NA-FATMA SULEIMAN , PEMBA
Wananchi wa kisiwa Pemba waingiwa na hofu juu ya uwepo wa mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hali ambayo imepelekea maisha yao kuwa magumu kutokana na mazao yao kuharibika.
Walisema mvua ni neema kwani huhuisha miti mbali mbali ikiwemo mikarafuu, minazi, na miti mengine, lakini kutokana na mvua kwa msimu huu kuwa kubwa hali hiyo kubadilika na kuwa vilio kwani bei za bidhaa kupanda na mazao ya mboga mboga kuharibika mashambani .
Moh’d Rashid Ali mwananchi mkaazi wa Machomane alieleza hofu yao kubwa kutokana na mvua hizi zinazoendelea kunyesha ni bei za bidhaa zitaongezeka mara dufu huku na mashambani mazao kupungua kutokana na kupukutika na baadhi ya mazao kuoza.
Alisema kuwa licha ya mvua kurutubisha vilimo na kuondosha joto lakini zinapozidi athari zake huwa nyingi kulikoni faida.
"Mvua ni neema na huwa tunalihitaji lakini inapo kuwa kubwa kama hivi kila kitu kinaharibika kwa kuoza," alieleza.
Mmoja ya wakulima ambae amekumbwa na kadhia ya kuharibikiwa na kilimo chake anaetambulika kwa jina la Kombo Mussa Kombo kutoka kijiji cha Mbuyudoda kilichopo Kangagani alisema kuwa zaidi ya shilingi milioni sita amezipoteza kutokana na kilimo chake cha mboga mboga kuharibika ikiwemo mchicha, pamoja na tungule kupasuka na kuoza , mabilingani kupukutika pamoja na mahindi.
Alieleza eka mzima ambayo alitarajia kuihudumikia familia yake ikiwemo kuilisha na kusomesha watoto imepotea hivyo ameiomba Serikali kupitia wizara ya kilimo kuwatembelea na kuwafariji ili kuona athari zilizojitokeza kwa wakulima kisiwani Pemba.
"Tunaiomba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kututembelea ili waweze kuona athari tulizopata kutokana na Mvua kubwa ", alieleza.
Kwa upande wake mfanya biashara Saidi Abdalla Said alisema uwepo wa mvua kubwa umepelekea biashara kushuka na bidhaa kuongezeka bei ikiwemo Tungule huku lawama kwa wananchi zikiongezeka kutokana na mfumuko wa bei .
Mdhamini wa wizara ya kilimo Pemba Idrisa Hassan Abdallah alisema kuwepo kwa mvua hizi Pemba zipo athari za wazi ambazo zimetokea katika wilaya zote nne ikiwemo mashamba kuingia maji yenye taka (mafuriko madogo) mashamba kushambuliwa na wadudu ikiwemo nzige , mboga mboga kupasuka na kuoza hasa katika ukanda wa mashariki Alisema uwepo wa mtiririko wa mvua ambao sio wa kawaida inakadiriwa sio chini ya asilimia tano ya athari zilizojitokeza na baadhi ya mshamba kuharibika ikiwemo wilaya ya mkoani kuingiwa na nzige , mashamba ya Kengeja ,Chumbageni , Ukutini na mashamba yaliopo Chambani kupata mafuriko madogo na kushambuliwa na wadudu.
Alisema katika wilaya ya Chake Chake pia mafuriko yaliweza kutokea katika mashamba pamoja na kushambuliwa na wadudu ikiwemo Vitongoji ,Pujini ,Kwale na Madungu.
Aidha aliwashauri wakulima kisiwani Pemba katika kipindi cha mvua kama hizi kulima vilimo vinavyoendana kulingana na mvua ikiwemo vilimo vya muda mrefu ambapo na kwa upande wa mashariki kuotesha miti inayostawi ili kupunguza athari katika msimu wa mvua .
‘’ Nawashauri Wakulima katika kipindi kama hichi cha mvua kubwa ambazo sio za kawaida kulima vilimo vya muda mrefu ili kupunguza athari kama hizi’’, alieleza.
Hata hivyo alisema wizara imetoa ruzuku kwa wakulima wote katika kuwapunguzia mzigo hivyo kuwataka wakulima kwenda kuchukua mbolea ili kutimiza malengo ya Raisi wa Zanzibar Dk, Hussein Ali Mwinyi ya kuwakwamua wakulima katika hali duni. MWISHO.
0 Comments