ya kula chakula kwa muda Fulani kwa nia ya kuyapa joto mayai. Hali hii hufanya jike kunyonyoka manyoya na hata kukonda.
Jike hunyonyoka manyoya sehemu za tumboni ili kuweza kuyapasha joto mayai yake vizuri. Wakati mwingine ndege dume hulazmika kuleta chakula kiotani ili kumlisha jike. Baadhi ya ndege dume husaidia kuatamia mayai jike anapokwenda kujitafuatia chakula. Makinda wanapoanguliwa huwa hawana uwezo wa kuruka kwani mabawa yao hayana manyoya, hivyo hubaki kiotani. Kwa wakati huo jike na dume husaidiana kulinda makinda wao mpaka watakapomudu kuruka na kujitafutia chakula.
CHAKULA CHA NDEGE.
Ndege hula vyakula vya aina mbalimbali kama vile nafaka, wadudu, mizigo, matunda, majani, samaki, mabaki ya vyakula nekta nakadhalika.
Ulaji wa vyakula hivi hutegemeana na aina ya ndege na maumbile yake. Kwa mfano ndege wenye midomo iliyochongoka hunyonya nekta ya maua. Ndege aina ya Tai hula mizoga; hawa midomo yao ni mikubwa na imara Aidha ndege pia hutumia kucha zaokujipatia chakula kwa njia ya kuchakua. Wengine hutumia mdomo yao na kucha zao kwutafuta wadudu , samaki, na hata wanyama wadogo wadogo.
MAUMBILE YA NDEGE.
Ndege hutofautiana kimaumbile. Ipo tofauti kati ya Dume na Jike pia makinda. Kwa mfano Tausi dume ana rangi nzuri zaidi kuliko jike na mkia wake ni mrefu na wenye urembo mwingi na rangi nzuri.
Njiwa jike huwa na mdomo mrefu kuliko njiwa dume. Bundi jike shingo yake ni nyembamba wakati ile ya dume ni nene.
Wakati mwingine ukubwa wa vichwa hutofautisha ndege jike na dume. Jike huwa na kichwa kidogo ambapo dume chake ni kikubwa. Baadhi ya ndege dume huwa na ushungi juu ya vichwa vyao.
Mara nyingi dume huwa na umbile kubwa na rangi za kupendeza kuliko jike.
Ndege wana manyoya mazuri yenye rangi za kuvutia kwa mfano, Tausi, Kanga, Kasuku, na wengine kwa sababu hii manyoya yao hutumika kwa mapambo. Ndege wana sauti tofauti kama walivyo wanadamu.
Sauti za ndege huburudisha, kama vile ile ya Chiriku. Nyimbo za ndege huwa na maana na ujumbe fulani.Madhalani ndege dume aimbapo huashiria jike kwamba ‘liko dume bora hapo’. Madume wengine wasingilie himaya yake vinginevyo vita vitazuka.
Baadhi ya sauti huashiria hatari na kutoa tahadhadhari. Baadhi ya ndege huimba kwa muda mfupi huku wakibadilisha sauti, wakati wengine hawawezi kubadilisha sauti. Chiriku anaaminika kuwa ndege mwenye sauti nzuri zaidi ya wengine.
Sauti za ndege pia huoanishwa na matukio katika jamii mbalimbali. Kwa mfano Bundi kwa jamii nyingi za kiafrika huaminika kuwa ni ndege wa uchuro. Lakini Ulaya bundi ni ndege wa busara.
Ndege huhama kutoka sehemu mmoja kwenda nyingine. Sababu za uhamiaji huo ni kutafuta chakula, maji, mabadiliko ya hali ya hewa na kuharibiwa mazingira yao. Pia hutafuta sehemu za kuzaliana.
Ndege wana tabia ya kuishi kwa makundi kulingana na aina zao. Huruka au hutembea pamoja kwa mafano korongo, penguini, yangeyange, kunguru, kweleakwelea na wengine wengi.
FAIDA
Kuwepo kwa ndege katikamazingira ni mapambo na burudani. Pia ishara ya utajiri wa bioanuwai ya mahali pale.
Manyoya ya ndege hutumika kutengenezea mapambo mbalimbali na nguo za kujikinga na baridi.
Ndege huwasaidia wakulima kupunguza wadudu waharibifu kwa kuwala.
Ndege ni kivutio kwa watalii hivyo huliongezea taifa mbegu.
Ndege husaidia kuchavusha mimea na kusambaza mbegu.
Maadui wakubwa wa ndege ni binadamu, nyoka na ndege wengine. Wapo ndege ambao ni waharibifu kama vile kwelea kwelea ambao hula mazao mashambani, kunguru weusi wanaochafua mazingira kwa kusambaza magonjwa.
CHA KUFANYA
Tuhifadhi mazingira ambayo ni makazi ya ndege.
Tusiwabughudhi ndege ili wasihame
Jamii ielimishe kuhusu umuhimu wa ndege ili iwahifadhi.
chanzo:http://jaizmelaleo.blogspot.com
chanzo:http://jaizmelaleo.blogspot.com
0 Comments