RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imejitahidi kulinda haki za binadamu na kutekelezwa kwa mujibu wa Mikataba ambayo Tanzania ni mwanachama.

Alisema, jitihada kubwa zimechukuliwa kuboresha hali ya upatikanaji wa haki mbalimbali za binaadamu zikiwemo usawa mbele ya sheria, afya, elimu, maji na mazingira safi, uhuru wa kutoa maoni, uhuru wa kuabudu, ajira, haki ya kumiliki mali na uhuru wa vyombo vya habari.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameyasema hayo ukumbi wa mikutano wa kimataifa jijini Arusha (AICC) alipomwakilisha Rais Samia kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 77 wa Tume ya Afrika ya Haki za Binaadam na watu.

Alisema, kutokana na uhuru huo, sasa Tanzania ina vyombo vya habari vingi zikiwemo redio 210, televisheni 56, magazeti 288 pamoja na mitandao mbalimbali ya kijamii.

Pia, alisema Tanzania imeimarisha uhuru wa kidemokrasia, haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.

Alieleza, bara la Afrika bado linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mapinduzi ya Serikali zilizo madarakani, vita vya wenyewe kwa wenyewe, mila na desturi zisizofaa, ukatili wa kijinsia, athari hasi za utandawazi na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu haki zao.

Rais Mwinyi alitoa wito kwa nchi na Serikali zote wanachama wa Umoja wa Afrika kuchukua hatua stahiki kukabiliana na changamoto hizo. Aidha, alieleza changamoto zote hizo wahanga wakubwa ni wanawake na watoto.

Pia, alieleza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kulitambua hilo, imeendelea kuchukua hatua za kutatua migogoro mbalimbali na kutekeleza Tamko la Dar es Salaam kuhusu Amani, Usalama, Demokrasia na maendeleo kwa Ukanda wa Maziwa Makuu.

Alisema, hivi sasa Tanzania inashiriki kwenye jeshi la Umoja wa Mataifa, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (Stabilization Mission) na Jeshi la Kulinda Amani (MONUSCO).

Pia, alielieza Tanzania inashiriki Jeshi la pamoja la kulinda amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na muda mrefu imeshiriki ulinzi wa amani nchi mbalimbali zikiwemo Darfur Sudan na Visiwa vya Comoro.

Hata hivyo, alitoa rai kwa washiriki wa mkutano huo, kutoa michango itakayoboresha hali ya haki za binadamu Afrika.

Wakizungumza kwenye Mkutano huo, Waziri wa Katiba na Sheria wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Pindi Hazara Chana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman walisema Mkutano huo wa 77 unaofaendelea Tanzania ni mwendelezo wa urithi na maono ya hayati baba wa taifa, Julius Kambarage Nyerere kwa kuendeleza ushirikiano wake na nchi nyengine za bara la Afrika tokea historia ya bara hilo kwenye harakati za uhuru na ukombozi wa Afrika na sawa Rais Dk Samia Suluhu Hassan na Rais Dk. Mwinyi bado wanaendeleza ushirikiano na nchi za Bara hilo kuendelea kupambania haki za Binaadam.

Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Watu, Prof. Remy Ngoy Lumbu, ameitaka Afrika ishirikane kukabiliana na matatizo yao ikiwemo rushwa, ukosefu wa miundombinu imara, haki duni za jamii kama afya, maji safi na umasikini pia alitoa wito kwa mataifa yote ya Afrika kujitahidi kufanikisha malengo ya itifaki ya Mapundo ambayo kwasasa inatimiza miaka 20 bila matarajio waliyoyakusudia.

Mkutano wa huo wa 77 umehudhuriwa na washiriki wapatao 900 wakiwemo mawaziri wa Sheria na haki za binaadamu wa nchi 35 za Afrika, Mabalozi na Viongozi wa Taasisi za Kitaifa za Haki za Binadamu, Asasi za Kiraia (AZAKI) pamoja na wawakilishi wa Serikali na makundi mbalimbali kutoka Bara la Afrika.

Awali mkutano huo ulitanguliwa na majukwaa ya taasisi za Kitaifa za Haki za Binadamu zipatazo 46 na Asasi za Kiraia takribani 210 kutoka Bara la Afrika waliojadili masuala ya ulinzi, utetezi na uhifadhi wa haki za binadamu barani Afrika.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR*