Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi ameagiza Wizara ya Afya kuanza haraka majadiliano na Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete JKCI ili huduma za upasuaji wa moyo zianze kutolewa Zanzibar kipindi kifupi kijacho.
Rais Dk.Mwinyi ametoa agizo hilo leo Februari 10,2024 katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip wakati akifunga Mkutano wa Kimataifa wa magonjwa ya moyo ulioandaliwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete JKCI na Wizara ya Afya Zanzibar ambao umewashirikisha Wataalamu wa Afya ndani na nje ya nchini.
Dk. Mwinyi amesema dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuimarisha huduma za Afya kwa kutoa matibabu ya magonjwa ya moyo na kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika.
"Kwa madhumuni ya kuboresha huduma za magonjwa ya mfumo wa moyo na mishipa ya Damu tupo tayari kushirikiana na Taasisi ya JKCI na Taasisi nyingine hivyo niagize muanze haraka majadiliano na huduma za upasuaji zianze kutolewa kwa kipindi kifupi kijacho," amesema.
Aidha Dk. Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo tayari kukuza ushirikiano na kutenga rasilimali zilizopo ili kuendeleza juhudi za utafiti, kinga na matibabu ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu.
"Tunayo matumaini makubwa kuwa kwa pamoja, tunaweza kuleta mabadiliko makubwa katika kuboresha matokeo ya athari za magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kwa kila mmoja wetu hapa nchini" Ameeleza.
Ameeleza kuwa, Serikali inafanya juhudi ili kuhakikisha Wananchi wengi zaidi wenye tatizo la maradhi ya moyo wanapata faraja kwa kuishi maisha ya furaha na siha kwa kutekeleza mkakati wa Taifa wa kupunguza matumizi ya vyakula vinavyohusishwa na sababu ya magonjwa hayo.
"Mkakati huu ni pamoja na kukuza Afya kwa kuhimiza Wananchi kutumia vyakula vinavyoshauriwa na wataalamu na kuwa na kawaida ya kufanya mazoezi," amefafanua.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete JKCI Dkt. Peter Kisenge ameeleza kuwa Mkutano huo umewashirikisha zaidi ya Wataalamu 500 Tanzania na Wataalamu zaidi ya 40 kutoka kutoka mataifa zaidi ya 34.
"Mkutano huu umewashirikisha Wataalamu kutoka mataifa mbalimbali ambapo Zanzibar zaidi ya madaktari 100 wameshiriki," ameeleza.
Hata hivyo ameeleza kuwa, baada ya Mkutano huo wa Kimataifa taasisi ya JKCI inakwenda kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuanzisha Taasisi ya moyo na kusaidia Wazanzibar.
"Tunazungumza na Mhe.Rais Dkt Mwinyi sasa tunakwenda kuanzisha Taasisi ya Moyo hapa Zanzibar itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za kujibu nje ya nchi," ameeleza.
0 Comments