Imeandikwa na Fatma Suleiman - Pemba

Kwamujibu wa Takwimu kutoka Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) ni kuwa, lita 1,120,000 za maji safi na salama zinahitajika kwa watu 8,000 wa Shehia ya Ndagoni Wilaya ya Chake Chake Pemba kwa matumizi mbalimbali ya kijamii, ni sawa wa wastani wa lita 140 kwa matumizi ya kila mtu mmoja kwa siku.Jambo la kusikitisha ni kuwa lita hizo zimekuwa zikikosekana na hatimae kuwaacha wananchi hao wakitumia maji yasio salama yanayotokana na visima vya kata (vidimbwi na vishimo)
“dhiki tunayoipata akina mama ni kubwa sana, kwani toka mwezi wa ni miezi mitatu sasa maji hatuyapati na siku yanayotoka huwa usiku mkubwa wa manane na alfajiri mapema yanafungwa, hali hio inatufanya tuache vitanda na watoto wachanga tukimbilie maji mabondeni na huko huwa kumejaa watu wengi” alisema Bi Sada Rashid Haji mkaazi wa kichanjaani Ndagoni ambaye ni miongoni mwa wananchi wa vijiji vitatu Kichanjaani Depu, Kilimani na Ngagu Shehia ya Ndagoni Wilaya ya Chake Chake Pemba.
Wakaazi hao hivi sasa wamelazimika kuchimba visima vidogo vidogo kama ilivyoelezwa huko juu vilivyozoeleka sana katika maeneo ya vijijini hivyo.
Kutokana na hali ya kijografia kwa maeneo hayo ya Ndagoni kuwepo pembezoni mwa bahari ya Hindi, ni kuwa, hata wanapojaribu kuchimba visima vya uhakika ili wapate maji safi inawawiya vigumu kwasababu mahi hayo hujachanganyika na baji ya bahari na huwa na ladha ya chimvi ndani yake hivyo huwa ni vigumu kuyatumia kwa matumizi yao ya nyumbani. Uwemo wa changamoto hii, ndio umevifanya vijiji hivi kuyategemea zaidi maji ya Serikali kupitia Mamlaka ya Maji ZAWA ambayo pia hayapatikani kikawaida.


Mwandishi wa Makala hii alifika kijijini hapo kuwashuhudia akinamama na watoto wakiendelea kuteseka kupambania maji ya ZAWA.

Vilio vikubwa vilisikika hapa wakilalamika juu ya kadhia ya ukosefu ya wa maji safi na salama kwa muda mrefu sasa na kuelezea juu ya wasi wasi walionao kutokana na maji wanayotumia kutokuwa na uhakika wa afya zao.
Akinamama waliosawijika nyuso zao,walionekana na mwandishi wa makala hii wakiwa na ndoo zao mikononi wakitafakari ni wapi watapata maji kwa ajili ya matumizi muhimu kwa wakati licha ya uchovu waliyoonekana nao.
Sada Rashid Haji mmoja kati ya watu wanaoathiriwa na tatizo hilo alionekana kuwa na furaha baada ya kile alichokuwa akikisubiri kwa hamu kufika yaani vyombo vya habari.
Sada alifunguka kwa uchungu juu ya shida wanayopambana nayo ya ukosefu wa huduma ya maji safi na salama kwa muda mrefu sasa, na haya ndiyo miongoni mwa aliyoyaeleza.
“hali ni kama hii unayoiona, ukiachana na kuwa hayotoki mferejini tukaamua kuja katika visima vyetu vya asili lakini pia ni shida kwani visima ni vidogo na watu ni wengi halafu ukiyaangalia maji yenyewe na mazingira jinsi yalivyo sio safi na salama kwa afya zetu,” alisema.
Aliendelea kueleza kuwa, binadamu kimaumbile lazima apate maji wakikosa hawataishi vizuri na ndio maana sasa wanatumia hayo maji machafu alimradi tu maisha yasonge mbele.
Sada hakusita kuwaomba viongozi wa ngazi ya Majimbo na Serikali kuu kuwatembelea wakajue shida zao ili wawatatulie, alisema kama walivyoweza kuwafika kipindi cha kuomba ridhaa ya kutaka kura basi pia warejee tena kuangalia hali halisi ya maisha yao na sio kusubiri hadi kipindi chengine cha uchaguzi ndio waonekane.
Naye Sabrina Mbarouk Seif mkaazi wa Ndagoni alisema, kwa muda mrefu sasa wanasumbuka kwa kutembea masafa makubwa kutafuta maji na hata hayo wanayoyapata kutoka kwenye visima vyao kutonyweka na hulazimika kutumia kwa sababu hawana pengine pakupata maji safi na salama.

''vidimbwi vyetu ni kama hivi unavyoviona maji hayanyweki lakini twanywa hivyo hivyo,yanaharisha hayo lakini tutafanya nini” alisema Sabrina ambaye ni mja mzito huku akiwa amepakata ndoo akisubiri zamu yake ya kuteka maji ifike.
Aidha anaiomba mamlaka ya maji Zanzibar ZAWA upande wa Pemba, kuwafanyia utaratibu wa kuwapatia maji angalau kwa mgao ili kuwawepusha matatizo ambayo yanaweza kujitokeza ikiwemo maradhi ya mripuko pamoja na vitendo vya ukatili na udhalilishaji vinaweza kutokea hasa nyakati za usiku za utafutaji maji
“Ni heri tuwe tunapata maji kwa zamu, tutajua zamu yetu ni siku fulani kuliko shida hii tunayoipitia tunatoka saa 8 usiku tunaenda kisimani ukifika mwenzako kashafika ana ndoo kumi au zaidi, alielezea Sabrina.
Aidha Sabrina aliongeza, kutokana na hali yake ya uja uzito hawezi kutoka usiku kwenda mabondeni kupanga msongo akihofia kujifungua njiani hivyo hulazimika kuwaomba wasamaria wema wamgaie maji angalau ndoo mbili ili akatumie na watoto wake nyumbani.
Nassor Khamis Abdallah mkaazi wa kijiji cha Kichanjaani Kilimani anaelezea mkasa wa ukosefu wa maji anasema, tatizo hilo limeanzia katika kijiji cha Ndagoni mjini hadi kufikia Mkumbuu na hatua alizozichukuwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa ZAWA ili kuweza kupatiwa msaada lakini hadi sasa tatizo hilo linaendelea.
“mimi mwenyewe ndani ya mwezi huu nilikwenda ZAWA kuripoti na wakaja hadi hapa kisimani tulipo, nikawaonesha maji tunywayo kuwa hayastahiki kwa matumizi ya binaadamu na sio salama na wao waliyaona”, alisema.
Alieleza kuwa hivi karibuni ZAWA walikuja kutengeneza lakini maji yao yalitoka siku moja usiku na vijiji vyengine hayakufika hadi leo hayajatoka tena.
Nassor anasema, ili wapate furaha, kunyeshe mvua ndio angalau hupata maji ambayo wanasema ni safi na salama kwao.

” tunahofu hata kujitokeza masula ya udhalilishaji hususan kwa watoto wa kike kwasababu, wanalazimika kuyafuata maji mabondeni nyakati za usiku ambako ni rahisi kwa mtu mbaya kuwatendea matendo uchafu”alieleza.
Visima ambavyo wanavitumia maarufu visima vya kata mara nyingi urefu wake huwa ni wastani wa nusu pima hadi pima kasoro, huzalisha maji wastani wa ndoo 15 hadi 20 za lita 10, kiasi ambacho hakiwatoshelezi katika matumizi yao ya kila siku.
Mazingira ya visima hivyo sio mazuri hata kidogo kiusalama wa afya kwa matumizi ya kunywa na kupikia, hii ni kwa saba
bu ndani yake huruhusu kupenya na wadudu wabaya kwa afya ya binaadamu kama vile vyoka na wengineo, pia kwa kuwa visima hivi havifunikwi maji majachu na uchafu mwengineo huchanganyika pamoja na kuhatarisha afya za wanyaji wa maji hayo.
Mwandishi wa Makala hii alibisha hodi kwa Sheha wa shehia ya Ndagoni Massoud Ali Mohamed ambae alieleza kulifahamu tatizo hilo kwa wananchi wake, kwasababu amesha elezwa mara kadhaa kuhusu changamoto hiyo, na yeye kama kiongozi wa eneo hilo ameshaliripoti katika mamla husika ambayo Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA)
"walikuja wananchi kunieleza changamoto hii ya maji na nilichukua juhudi za kwenda ZAWA na naamini wanalijiua hili na tayari walishaleta mafundi wao wakiambatana na mafundi kutoka ZECO kuona kwa jinsi gani wanamaliza tatizo hili na juhudi zinaendelea” alieleza sheha huyo.
Kiongozi huyo aliwataka wananchi kuwa watulivu na subra kwani panapotokea hitilafu yeyote ustahamilivu unahitajika huku wenye dhamana hiyo wakiendelea na jitihada za kulipatia ufumbuzi tatizo la maji kwa wananchi hao.
Sheha huyo aliishauri Serikali kuona namna ya kuwachimbia kisima wananchi wa kichanjaani kilimani pamoja na Ndagoni ili kuwapatia wananchi wake huduma hiyo muhimu kwa urahisi na kwa ufanisi zaidi.