Mjane wa watoto saba aomba msaada wa kuezekewa, ni baada ya kuachwa yeye na mume wake


MJANE mwenye watoto saba amewaomba wahisani na watu wenye uwezo, kumpa msaada wa bati na miti, kwa ajili ya kuezekea nyumba yake, ili apate kustirika na watoto wake.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi nyumbani kijiji cha Madenjani Wilaya ya Wete Pemba, mama Rehema Salum Issa ‘Vumilia’ alisema nyumba anayokaa imeshakua mbovu, mvua yote inamnyeshea ndani mwake.

Alisema anapatashida kwani mvua inaponyesha husimama barazani hata kama ni usiku mkubwa,kwa vile ndani hujaa maji na kukosa sehemu salama.

‘’Ndani hujaa maji, vitanda vyangu vyote vimeshaharibika sina hata pakulala na watoto wangu saba, naomba binadamu wezangu munisaidie nateseka,’’alilalamika.





Alieleza tayari alishajenga vyumba viwili vya matufali, ingawa ameshindwa kuezeka, hivyo ameomba asaidiwe bati pamoja na miti kwa ajili ya kuezekea, ili apate kuishi sehemu anapostahiki binadamu.

Alifahamisha kuwa mume wake amemuacha na watoto saba, na kumuachia mzigo wa malezi, na kwa sasa hamuulizi huduma ya aina yoyote kwa watoto wao.

Alisema amesharipoti maeneo mbalimbali ikiwemo ustawi wa jamii wilaya ya Wete pamoja wizara ya Maendeleo ya Jamii, ingawa hakuna hatua aliyochukuliwa.

Katika hatua nyingine, alimuomba sheha wa shehia kumuingiza katika miradi ya maendelo ambayo inakuja, ili iweze kuwasaidia kumoa uhakika wa chakula.

Mtoto wa mjane huyo, Bilali Mohamed Rashid (16) anaesoma darasa la kumi, anasema ndoto zake za baadae ni waziri wa Fedha.

Alifahamisha kuwa, kitendo chakukosa huduma kutoka kwa baba yao kinamuathiri, kwani wanashindwa kupata huduma wanazotakiwa, kutoka kwa wazazi wao, ndio maana anasoma kwa bidii.

‘’Tunakwenda skuli hatuna viatu mvua kama hizi, hatuli chochote, na tukirudi tunakuta hamna kitu, kwakweli hilo linaniathiri na linaweza kupelekea kushindwa kutimiza ndoto zangu,’’alifafanua.

Nae Nasra Mohamed Rashid ambae anasoma darasa la pili  amesema ipo haja serikali, kuweka adhabu kali kwa wazazi pindi wakizitekeleza familia zao.

Baba mzazi huyo ambae ni mstaafu wa JWTZ, Mohamed Rashid alipopigiwa simu na mwandishi wa habari alisema, sio kwasababu hataki kuwahudumia watoto wake, bali ni kutokana na halingumu ya maisha yake.

‘’Ni kweli mstaafu, ingawa ninachokipata, hakitoshelizi kukigawa nyumba mbili, inafaa kama hawa watoto atanirejeshea nipate kuwahudumia kwa chungu kimoja,’’alisema.

Mwana harakati wa kulinda na kutetea haki za watoto Pemba Tatu Abdalla Msellem alisema kuvunjika kwa ndoa isiwe sababu ya kila mzazi kufumbia macho wajibu wake wa malezi na huduma kwa watoto.

Sheikh Said Ahmed Mohamed  kutoka Ofisi ya Mufti Pembaanasema kisheria mwanamme ndie mwenye jukumu la kutoa matunzo kwa familia yake, hata baada ya kuvunjika kwa ndoa.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki lililopo Mkungu Malofa Chakechake Robert Miguwa Ndalami, anasema dini imeelekeza wanaume watoe huduma stahiki kwa familia zao akiwemo mama na watoto.

Kwa mujibu wa Ripoti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii jinsia, wazee, na watoto ya mwaka 2024-2025 kulipokelewa  jumla ya malalamiko 691 (Unguja 313 na Pemba 378) yanayohusu ukiukwaji wa haki za watoto, mivutano ya malezi,  na matunzo ya watoto.


Post a Comment

0 Comments