Imeandikwa na Salmin Juma - Zanzibar

Mrajisi wa Jumuiya zisizo za Kiserikali Zanzibar, Nd Ahmed Khalid Abdulla ameipongeza Jumuiya ya ya Ladies Joints Forum kwa kuona umuhimu wa kuwapatia elimu ya "uhifadhi na uwendelezaji wa rasilimali katika mradi wa Her Climate" wanawake na akina mama ndani ya Wilaya ya Kusini Unguja, amesema kufanya hivyo kutasaidia kwa hatua kubwa kuondosha tabaka la kiuchumi baina yao na akina baba.
Pongezi hizo zimetolewa leo huko katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Kusini Unguja na mwakilishi wa Mrajis ambae alikua mgeni rasmi Nd: Nassor Ali Mohd alipokua akiufungua mkutano maalum kuhusu utambulisho wa Mradi huo.
Nassor amesema , moja miongoni mwa rasilimali muhimu nchini, ni zao la mwani, hivyo taasisi ya Ladies Joint Forum kuja na mpango kazi kuhusu uimarishaji wa zao hilo ni wazi kua kutawasaidia sana akina mama kujikuza kiuchumi.
"kwa mujibu wa maelezo, naamini kazi yenu baada ya miaka minne mpaka mitano mbele tutaona imeleta faida kubwa kwa akina mama na vijana wa kike" amesema Nassor.
Akifafanua zaidi kuhusu mradi huo Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Ladies Joint Forum Miriam Dominick amesema, mradi huo unalenga kutoa mafunzo na taaluma mbalimbali za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo wanawake 25 kutoka Paje watachaguliwa kupata mafunzo hayo ili wawe na uwezo wa kuzalisha mwani wenye kiwango na ubora hata kama kutakua na mabadiliko ya hali ya hewa.
"kwa hatua ya awali hatuwezi kuchukua watu wengi na ndio maana kwanza tunaanza na watu 25 ambao watakua mabalozi kwa wengine, lengo ni kutengeneza mawakala ambao tunaamini wataeneza kwa kasi taaluma tutakayowapatia na tunalenga elimu hii kufikiwa na watu 10,000 idadi hii inaweza kufikiwa haraka mara pale watu wetu watakaposambaza taaluma hii " amesema Miryam.

Akiendelea kuuelezea mradi huo amesema, shuhuli kubwa zitakazofanywa katika Mradio wa" Her Climate" ni kufanya vikao na viongozi kuwaelezea kuhusu mradi na faida zake ambapo hili limeshafanyika, na la pili ni mchakato wa utoaji wa mafunzo kutoka kwa wataalamu mbalimbali, na mwisho ni kuandaa mkutano ambao utawakutanisha wadau wa mazingira na wakulima wa mwani kwalengo la kuimarisha umoja wa mafanikio katika zao la hilo.
Kwa upande wake Mratibu wa Ladies Joint Forum kutoka Zanzibar Bi Nunuu Saleh Salum akijibu suala la mwandishi wa habari hizi aliyetaka kujua kwanini mradi huo unafanyika Paje amesema, eneo hilo limeonekana ndio lenye wakulima wengi wa mwani kwa Wilaya hiyo, hivyo wameamua kwenda huko ili kuwapa nguvu zaidi ya kufikia malengo yao ya kujikomboa kiuchumi.
Kwa upande wao washiriki wa mkutano huo kutoka Paje wameipongeza Jumuiya ya Ladies Joint Forum kwa uwamuzi wao wa kuwapelekea mafunzo hayo kwao huku wakiahidi kuwa, watayafanyia kazi mafunzo yote watakayopewa.
Like
Comment
Share