Imeandikwa na Ibrahim Mustafa, SUZA
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma ameliomba Jeshi la Polisi Zanzibar kushughulikia haraka kesi ya mtoto mwemye miaka mitatu (3) ambae amefanyiwa kitendo cha ukatili wa kupigwa hadi kuvunjwa mkono na babaake wa kambo Lukman Shaffii (27) Mkaazi wa Magomeni Unguja, Mkoa wa Mjini Magharib.
Kauli hiyo ameitowa wakati alipofika kumkagua mtoto huyo huko Maungani Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, ambapo mtoto huyo anaishi na bibi yake kwa sasa baada ya kutokea tukio hilo la ukatili wa kinyama.
Amesema endapo Jeshi la Polishi litashughulikia kesi hiyo kwa haraka na uadilifu basi sheria itafuata mkondo wake na itakua funzo kwa wazazi wengine wenye tabia kama hiyo, na hatua hiyo itawafunza kujua kama mtoto ni wa Serikali.
“Naliomba Jeshi la Polisi kushughulikia ipasavyo kesi za ukatili na udhalilishaji wa watoto katika jamii ili kuweza kuona vitendo hivyo vinapungua kwani watoto ndio taifa bora la badaae” Amesema Waziri Riziki.
Waziri Riziki amesema uwepo wa vitendo hivyo vya udhalilishaji vinarudisha nyuma upatikanaji wa maendeleo hapa nchini. Hivyo amewaomba wazazi na walezi katika kuripoti bila ya kuona muhali katika jamii inayowazunguuka.
“Naisisitiza jamii kupiga vita vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kwani vitendo hivyo vinachangia kuongezeka kwa uovu katika jamii, mtoto sio kama hapigwi bali kunataratibu za kumuonya mtoto” Amesema Riziki.
Naye Afisa Hifadhi ya mtoto Idara ya Ustawi wa Jamii na Wazee Ndugu Ramadhani Mohammed Ramadhani amesema hali waliyomkutanayo mtoto huyo haikuwaridhisha na tayari wameshamshughulikia kwa kumpatia huduma zinazo stahiki pia wameahidi kuendelea kuwachukulia hatua wazazi wenye tabia kama hizo ili kuwa fundisho kwa wengine.
chanzo:pembatoday
0 Comments