Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema Serikali itaendelea kutekeleza kwa ufanisi mikakati muhimu inayohakikisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, kwa wananchi wa mijini na vijijini, ili kufanikisha Mipango ya Maendeleo na Kukuza Uchumi wa Nchi.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo leo akiwahutubia viongozi na wananchi wakati wa Ufunguzi wa Maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, huko Chamanangwe, Shehia ya Kiuyu-Minungwini, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema, Serikali inaendelea na Utekelezaji wa Mikakati hiyo ambayo imejiwekea, kupitia Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya Mwaka 2050, kwa dhamira pia ya kutambua kuwa, maji ni sehemu ya uhai, afya na haki ya msingi ya binadamu.
Akibainisha Mikakati ambayo ni pamoja na rasilimali hiyo muhimu amesema, hadi kufikia Mwezi wa Machi 2023, hali ya uzalishaji wa maji Nchini imeendelea kuimarika, kwa kufikia asilimia 67 visiwa vya Unguja na Pemba, ikilinganishwa na asilimia 56 iliyofikiwa mwezi Machi 2022, huku Kiwango cha Uzalishaji-maji kikitarajiwa kuongezeka na kufikia wastani wa asilimia 75 ifikapo mwishoni mwa Mwaka 2023.
“Ni dhahiri kwamba mahitaji ya maji Nchini yameendelea kukua, hivyo ni budi kila mmoja wetu kuyatunza na kuyatumia kwa uangalifu, sambamba na kuvitunza vyanzo vyenyewe; kutokana na ukweli huo, Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi, Washirika wa Maendeo, pamoja na Asasi za Kiraia, tunao wajibu mkubwa wa kuwawezesha wakulima, ili kuendeleza juhudi za uzalishaji wa chakula, na hatimaye kuongeza tija kwa maendeleo yao binafsi na jamii kwa ujumla, kwaajili pia ya kuiwezesha Nchi kujitosheleza kwa chakula, huku tukizingatia matumizi bora na endelevu ya maji”.
0 Comments